loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanzania haikamatiki

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas amesema kutokana na Rais John Magufuli kuwa na mafanikio makubwa aliyofanya ndani ya miaka minne ya utawala wake, vyombo vingi vikubwa duniani vimeomba kuja kuandika mazuri ya Tanzania.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Serikali hadi Agosti, mwaka huu jijini hapa, Dk Abbasi alisema Tanzania inaendelea kung’ara kimataifa licha ya changamoto mbalimbali za baadhi ya Watanzania kushirikiana na mawakala wengine wa nje kutaka kuihujumu nchi.

“Kama mlivyosikia suala la kushikwa ndege zetu na kutumia baadhi ya majarida kujaribu kuichafua nchi, heshima na hadhi ya Tanzania kimataifa imeendelea kupanda kutokana na nia njema na kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Rais Magufuli,” alisema.

Alisema Julai, 2019, Tanzania ilipata fursa ya kipekee ya kumulikwa na Jarida la Forbes Afrika katika toleo lililokuwa na kichwa cha habari, “Tanzania-Building Prosperity,” likimtaja Rais Magufuli kuwa kiongozi mwenye maono makubwa na kutokana na mafanikio hayo vyombo vingi vikubwa duniani vimeomba kuja kuandika mazuri ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Dk Abbasi, ripoti iliyotolewa Julai 12, 2019 kwa pamoja kati ya Transparency International na Afro-Barometer, Tanzania imeongoza katika nchi 35 kwa kuonesha juhudi za wazi na zenye umakini katika kupambana na rushwa na imekuwa nchi ya kwanza katika kipengele cha Ofisi Kuu za nchi kwa maana ya Ofisi ya Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa hazihongeki.

Dk Abbasi alisema mafanikio haya yanatokana na msimamo thabiti wa Rais Magufuli na serikali yake lakini pia jinsi alivyoimarisha taasisi muhimu kama vile Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa(Takukuru), kuanzisha mahakama ya ufisadi na uhujumu uchumi na mfumo wa udhibiti wa rushwa katika manunuzi kupitia PPRA.

“Kwa mfano, Takukuru imeokoa Sh bilioni 86 zilizotokana na mishahara hewa na ukwepaji kodi.

Aidha, Sh bilioni 25.5 zimerejeshwa serikalini kati yake, Sh bilioni 14.6 zinatokana na urejeshwaji wa mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu na Sh bilioni 10.9 zilizotokana na thamani ya mali zilizotaifishwa yakiwemo magari, vituo vya mafuta, nyumba nane, magari nane na Sh bilioni 20 ni mali zilizozuiwa kesi zikiendelea,” alisema.

Alisema Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imeokoa takribani Sh bilioni 46.9 zilizokuwa zipotee kutokana na kutofuatwa taratibu za manunuzi, malipo ya zaidi ya mkataba kwa wakandarasi au baadhi kutorudisha fedha walizopewa kama dhamana, uzembe na rushwa.

Aidha, baada ya kufanya kwa ufanisi mkubwa mkutano wa SADC, Tanzania itaendelea kunufaika na kuwa mwenyeji wa mikutano mbalimbali ya Kimataifa ikiwemo Tamasha la Utamaduni Afrika Mashariki (JAMAFEST) litakapolifanyika kati ya Septemba 21 na 28, mwaka huu.

“Litahusisha watu takribani 100,000 kutoka nchi sita za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudani ya Kusini. Tamasha hili litafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,” alisema.

Alisema pia SADC itaendelea kuacha alama muhimu nchini ikiwemo mikutano mingine mingi itakayofanyika nchini ukiwemo wa sekta ya habari na mawasiliano utakaofanyika katikati ya Septemba, mwaka huu.

Dk Abbasi alisema pia, “taasisi zetu zitaendelea kunufaika mfano Bohari ya Dawa (MSD) imekamilisha mfumo wa kusambaza dawa nchi zote za SADC, kampuni ya simu Tanzania (TTCL) inaendelea kusambaza mkongo wa Mawasiliano (tayari Zambia, Malawi).”

Kuhusu mradi wa kufua umeme, Dk Abbas alisema safari ya miaka mitatu ya ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) umeshaanza na kuwa mradi huo wa megawati 2115 na wa nne Barani Afrika utagharimu Sh Trilioni 6.5 na tayari serikali imetoa Sh Trilioni 1.07 na kuwa hivi sasa hatua ya kwanza ya kuchepusha mto kwa kuchoronga handaki imekamilika.

Alisema umeme wa gesi na serikali inaendelea kukamilisha mradi wa upanuzi wa Kinyerezi-I ambao kwMradi huu wa megawati 185 utakamilika ndani ya miezi mitatu.

“Gharama za mradi huu unaogharamiwa na serikali ni Dola za Marekani 188 na serikali imeshalipa dola 128 hadi sasa,” alisema. Dk Abbasi alisema pia serikali imetangaza zabuni ya kuagiza vichwa 22 vya treni na vitano vya mafuta (Diesel Locomotive) na 17 vya umeme yaani (Electrical Locomotive) na mabehewa ya abiria 60 na 1,430 ya mizigo.

“Pia imetangaza zabuni ya kununua treni tano zilizokamilika za abiria zenye mabehewa nane kila moja na vichwa viwili kwa ajili ya uendeshaji wa treni za abiria kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro na kisha Dodoma,”alisema.

Kuhusu ujenzi wa madaraja, Dk Abbasi alisema serikali imeamua kujenga madaraja na tayari imetenga fedha za ndani Sh bilioni 71.4 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja jipya la mto Wami lenye urefu wa mita 513.5 litakalojumuisha ujenzi wa barabara za kilomita 4.3 kwa kila upande na kazi ishaanza.

Alisema serikali pia imesaini mkataba wa Sh bilioni 699.9 kwa ajili ya ujenzi wa daraja refu zaidi kwa ajili ya kuvuka Ziwa Afrika Mashariki na Kati la kilomita 3.2 kuunganisha mikoa ya Mwanza na Geita kwenye eneo la Ziwa Victoria; Kigongo-Busisi.

Pia serikali imeamua kujenga madaraja na kupitia TARURA, serikali imejenga madaraja madogo katika wilaya saba nchini likiwemo la Kondoa (Kisese, lenye urefu mita 38, linalogharimu Sh bilioni 2.08) na Kishapu (Manonga, lenye urefu mita 45 na litagharimu Sh bilioni 2.436).

“Mengine ni Bahi-Chipanga Bridge, urefu mita 45, litakalogharimu Sh bilioni 2.11; Iringa (M), Tagamenda Bridge, urefu mita 30, Sh bilioni 4.5; Songwe (W)- Kikamba Bridge, urefu mita 60, Sh bilioni 1.2; Iramba- Mtoa Bridge, urefu mita 60, gharama Sh bilioni 2.676 na Kilombero-Kihansi Bridge, urefu mita 40, gharama Sh milioni 972.

Alisema pia jijini Dar es Salaam inafanya ujenzi wa Daraja la Juu (Ubungo Interchange) kwa fedha zaidi ya Sh bilioni 200 kutoka Benki ya Dunia unaendelea na tayari umefikia asilimia 50. Mradi huu utakabidhiwa kwa serikali ifikapo 2020.

“Pia imeamua kupanua barabara ya njia sita kati ya Kimara na Kabaha. Hadi kufikia Julai, mwaka huu, ujenzi wa barabara ya njia sita pamoja na barabara za waenda kwa miguu ya Kimara-Kibaha kilometa 19.2 wenye thamani ya Sh bilioni 140.44 unaojumuisha madaraja ya Kibamba, Kiluvya na Mpiji umefikia asilimia 40.

Mradi huu unagharamiwa na serikali ya Tanzania kwa asilimia 100,” alisema. Katika sekta ya afya, serikali imeshatoa Sh bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa (RHH) na sehemu nyingi ujenzi umekamilika.

“Mikoa hiyo ni Mwanza, Simiyu, Njombe, Songwe, Katavi, Geita na Dar es salaam (Mwananyamala) na Sh bilioni tatu imetolewa kujenga hospitali ya kanda ya wazazi Mbeya na Sh bilioni 6.32 kwa ajili ya kujenga hospitali ya kanda Mtwara.

Alisema serikali imeamua kuwekeza katika maisha ya watu ngazi ya wilaya, Serikali mwaka huu ilitoa Sh bilioni 105 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za wilaya 67.

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi