loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Geita inavyojiandaa na mitambo ya kuongeza ubora wa dhahabu

TANGU mwaka huu uanze, Mkoa wa Geita umekua na ndoto kadhaa katika kuhakikisha madini ya dhahabu yanayozalishwa ndani ya mkoa huo yanaleta matokeo makubwa zaidi.

Ikumbukwe kwamba mkoa wa Geita ulianza kwa kukaribisha na kuweka mazingira mazuri kwa viwanda vidogo vya kuchenjua dhahabu baada ya hatua ya serikali ya kuzuiwa kwa kaboni zenye dhahabu kusafirishwa kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine. Hatua hiyo inaelezwa kwamba imesaidia sana katika kudhibiti utoroshaji wa madini.

Kisha Geita ikawa ya kwanza nchini kuanzisha soko la dhahabu huku Mkuu wa Mkoa huo, Robert Gabriel, akiendelea kuhaha kuhamasisha uanzishwaji wa masoko zaidi ya madini ambayo hadi sasa yamefikia sita katika mkoa huo.

Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba Geita ndio inazalisha kiwango kikubwa cha dhahabu kuliko mkoa wowote nchini, ikifuatiwa na mikoa ya Mara, Shinyanga, Mwanza na Mbeya.

Biashara lililofanyika mkoani humo mwaka jana, Gabriel aliweka wazi kwamba atahakikisha Geita inanufaika na madini ya dhahabu kwa asilimia 100. Februari 25 mwaka huu, Mwekezaji Mtanzania, Mama Sarah Masasi, alifika mkoani Geita akilenga kuwekeza katika madini ya dhahabu, kwa maana ya kuweka mtambo wa uongezaji ubora wa madini ya dhahabu (gold refinery plant).

Kwa sasa mitambo iliyoko Geita, yaani ile ya kuchoma kaboni zenye dhahabu (elusion plants) kutoka kwa wachimbaji wadogo, haitoi dhahabu iliyo tayari kwa mtumiaji wa mwisho.

Mwekezaji huyo ambaye sasa anatazamia kutoa dhahabu iliyo tayari kwa matumizi alipokelewa na wenyeji wake mkoani Geita wakiongozwa na mkuu wa mkoa huo akiwa na taasisi zote muhumu katika kufanikisha kwa haraka uwekezaji huo.

Baadhi ya taasisi hizo ni Shirila la Ugavi wa Umeme (Tanesco), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Geuwasa), Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) na zinginezo. Mama Masasi anakiri kwamba alifarijika kwa mapokezi aliyoyapata akisema anaamini uwepo wa timu hiyo nzito utasababisha uwekezaji anaotarajia kuufanya kuwa mwepesi na kukamilika vyema na kwa wakati.

Mama Masasi aliomba kupatiwa eneo la ukubwa wa ekari 4.5 likiwa mahali salama na kwamba ili uwezekaji anaotarajia kuufanya uwe na faida ilikuwa ni lazima pia apate wastani wa malighafi isiyopungua tani 50 hadi 80 kwa mwaka.

Mama Masasi aliendelea kusema kuwa, mitambo itakayotumika itawekwa na Kampuni ya Kimataifa ya Bactrac Company Technologies TERA, inyoaminika duniani katika sekta hiyo kwa kuwa na uwezo wa kuweka mitambo yenye uwezo wa kutenganisha madini ya dhahabu na madini ambatana.

Ni kwa msingi huo akasema angependa kuhakikishiwa uwepo wa mazingira mazuri kiuwekezaji baina ya pande zote, yaani Serikali, mwekezaji na wateja wa dhahabu, yaani soko.

Mama Masasi alisema: “Asante Mungu kwa kunifikisha hapa na kufahamiana nanyi, ninaahidi kuwa mtumishi wenu nikihakikisha Geita inafahamika kimataifa kwa uzalishaji dhahabu na mjue ninawahitaji kila siku ya maisha ya mradi huu.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa alimweleza mwekezaji huyo kuwa hakukosea kuja Geita, akamhakikishia upatikanaji wa eneo la ukubwa wa ekari tano bure tofauti na maombi yake ya ekari 4.5.

Mkuu wa mkoa pia alimhakikishia usalama na upatikanaji wa malighafi ya dhahabu, huku akimhakikishia pia uwepo wa miundombinu yote itakayotosheleza uanzishwaji wa kiwanda hicho.

Awali, Charles Itembe, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Azania ambayo inatazamia kutoa mkopo kwa mwekezaji huyo alisema benki yake ingependa kuhakikishiwa upatikanaji wa uhakika wa malighafi ili mteja wao huyo aweze kurejesha mkopo. Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Dk Japhet Simeo, aliwashauri watalaamu wa madini kumpa taarifa kamili na sahihi mwekezaji huyo ili kuepuka kumvunja moyo na kwamba taarifa atakazozipata kwao zitamwezesha kuamua ni aina gani ya uwekezaji anaweza kuufanya.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda, alimtoa hofu mwekezaji huyo kuhusu upatikanaji wa malighafi lakini akaomba muda ili kuja na takwimu sahihi zitakazomhakikishia na kumpa ujasiri mwekezaji huyo kundelea na mradi.

Agosti 29, 2019, Mama Sarah aliwasili tena Geita na kupelekwa kwenye eneo ambalo mkoa umempa kwa ajili ya kuanzisha kiwanda hicho cha uongezaji ubora wa madini ya dhahabu na kama ilivyo sera ya mkoa wa Geita ya kutokuwa na urasimu kwa wawekezaji, Mama Sarah amepewa kiwanja chenye ukubwa wa ekari nane bure. Kiwanja hicho kiko katika Mtaa wa Bombambili, Kata ya Bombambili na tayari amekabidhiwa hati na ofisi ya Mkurugenzi wa Mji wa Geita.

Katika kufanikishwa uwekezaji huo, ofisi ya Mkurugenzi wa Mji wa Geita tayari imechonga barabara yenye urefu wa kilometa 3.5 kutoka katikati ya mji hadi mahala kitakapojengwa kiwanja hicho. Tanesco na Geuwasa wako kwenye taratibu za kufikisha miundombinu ya umeme na maji. Baada ya kuoneshwa eneo hili lililopo maeneo ya viwanda, Mama Sarah alieleza kuridhishwa kwa kiasi kikubwa ambapo amesema ujenzi unatarajia kuanza hivi karibuni .

Mwekezaji huyo amemshukuru mkuu wa mkoa, Robert Gabriel, mkurugenzi wa halmashauri ya mji, Modest Apolinary na maofisa kutoka ofisi za madini, Geuwasa, Tanesco na Tarura kwa kuhakikisha uwekezaji anaotarajia kuufanya haukwami.

Mwekezaji huyo ambaye ameahidi kushiriki katika maonesho ya pili ya madini yatakayofanyika mjini Geita kuanzia Septemba 20-29 ametembelea soko la madini na kushuhudia uuzwaji wa dhahabu ya kilo 1.171 yenye ubora wa asilimia 93 yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 124 ambapo bei ya gramu moja kwenye soko la dunia kwa dhahabu hiyo mwezi Agosti ilikuwa Sh 113,260.

Gabriel anasema bado mkoa wa Geita unawakaribisha wawekezaji kwa ajili ya kujenga hoteli za kitalii, kumbi za kisasa za mikutano pamoja na viwanda akisema Geita haina urasimu kwa mwekezaji.

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: Boaz Mazigo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi