loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanzania yangu ni Afrika yetu

Miongoni mwa nchi za Afrika zinazotajwa sana ulimwenguni kwa uzuri, ni Tanzania.

Wengine hata wanaiita Mama Afrika. Hii ni kutokana na mchango wake mkubwa katika ukombozi wa nchi nyingi za Bara la Afrika ilipojitoa chini ya utawala wa Mwalimu Julius K. Nyerere.

Kutokana na mchango wake mkubwa katika nchi nyingi za Afrika kwa maendeleo ya kisiasa na hasahasa kusaidia kulinda amani, nchi hii ya Afrika Mashariki inasifika na kufahamika zaidi katika nchi nyingi kuwa ni Kisiwa cha Amani hata kupewa vipaumbele katika jumuiya kubwa za kimataifa.

Si siri, karibu kila linapotajwa Bara la Afrika, nyuma yake kuna Tanzania; kwa nini Tanzania? Watu mbalimbali wanasema ni kwa sababu ndiyo nchi inayotajwa kudumu katika amani ambayo ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ama yawe ya kijamii, kiutamaduni, kiuchumi, kiasiasa au kiulinzi.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Tanzania ni nchi yenye vivutio vingi vya utalii na rasilimali nyingi zisizopatikana katika nchi nyingine duniani.

Mara nyingi na kwa uwazi kabisa, Rais John Magufuli amekuwa akisisitiza ukweli huu huku akiwahimiza Watanzania kufanya kazi kwa juhudi na maarifa sambamba na kulinda rasilimali walizo nazo kupitia matumizi sahihi na yenye tija.

Chimbuko la lugha ya Kiswahili ambayo Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliipitisha kuwa lugha rasmi ya nne, ni Tanzania na hiyo, ndiyo lugha inayokua kwa kasi zaidi barani Afrika huku mataifa ya nje yakiitambua kama lugha ya Afrika.

Tanzania yangu, Afrika yetu ni nchi pekee inayozingirwa na maji pande zote. Kaskazini kuna Ziwa Victoria; ziwa la pili kwa ukubwa duniani na Mashariki, kuna Bahari ya Hindi.

Kwa upande wa Kusini, kuna Ziwa Nyasa na Magharibi kuna Ziwa Tanganyika ambalo ni ziwa la pili lenye kina kirefu duniani. Ndani ya maziwa haya, kuna samaki watamu tofautitofauti wasiopatikana mahali pengine. Miongoni mwa samaki maarufu wanaopatikana katika Ziwa Victoria kwa mujibu wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, ni sato na sangara wanaopendwa kuliwa sana Tanzania hasa katika mikoa ya Mwanza, Mara na Kagera lilipo ziwa hilo.

Samaki hawa na wengine wengi, wamekuwa kivutio na bidhaa adimu kwa mataifa mbalimbali yakiwamo ya Ulaya, Amerika na Asia kutokana na ubora wake. Hili nalo ni moja ya mambo yanayonifanya niseme:

“Tanzania yangu, Afrika Yetu.” Wapo pia samaki wengi katika maziwa, mito na sehemu kubwa za maji nchini Tanzania. Tukiamua kusema tuvue tu na tusifanye kazi nyingine yoyote, tutavua samaki wengi wa kutosha kwa siku moja kuufukuza umaskini wote nchini Tanzania.

Madini mbalimbali yaliyopo Tanzania, ni nembo tosha ya utajiri wa Afrika. Madini aina ya ‘tanzanite’ yanayotokea Mererani Arusha ni nembo ya uwakilishi wa Tanzania katika soko la kimataifa, kutokana na asili ya jina.

Katika jiji la Arusha mbali na Mererani inasemekana kuna madini mengi zaidi ya Tanzanite ambayo mengine tukichimba miaka 100 bado yataendelea kuwepo tu. Mbali na hayo katika mikoa kama Geita, Mwadui (Shinyanga), Sekenke (Singida) yapo madini ya dhahabu.

Rais Magufuli amewahi kuzitaja aina nyingi za madini yapatikanayo katika mikoa na maeneo mbalimbali nchini yakiwamo ya almasi, shaba, rubi, lulu, makaa ya mawe n.k. yote yanapatikana Tanzania. Tanzania imebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutuba inayostawisha mimea mingi.

Kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara kinafanyika nchini Tanzania karibu mwaka mzima kwa mazao ya chakula kama mahindi, mpunga, uwele, maharagwe, ngano, ulezi na kadhalika na kuhusu mazao ya biashara, miongoni mwa mengi, yapo ya chai, katani, kahawa na mpira.

Kimsingi, mtu anaweza kuuthibitishia ulimwengu na hata Bara la Afrika mantiki ya kusema kwa ujasiri kuwa, Tanzania yangu ni Afrika yetu.

Hii ni kwa kuwa pamoja na mambo mengine, tukiamua tusitegemee kilimo cha mvua, tukatengeneza mifumo ya umwagiliaji kutokana na maji tuliyo nayo katika mito, mabwawa, maziwa, bahari na vyanzo vingine vya maji, tutaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kwa kilimo duniani. Kupitia hili tutaweza kuilisha Afrika yote na chakula kingine tukawauzia Wazungu.

Maandiko Matakatifu yanaitaja Israeli kama nchi iliyobarikiwa na tunauona uhalisia wake kuwa ni pamoja na kuzungukwa na mawe pande zote, lakini inastawisha mazao mengi kwa kutumia vizuri maji waliyo nayo japo eneo lake la kilimo ni dogo. Tanzania tuna kivutio cha mlima mrefu kuliko yote barani Afrika.

Mlima huu siyo mwingine, bali Mlima Kilimanjaro uliopo Moshi mkoani Kilimajaro. Watalii kutoka sehemu tofauti duniani, wanakuja Tanzania ili kuuona Mlima Kilimanjaro na kuipa heshima kubwa Afrika. Ndiyo maana ninasema:

“Tanzania yangu ni Afrika yetu.” Hifadhi za wanyama pori ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii nchini Tanzania na Afrika kwa jumla. Mbuga kubwa ya wanyama duniani kote iko Tanzania.

Hiyo ni Serengeti. Mbuga pekee iliyobeba wanyama wa kila namna, wakiwemo jamii ya paka kama duma, chui na simba wakiwamo wanaopanda miti sambamba na wale walao nyasi kama nyati, swala, nyumbu, tembo, pofu, pundamilia, faru na wengineo wengi.

Ziko hifadhi nyingi za wanyamapori nyingi ambazo miongoni mwao ni Ngorongoro, Mikumi, Tarangire, Katavi na nyinginezo nyingi. Yote haya ni baadhi tu kati ya vivutio vingi vilivyopo Tanzania. Hatuna budi kujivunia baraka hizi tulizopewa na Mungu zinazolinufaisha pia Bara la Afrika na kwingineko duniani ndiyo maana ninasema tena kuwa: “Tanzania yangu, Afrika yetu.”

Mwandishi ni msomaji na mchangiaji katika gazeti hili. 0675335367

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: David Mangara

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi