loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

KUKAMATWA KWA NDEGE YA ATCL…Tutofautishe mambo ya siasa na utaifa

KATIKA makala zangu hizi kwa ‘Maslahi ya Taifa’, leo nazungumzia somo la uzalendo kwa nchi yetu ambayo ni urithi aliotupa Mungu wetu. Kwamba ni muhimu kutofautisha siku zote mambo ya kisiasa na yale yanayohusu utaifa wetu.

Nimejiuliza sana kwamba inakuwaje nchi yako inapatwa na majanga, halafu wewe unafurahi. Huu ni uzalendo wa aina gani? Huu ni uzalendo wa ajabu kabisa kuwahi kutokea.

Baada ya kupatikana kwa taarifa mbaya ya kukamatwa kwa ndege yetu na kuzuiliwa Afrika Kusini, taarifa hiyo ilipokewa kwa mshtuko na kuzua mijadala mingi kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii.

Kuna baadhi ya Watanzania wenzetu, badala ya kusikitika na kuwa wamoja katika hili na wenzao wanaosikitika, wao wanafurahia kukamatwa kwa ndege hii, hali inayoonesha kwamba wanaiombea mabaya nchi yetu.

Hawa kwa kweli ni watu wa ajabu sana. Mtoto mtundu ukiwa unamchapa sana, badala ya kumwelimisha au kumpa adhabu mbadala, mwisho wake huyo mtoto anakuwa sugu, anakuwa nunda, anakuwa yuko tayari kufanya lolote bila kujali atachapwa au la. Hivyo inawezekana huku ‘kubana kwa vyuma’ kumewafanya baadhi ya Watanzania wenzetu kuwa manunda wanaofurahia majanga kwa taifa lao.

Mtu yeyote anayefurahia majanga sio tu ya binadamu mwingine, bali kufurahia mateso ya kiumbe chochote, anachofanya sio ubinadamu bali ni unyama. Watu wa aina hii ambao kwa lugha ya Kiingereza wanaitwa sadists, hupata raha kwa mateso ya wengine.

Rais John Magufuli aliwahi kuwataka Watanzania kujiandaa na vita ya uchumi ambayo hakuna shaka kwamba tumeanza kupambana nayo lakini katika hali hii ya wenzetu kushangilia majanga ambayo taifa linapata, basi vita hii itatusumbua sana. Katika hali kama hii, Tanzania kama taifa ina haja kubwa sasa ya kujitathimini na ikibidi kuanza kufundisha somo la uzalendo katika mitaala yetu ili kukuza uzalendo wetu kwa taifa letu.

Nchi inatakiwa kufanya kampeni ya uhamasishaji uzalendo kwa kutoa elimu ya uraia ili jamii iweze kutenganisha matukio ya kisiasa na matukio ya kitaifa. Katika matukio ya kisiasa kwa nchi zinazojali utaifa wao, watu wanajiunga na itikadi za vyama tofauti lakini kwenye matukio ya kitaifa wanaungana na kuwa pamoja na hivyo ndivyo tunapaswa kuwa Watanzania kwa sababu suala la kukamatwa kwa ndege lina maslahi kwa taifa.

Japo Rais Magufuli ni mwana CCM na aligombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, baada ya kushinda na kuunda serikali sasa ni Rais wa Watanzania. Lakini kwa bahati mbaya sana kuna watu wakiwemo wapinzani wanamwona kama Rais wa CCM.

Hawa ndio bado wanaiona serikali ya Tanzania kama ni serikali ya CCM na wanaona kila kitu kinachofanywa na serikali eti ni kwa ajili ya CCM na hivyo mafanikio yoyote ya Rais Magufuli na serikali yake, wanayahesabu ni mafanikio ya CCM na hivyo nchi ikikutwa na majanga yoyote, wao wanashangilia wakihesabu ni majanga kwa CCM.

Huu ni mtazamo finyu na potofu sana kwa sababu tunaona manufaa ya miradi na mipango inayofanywa na serikali iliyoko madarakani kama CCM ilivyoahidi kwenye ilani yake ya uchaguzi kwa Watanzania wote na siyo kwa wana CCM pekee.

Kwani kuna ubaguzi wowote kati ya mwana-CCM na asiye mwana-CCM katika kupita kwenye barabara ya juu (flyover) ya Mfugale pale Tazara? Kuna ubaguzi wowote katika watu wanaopaswa kusafiri na ndege za Shirila la Ndege la Taifa (ATCL)?”

Je, faida inayopatikana kupitia uwepo wa ndege hizi, iwe ni kutokana na kodi au vinginevyo si ndio inayojenga barabara, kulipia elimu bure na huduma nyingine? Ukweli unabaki kwamba, japo mgombea anadhaminiwa na chama cha siasa na kupendekezwa na chama cha siasa, baada ya kupitishwa na NEC kuwa mgombea, huyu sasa anakuwa ni mgombea wa taifa.

Huyu anachaguliwa na Watanzania wote, wanachama wa chama chake na wasio wa chama chake alimradi wakiridhika na uwezo wake na sera za chama chake. Na akishachaguliwa anakuwa kiongozi wa taifa, ni kiongozi wa wote na sio kiongozi wa chama chake. Hivyo, Rais Magufuli japo ni mwana CCM, sio Rais wa CCM bali ni rais wa Watanzania wote wakiwemo hao wapinzani, hivyo majanga yoyote yatakayoikumba nchi sio majanga kwa Rais Magufuli, na siyo serikali yake pekee bali ni majanga kwa Tanzania nzima.

Kwamba watakaoathirika na majanga haya sio Rais Magufuli na serikali ya CCM pekee bali nchi nzima ya Tanzania kama taifa tukiwemo sisi Watanzania wote, uwe ni CCM, upinzani au huna chama. Uwe ni mkulima, mfanyakazi, uwe hupandi ndege au unapanda basi nchi ikikumbwa na majanga kama hili la kukamatwa na kushikiliwa kwa ndege yetu, ni janga la kitaifa na sote tutaathirika.

Baadhi ya viongozi wa dini wanatufundisha kwamba kiongozi wa umma haombewi dua mbaya na majanga bali anaombewa katika kipindi chake cha uongozi atende mema na pia Mwenyezi Mungu amfanye kuwa mwadilifu muda wote kwa manufaa yake na anaowaongoza.

Wanasema kumwombea mabaya kiongozi wa umma ni sawa na kumwombea dua mbaya rubani wa ndege ambayo na wewe umo ukisafiri ili aangushe hiyo ndege! Uzalendo wa kweli kwa nchi yako ni pamoja na kuitakia mema na mafanikio serikali iliyoko madarakani na kazi ya upinzani katika kipindi hiki ni kueleza namna ambavyo wenyewe unadhani ungefanya vizuri zaidi.

Yaani kama ni kununua ndege tunatazamia upinzani ueleze jinsi ambavyo wenyewe ungeweza kununua ndege nyingi na bora zaidi huku ukieleza upungufu wa sasa kama upo. Kimsingi, kama ambavyo amekuwa akisema Rais Magufuli, maendeleo hayana vyama na uzalendo wa kweli kwa taifa pia hauna vyama. Sisi ni Watazania, sawa na mwili mmoja na hivyo kiungo kimoja kinapopata shida lazima wote tujisikie vibaya.

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: Pascal Mayalla

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi