loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Fursa katika hifadhi mpya ya Nyerere

IJUMAA iliyopita tulianza kuangalia makala haya kuhusu hatua ya Rais John Magufuli kuagiza kutengwa kwa eneo la Pori la Akiba la Selous ili kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Julius Nyerere.

Tuliona kwamba kuna uwezekano mkubwa wa hifadhi hii kuwa kivutio kikubwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa karibu na jiji la Dar es Salaam na kuwa na uasili wa kutotumika sana kwa shughuli za kitalii hadi sasa.

Tukaona kwamba uwepo wa aina nyingi za wanyamapori, hifadhi kuwa eneo la Urithi wa Dunia na matukio ya kihistoria yaliyozaa majina kama Selous na Stiegler, yanaifanya hifadhi hii kuwa eneo ambalo wengi watapenda kwenda.

Taarifa zilizopo zinaonesha kwamba awali pori la Selous lilikuwa na kilomita za mraba 40,000 lakini likapanuliwa na serikali ya kikoloni. Inaelezwa kwamba uliwahi kuzuka ugonjwa wa malale kwenye maeneo ya Selous kati ya mwaka 1930 na mwaka 1940 na kusababisha utawala wa kikoloni kuwaondoa watu eneo la Selous na kuwaweka eneo salama.

Njia iliyotumika kuwafanya watu wasirejee katika eneo hilo ‘hatarishi’ kutokana na ugonjwa huo inaelezwa kwamba ilikuwa ni kumega ardhi za vijiji na kuwa sehemu ya pori la Selous na hivyo ukubwa wa pori ukaendelea kuongezeka hadi kufikia ukubwa wa sasa wa takribani kilometa za mraba 50,000. Bruce Kinloch aliyekuwa Mkurugenzi wa Wanyamapori wa utawala wa kikoloni, miaka michache kabla ya uhuru wa Tanganyika alianzisha uwindaji wa kulipia ulioiingiza fedha serikali hiyo ya kikoloni.

Fedha hizo zilitumika kujenga miundombinu kwenye pori la Selous ili kuwalinda wanyamapori dhidi ya majangili na uendeshaji wa pori. Baadae eneo la kaskazini likageuzwa kutoka eneo la uwindaji na kuwa eneo la utalii wa picha. Vitendo vya ujangili vilivyoshamiri miaka ya 1972 viliteketeza idadi kubwa ya tembo katika pori la Selous ambapo inakadiriwa tembo kati ya 120,000 hadi 30,000 waliuawa. Kuanzia miaka ya 1990 hadi leo vitendo vya ujangili vilipodhibitiwa wanyamapori wameongezeka kwa wingi sana katika pori hilo.

Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Julius Nyerere sasa kutaleta mwelekeo mpya wa shughuli za utalii kwenye eneo la Selous pamoja na ukanda wa utalii wa kusini. Idadi kubwa ya watalii wa ndani na wale wa nje ya nchi wataweza kuitembelea hifadhi hii kwani kwa sasa ni idadi ndogo sana ya watalii wa ndani wanaotembelea eneo hili. Faida zitakazotokana na kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Julius Nyerere ni pamoja na kuboreka kwa miumdombinu ya barabara ndani ya hifadhi na barabara ya kuingia hifadhini kutokea Kibiti ambayo Rais Magufuli amesema itajengwa.

Barabara hii licha ya kurahisisha usafiri wa watalii kuelekea hifadhini pia itachochea maendeleo kwenye maeneo ambayo inapita na kusababisha vijiji vinavyopitiwa na barabara hii kukua kwa kasi kutokana na kukua kwa shughuli za kiuchumi kwenye vijiji hivyo. Wafugaji na wakulima wanatazamiwa kupata soko la mazao ya matunda yao, mbogamboga, nafaka, nyama, maziwa na mayai kwa watalii na watu wengine wanaofanya shughuli za utalii.

Kwa hatua ya kuanzishwa kwa hifadhi hii inatazamiwa kwamba mahoteli, migahawa ya kitalii, nyumba za wageni na maduka ya bidhaa za watalii yataanzishwa na hivyo kukuza uchumi wa eneo hili la utalii wa ukanda wa kusini. Mabenki, maduka ya fedha za kigeni na makampuni ya simu yatapeleka huduma zao katika hifadhi na hivyo shughuli za kibiashara zitakua na ajira zitaongezeka kwenye maeneo husika.

Kimsingi, eneo lolote la utalii hufanya vizuri iwapo linafikika vizuri kwa maana ya kuwa na usafiri wa uhakika wa kumleta mtalii kutoka nchini kwake hadi Tanzania na usafiri wa ndani kuelekea hifadhini. Kwa kuwa sasa nchi ina ndege zake, kuna uhakika wa idadi ya watalii kuongezeka. Barabara kutoka Kibiti hadi Rufiji River Camp na zinginezo zinazoingia hifadhini zitarahisisha watalii kufika kwenye hifadhi.

Eneo la utalii pia litafanya vizuri iwapo kuna malazi yenye ubora kwa ajili ya watalii na hivyo kuanzishwa kwa hifadhi hii kunatoa fursa kwa wawekezaji kuchangamkia ujenzi wa malazi kwenye maeneo ya jirani na hifadhi. Eneo la utalii pia hufanya vizuri iwapo kuna huduma muhimu zinazowezesha mtalii kuendesha maisha yake kama kawaida na huduma hizi ni kama zilivyotajwa hapo juu ikiwa ni pamoja na huduma za afya na usalama.

Yote haya yanatoa fursa pia kwa wawekezaji kuwekeza kwenye biashara ya huduma hizi kwenye vijiji jirani na hifadhi. Shughuli za utalii zinazotumiwa kuwepo kwenye hifadhi hii ni pamoja na utalii kwa kutumia gari, utalii wa kutembea, utalii wa kutumia boti, uvuvi na mapumziko ya hotelini. Kama ilivyoelezwa katika makala iliyopita, Hifadhi ya Taifa ya Julius Nyerere ipo kwenye eneo la Urithi wa Dunia linalotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Tanzania ina maeneo sita ya urithi wa Dunia ambayo manne ni ya asili na mawili ni ya utamaduni. Maeneo ya Urithi wa Dunia ambayo ni ya asili ni eneo la Hifadhi la Ngorongoro (NCAA), Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba la Selous na Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro. Maeneo ya Urithi wa Dunia ya kitamaduni ni mji mkongwe wa Zanzibar na masalia ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara huko huko Kilwa.

Katika Afrika kuna nchi nne zenye maeneo mengi ya kuvutia ya Urithi wa Dunia. Nchi hizo ni Tunisia yenye maeneo manane, Algeria na Ethiopia zenye maeneo saba kila moja na Morocco na Tanzania zenye maeneo sita kila moja.

Hifadhi ya Taifa ya Julius Nyerere iliyo ndani ya eneo la Urithi wa Dunia la Selous bila shaka itachochea shughuli za utalii katika ukanda wa utalii wa kusini mwa Tanzania. Itakuza sekta ya malazi katika miji ya jirani na hifadhi na itasisimua biashara katika Jiji la Dar es Salaam hasa biashara ya malazi na maduka ya bidhaa za watalii kama vile vinyago, mavazi, vito, nk) Hifadhi hii pia itakuza shughuli za usafiri na utalii katika Jiji la Dar es Salaam kama vile kutembelea maeneo ya makumbusho na maeneo ya kihistoria na fukwe za Dar es Salaam. Jiji la Dar es salaam pia linatazamiwa kunufaika kwa kuwa mtalii kutoka nje atatua uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere na kufanya malazi kwenye hoteli za jiji hilo kabla ya kwenda Hifadhi ya Julius Nyerere na hifadhi zingine za Ukanda wa Utalii wa Kusini.

Kwa kuwa mtalii kwa kawaida hutembelea hifadhi mbili au tatu pamoja na maeneo ya fukwe, hifadhi zingine kama Mikumi, Udzungwa na Ruaha nazo zitafaidika. Maeneo ya utalii ya fukwe ya Mafia, Kilwa, Saadani na Zanzibar nayo yatanufaika. Kuwepo kwa ndege za uhakika hapa nchini ni kichocheo kizuri cha ongezeko la watalii sambamba na uanzishwaji wa hifadhi zingine mpya za Chato-Burigi na hii ya Nyerere. Mtalii anavutiwa zaidi kuona kitu kipya.

Kwa kuwa wengi wamekuja mara mbili au tatu na kukutana na vitu vile vile, uanzishaji wa hifadhi mpya kutawavutia hata watalii waliokwishawahi kuja Tanzania na kwenda Serengeti, Ngorongoro na Lake Manyara, sasa kwenda Burigi-Chato au Nyerere. Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) linapaswa kuanzisha safari mahususi zenye lengo la kuchochea utalii kwenye maeneo ambayo utalii wake ndio unakua kama vile safari za ndege kutoka Dar es Salaam kupitia Mafia kwenda Mtwara, vivyo hivyo na kurejea angalau mara mbili au tatu kwa wiki nyakati za jioni.

Hii itakuza utalii na biashara kwenye kisiwa cha Mafia. Utalii wa ndani pia utakua kwa maana ya mwananchi wa Mtwara au Dar es Salaam kuweza kwenda kufanya utalii na kupumzika Mafia kwa kuwa kutakuwa na usafiri wa uhakika na wa gharama nafuu. Mbali na kukuza utalii wa kusini, safari hizi pia zitamwezesha mfanyabiashara aliyetua kwa ndege ya asubuhi Mtwara kurudi na ndege ya jioni ya kupitia Mafia bila ya kuhitajika kulala Mtwara au Dar es Salaam.

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Ernest Makunga

1 Comments

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi