loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ndege iliyozuiliwa Afrika Kusini kurejeshwa

SERIKALI imewaondoa hofu Watanzania kuwa ndege ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Air Bus A220-300, inayoshikiliwa nchini Afrika Kusini kwa amri ya Mahakama Kuu, itarejea nchini.

Imewataka wananchi kutokuwa na hofu kuwa huenda ndege hiyo ikauzwa, ili kufidia deni inalodaiwa Serikali, lililosababisha ndege hiyo kukamatwa nchini humo.

Akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mjini Dodoma juzi, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas, alisema wanasheria wa Tanzania wakiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi, tayari wameshawasili Afrika Kusini na wameshaingia kazini, kuichambua kesi hiyo ili kuona ni eneo gani ambalo wanaweza kuchukua hatua, zitakazowasaidia kupambana mahakamani ili itarudi na kuendelea na safari zake kama kawaida.

Aeleza sababu za kushikiliwa Dk Abbas alisema kushikiliwa kwa ndege hiyo, kunatokana na kesi iliyokuwapo tangu miaka ya 1980 kati ya Serikali ya Tanzania na raia wa Afrika Kusini, Hermanus Steyn ambaye mali zake zilitaifishwa na serikali yakiwamo mashamba, mifugo na nyinginezo. Alisema utaifishwaji huo, uliridhiwa na Steyn mwenyewe,lakini alitaka alipwe fidia.

“Kesi hii ni madai ya muda mrefu ya fidia ya ardhi iliyotwaliwa tangu miaka ya 1980, hivyo siyo kesi kwamba ni ATCL ndiyo inadaiwa, hapana. Tunaipambania ndege hii kwa maslahi ya Taifa letu na tuna amini siku moja itarudi kuendelea na shughuli zake za kawaida,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk Abbas, suala hilo lilikuwa linafanyiwa kazi na serikali za awamu zote, lakini katika miaka ya 1990 serikali na mkulima huyo, walikubaliana kiwango cha fidia, ambacho angelipwa. Hata hivyo, alisema baadaye yalitokea mabishano, hivyo miaka ya 2000 walikubaliana tena na hatimaye Serikali ya Awamu ya Nne ilimlipa kiasi kikubwa cha fidia, kilichotakiwa kisheria na kiasi kidogo ndicho kilichobaki.

Alisema msingi wa kesi hiyo, kwa sasa unatokana na uamuzi wa Steyn kuiomba Mahakama Kuu ya Afrika Kusini, imsaidie kutekeleza hukumu ili alipwe kiasi cha fidia kilichobaki.

Msemaji Mkuu huyo wa Serikali alisema zipo nchi ambazo kwa taratibu za kisheria, zinaweza kuomba hukumu ya nchi nyingine.

“Hukumu tayari tunayo na ukiisoma ina mambo makubwa mawili ambayo Watanzania wanapaswa kuyaelewa. Kesi ya msingi haijasikilizwa, kama nilivyosema ametumia sheria za Afrika Kusini kuomba kutekeleza hukumu ya nchi nyingine, kwa hiyo ana hukumu ambayo ilishapatikana huku kwetu, lakini akaomba itekelezwe kule Afrika Kusini kwa maana ya kile kiasi kilichobaki.

“Kwa hiyo kesi ya msingi, ya hicho kiasi kilichobaki, kwamba sisi tutakikubali tukilipe au tunapingana nacho haijasikilizwa, isipokuwa aliomba maombi madogo ambayo yana taratibu mbili, ambazo mnaweza mkasikilizwa wote au upande mmoja tu ukasikilizwa, kwa hiyo yeye alichagua asikilizwe na Mahakama bila sisi kuwapo, kwa hiyo hiki ndicho kilichofanyika” alisema.

Dk Abbas alisema wataangalia sheria inasemaje, lakini kutokana na ufahamu alionao kama ofisa wa Mahakama kutokana na fani ya uwakili alionayo, anajua kwamba hukumu ambayo imetolewa upande mmoja, inaweza kubatilishwa. Alisema kwa kuwa Tanzania kwa sasa ndiyo inaongoza Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), lakini pia kwa kuwa Serikali inaheshimu utawala wa sheria, katika suala hilo sheria itafuata mkondo wake.

Alisema kwamba watahakikisha wanasimamia maslahi ya Taifa ili ndege hiyo irudi na kuendelea na safari zake. Alipopigiwa simu jana na gazeti hili kuhusu suala hilo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema hawezi kuongelea kwenye simu, bali apelekewe maswali kwa njia ya maandishi, akisema kuna baadhi ya vyombo vya habari, vilipotosha taarifa yake juu ya sakata hilo.

Aidha, juhudi za Habari- Leo kumpata Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Kilangi ambaye yuko Afrika Kusini kufuatilia suala hilo, ziligonga mwamba kutokana na simu yake kutopatikana na hewani na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno kwa njia ya Whatsapp, hadi tunakwenda mitamboni jana alikuwa hajajibu.

Inadaiwa Steyn alipata kumiliki mashamba hapa nchini miaka kadhaa iliyopita, lakini baadaye yalitaifishwa na serikali na kisha akafungua kesi mahakamani, akidai kulipwa fidia. Inadaiwa mwaka 1994 iliamriwa na Mahakama Kuu kuwa anapaswa kulipwa fidia ya Dola za Marekani milioni 36. Lakini, baada ya mazungumzo alikubali kulipwa Dola milioni 30 na mwaka 2012 alilipwa Dola milioni 20 na kubaki Dola milioni 10, ambazo ndiyo zimeibua sakata lote hilo la kuzuiwa ndege hiyo ya Tanzania.

MGOMBEA urais wa ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi

Magufuli: Nataka kumalizia kazi

masaa 14 yaliyopita Magnus Mahenge, Dodoma

MGOMBEA urais wa ...

Wanawake waihakikishia CCM ushindi

masaa 14 yaliyopita Magnus Mahenge, Dodoma

 

Waziri aagiza mifumo ya fedha ipunguze rushwa

masaa 16 yaliyopita Mwandishi Maalumu, Simiyu

WAZIRI ...