loader
Picha

MWAMBESI Msitu uliopandishwa hadhi kuongeza uhifadhi

MSITU wa Mwambesi, uliopo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma ulioanzishwa mwaka 1956, ulikuwa msitu wa kawaida lakini kutokana na umuhimu wake ikiwemo kuwa na miti adimu duniani, mwaka 2017/2018 ulipandishwa hadhi ya kuwa msitu wa hifadhi ya taifa.

Meneja wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani Tunduru, Denis Mwangama, anasema msitu huo umepandishwa hadhi ili kuongeza uhifadhi zaidi kutokana na kuwa na utajiri wa viumbe vya kipekee duniani wakiwamo wanyama, ndege na mimea.

Anawataja wanyama waliopo katika msitu huo uliopo kando mwa mto Ruvuma kuwa ni simba, tembo, chui, kuro, jamii mbalimbali za nyani, jamii za swala, nyati na wanyama wengine.

Ndege kutoka Madagascar Mwangama anasema katika msitu wa Mwambesi kuna jamii ya ndege maarufu duniani anayeitwa Pentiole ambaye utafiti uliofanywa na PALMS Foundation mwaka 2015 umebaini kuwa ndege huyo amehamia hapo kutoka nchini Madagascar baada ya mazingira aliyokuwa anaishi huko kuharibiwa na shughuli za kibinadamu.

Kwa mujibu wa Mwangama, ndege huyo ana tabia ya kuzamia samaki kwenye maji na kwamba ndege hao wanapenda kuishi kwenye maporomoko ya mto Ruvuma yanayoitwa Sunda yaliyopo ndani ya hifadhi hiyo.

Mwangama anasema ndege huyo huogolea kulingana na mawimbi ya maji yadondokayo kwenye maporomoko hayo akitafuta mawindo yake ya samaki ambayo ndicho chakula chake pekee.

Licha ya ndege huyo, Mwangama anayataja maporomoko ya Sunda kuwa ni miongoni mwa vivutio vya utalii katika hifadhi ya Mwambesi. Anasema katika maporomoko hayo kuna mapango yaliyotumika kama sehemu ya kujificha wakati wa vita ya Majimaji kati ya mwaka 1905 hadi 1907.

Mto huu ndio uliokuwa ukitumika kwenye vita vya Majimaji. Watu wa makabila ya ukanda wa kusini hususani Wangoni walitumia maji yake (kiimani) katika kuzimia silaha za moto chini ya uongozi wa Kinjeketile Ngwale.

Pia eneo hilo linaaminika Wajerumani walitumia kama njia kubwa wakitokea Msumbiji katika biashara ya meno ya Tembo na Waarabu walipita pembezoni mwa mto huo kuwapitisha watumwa.

Hata hivyo anasema awali kabla ya serikali kuamua msitu huo kuwa msitu wa hifadhi, kulikuwa na vitalu vya uwindaji wa kitalii na ndani ya msitu kulikuwa na kambi ya wawindaji iliyoitwa Big Game.

Kulikuwa pia na kampuni ya uwindaji iliyoitwa Tandara Hunting Safaris. Kulingana na meneja huyo, msitu huo una ukubwa wa zaidi ya hekta 112,000 na umbali kutoka Tunduru mjini hadi ofisi za msitu huo ni kilometa 90. Aidha kutoka ofisi za msitu hadi kwenye msitu ni kilometa tano.

“Msitu huu upo kando kando mwa mto Ruvuma, pia unafanya mpaka wa asili kwa upande wa kusini magharibi mwa msitu na kwamba kupitia mto Ruvuma kuna fukwe nzuri ambazo ni kivutio kwa wageni wanapotembelea msitu huu ’’, anasema.

Meneja huyo wa TFS anasema Hifadhi ya Mwambesi pia ina wanyama wa mtoni kama mamba na viboko hasa wakati wa masika wanakuwa wengi na kuvutia wageni wengi wanaobahatika kutembelea msitu huo.

Anasema mtalii akiwa katika msitu wa Mwambesi anaweza kufanya utalii wa kuteleza kwenye mitumbwi katika mto Ruvuma uliopo ndani ya hifadhi hiyo na aina hiyo ya utalii haipatikani katika misitu mingine nchini.

Deborah Mwakanosya ni Meneja wa Msitu wa Hifadhi ya Taifa wa Mazingira Asilia Mwambesi, anasema Mwambesi ni msitu wa asili wa pili kwa ukubwa kwa Tanzania ukiongozwa na msitu wa Kilombero mkoani Morogoro.

Anasema msitu huo ambao umezungukwa na mto Ruvuma, umesheheni baianowai mbalimbali za mimea adimu duniani ikiwemo miti aina ya Mipozipozi ambayo ina tabia ya kudondosha maji na inapatikana sehemu chache duniani ikiwemo katika msitu huo. Mwakanosya anasema mti huo una tabia ya kuimarisha ndoa na kwamba wengi ambao wameutumia umeleta mafanikio makubwa kwa kuimarisha mahusiano katika ndoa hivyo kudumisha ndoa za watu wengi.

Hata hivyo hakufafanua zaidi kuhusu kuimarisha ndoa kunakofanywa na mti huo. Miti mingine maarufu inayopatikana kwenye msitu huo anaitaja kuwa ni Muamalula unaopendwa na wanyama wengi wakiwemo Tembo, Ngedere na Nyani ambao wanakula matunda yake ambayo huwalewesha kama ambavyo mwanadamu anavyolewa akizidisha pombe.

“Wanyama wanapenda kula matunda hayo hivyo wanalewa na kupata mapumziko. Ndiyo maana tunasema ukifika Mwambesi unaweza kujifunza mengi na kufanya utafiti katika masuala mbalimbali ’’, anasisitiza Mwakanosya.

Aina nyingine maarufu ya miti katika hifadhi hiyo anaitaja kuwa ni Kigari Afrikana (Sausage tree). Hii ni miti inayotoa matunda ambayo wanakula wanyama hasa Tembo na kwamba miti hiyo inasaidia kurekebisha chembe nyekundu za damu katika mwili wa mwanadamu.

Anasema binadamu anaweza kutumia magamba ya miti ya Kigari Afrikana kama majani ya chai kwa ajili ya kuongeza damu hivyo anaweza kunywa kama sharubati (juisi). Mtaalam huyo wa miti anaitaja miti mingine adimu ambayo inapatikana wilayani Tunduru kuwa ni miti mawe ambayo ni jamii ya miti ya Mitetereka ambayo katika dunia nzima inapatikana katika nchi mbili; Tanzania katika maeneo ya Tunduru na Namtumbo mkoani Ruvuma na nchini Marekani.

“Miti hii inapatikana katika kijiji cha Mbati, wilayani Tunduru na kijiji cha Likuyu wilayani Namtumbo. Asili yake ukiuona juu kwenye matawi ni mti wa kawaida lakini chini kwenye shina ni jiwe zito, ni mfumo ambao Mungu ameutengeneza wa kipekee kwa miti aina ya Mitetereka’’, anasisitiza Mwakanosya.

Anasisitiza kuwa kuwepo kwa kivutio cha miti mawe kunaonesha kuwa kusini mwa Tanzania kuna utajiri wa vivutio vya utalii ambavyo havipatikani sehemu nyingine yeyote nchini hivyo vivutio hivyo vikiibuliwa na kutangazwa , vinaweza kuvutia watalii wengi .

Kwa mujibu wa Mtaalam huyo wa miti, mti mawe unaweza kuishi kwa zaidi ya miaka 120 na anaitaja changamoto kubwa inayoikabili miti hiyo kuwa ni kushambuliwa na watu wengi.

Anatoa rai kwa wananchi katika maeneo hayo kuacha kuharibu miti hiyo ili kuifanya iwe endelevu katika kizazi cha sasa na kijacho. Msitu wa Mwambesi una mabwawa makubwa ambayo yamekuwa makazi mazuri ya wanyamapori pembezoni mwake hali inayofanya kuwe na aina mbalimbali za wanyamapori katika msitu huo. Mwambesi ni moja kati ya misitu mikubwa ya Hifadhi za Mazingira Asilia tulionayo wenye utajiri mwingi wa flora na fauna za kutosha.

Msitu huu unahifadhiwa kisheria chini ya uangalizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Wilaya ya Tunduru kwa kushirikina na Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) Kanda ya Kusini.

BAADA ya kupiga kambi kwa siku tofauti 15 katika vituo ...

foto
Mwandishi: Albano Midelo

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi