loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Akili za kuambiwa changanya na zako

“AKILI za kuambiwa, changanya na za kwako.” Huu ni msemo ambao umepata umaarufu baada ya kutumiwa na Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete katika mikutano yake mbalimbali.

Pamoja na mambo mengine, msemo huu unamaanisha kwamba, maneno au ushauri unaopewa na watu, pamoja na kutathimini ni vyema ukautafakari, na kuuchuja kabla ya kuufanyia kazi.

Kwamba, ni muhimu sana kupima kwa makini kila jambo au ushauri wowote, usikiao au kupewa na watu mbalimbali. Ni vyema hata kujiuliza na kutafakari juu ya mtoa ushauri au msemaji husika na nia yake.

Maana inaweza kutokea mtu akashauri jambo fulani lifanyike kwa namna fulani kumbe akiwa na maslahi yake binafsi kuliko yale ya walengwa. Wanahistoria wanasema kwamba kabla ya ujio wa wakoloni, Afrika ilikuwa ikiendelea kivyake vyake, ikiunda mashine zake baada ya kugundua chuma, ikiunda nguo zake na masuala mengine muhimu.

Lakini wakoloni walipokuvamia mama Afrika wakitafuta mali ghafi, masoko na wazalishaji wasiohitaji ujira mkubwa, wakaanza kukuletea mama Afrika vitu walivyozalisha kwao na hapo ndipo watoto wako wakajikuta wanazembea kufikiri kuzalisha vya kwao na kuanza kusubiri kila kitu waletewe au wazalishiwe na wakoloni.

Baada ya Mama Afrika kupata uhuru, mbali na watoto wako kuendelea kusubiri kinachotengenezwa na wakoloni (mabeberu), Afrika umeendelea na mazoea ya kutegemea pia ushauri wa watu hao wa nje katika kutatua changamoto zako na hapo ndipo kuna tatizo.

Kwa vile kile kilichowafanya waje kukutawala, hususani raslimali zako bado wanakihitaji, ushauri au misaada ya aina mbalimbali ambayo wamekuwa wakikupa, kiuhalisia siyo msaada bali ni bomba la kuendelea kukunyonya.

Ushauri na misaada yao yenye masharti baadhi ikionekana kama ya maana sana, imekuwa ikikusababishia matokeo hasi tofauti na yaliyotarajiwa.

Utasikia wanakushauri; “Usifanye hili, fanye lile” lakini ukweli ni kwamba wakati mwingine ushauri wao unalenga zaidi maslahi yao binafsi na siyo ya watoto wako.

Kilicho wazi ni kwamba mabeberu hawa hawapendi kabisa kuona Afrika unajitegemea kwa sababu wao watakosa mahala pa kuendelea kunyonya na ndio maana wanafikia hata kuzuia usisimamishe miradi yenye manufaa kwa visingizio hivi na vile.

Ndio maana watahimiza usitekeleze mradi kama ule wa Nyerere wa kufua umeme kwenye maporomoko ya Bonde la Mto Rufiji wakidai eti unaharibu mazingira kumbe hawataki upate umeme wa kutosha kuendesha viwanda vyako kwani ni sababu ya wewe ‘kujikomboa’ kutotegemea viwanda vyao.

Watakushauri usijenge treni ya umeme wakidai ni gharama kubwa na eti haina manufaa makubwa kiuchumi kama ambavyo miaka 1970 walipofanyia hiana kujenga reli ya Tazara hadi viongozi shupavu wa wakati huo wakaenda China na kusaidiwa.

Watakwambia hauna ujuzi au utaalamu wa jambo hili au lie; ili kwa kutumia wataalamu wao wakunyonye Mama Afrika na kukuibia kadri wawezavyo. Watakwambia hauna teknolojia hii au ile ili wakuletee teknolojia au mitambo inayokulazimu uendelee kuwategemea katika uendeshaji wako wa mambo, huku wakinyonya raslimali zako.

Watakuomba uwapatie miaka kadhaa ili wafanye utafiti wa hili au lile katika ardhi yako yenye mali kibao kama vile madini, mafuta, na gesi. Watatumia muda mwingi kuchota mali yako bure – kwa ‘kibandiko’ cha utafiti na majaribio ya mradi husika.

Wakimaliza hatua hiyo watakuambia uwape muda waanze mradi au wakati mwingine wadai hawaoni kitu kumbe wameshachukua kila kitu! Afrika, watakwambia sera yako ya uchumi sio nzuri halafu wanakupa waliyoitunga wao ambayo wanataka itumiwe na kila nchi ya Afrika bila kujali kwamba mazingira ya nchi na nchi yanatofautiana sana.

Bila shaka bado unakumbuka ile sera yao ya Structural Adjustment Program (SAP) ambayo walikutaka uitekeleze ndipo wakupe misaada na mikopo uchwara wakisema italeta neema kwa watu wako. Kweli ilileta neema au nakama?

Hawa jamaa watakwambia eneo lako si salama, unahitaji ulinzi kumbe wanataka waweke kambi zao kwako waendelee kukutawala hata kijeshi au siku moja ukionekana unatishia maslahi yao basi wanasababisha nchi isitawalike.

Watakwambia ndugu yako, mwafrika mwenzako anakuchukia na anataka kukuua ili mpigane na nduguyo, wapate fursa ya kuuza au kufanyia majaribio silaha zao na kuiba raslimali zako. Hawahitaji kuona una amani na hasa wanapotaka kukunyonya.

Yaani, migogoro ya watoto wako wenyewe kwa wenyewe kwao kama kunguru wanaona sawa na vita vya panzi. Hawa jamaa hawataki kuona unakuwa na kitalu cha shibe.

Yaani, njaa wanatamani itamalaki kwa watu wako ili wajifanye wanakupa misaada ili kupitia humo waendelee kukutawala na kukunyonya. Hawataki kuona una umoja yaani wanafurahia utengano na migawanyiko miongoni mwa watu wako.

Afrika moja, inawaogopesha hivyo hawataki kuiona inasimama imara. Utasikia wanakwambia, eti unazaa watoto wengi mno, usioweza kuwatunza.

Pamoja na mambo mengine, wanataka upungukiwe nguvu kazi na masoko kwa maendeleo yako. Wanakuona, eti wewe ni msahaulifu mno kiasi kwamba haukumbuki jinsi ‘walivyojidai’ kupunguza idadi ya watu wao, na madhara yaliyowapata hadi sasa wanabadilisha sera zao za uzazi wa mpango!

Sio kwamba nakufundisha au kusema kitu kipya ambacho hukijui, bali nakukumbusha tu mama yangu Afrika; akili za kuambiwa, changanya na zako. Walau sasa Afrika una viongozi ambao wanaona na kutafakari vyema kwa maslahi ya nchi na watuwako.

Hatua ya Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli kutekeleza miradi mbalimbali mikubwa yenye maslahi kwa Taifa lake kinyume na matarajio ya hao ‘wajomba’ hakika ni ya kupongeza sana. Miradi hiyo ni kama ule wa kufua umeme kwenye Bonde la Mto Rufuji, ujenzi wa treni ya kisasa inayotumia umeme, ujenzi wa miradi ya maji, vituo vya afya na ujenzi wa barabara mbalimbali zinazoendelea nchini kote kwa kutaja tu kwa uchache.

Lakini mambo ambayo yamenivutia kuandika makala haya ni maneno aliyoyasema katika Jukwaa la Uongozi wa Bara la Afrika hivi karibuni pale Ikulu Jiji Dar es Salaam mmoja wa watoto wako ambao wameibukia kuwa viongozi shupavu, Dk John Magufuli.

Alisema: “Waafrika hawakutafsiri vizuri dhana ya uhuru na kujitegemea. Lengo la kupigania uhuru lilikuwa ni kurejesha raslimali zilizokuwa kwenye mikono ya wakoloni ili ziweze kusimamiwa na Waafrika wenyewe, kuwa na maamuzi nazo pamoja na kuzitumia kwa ajili ya kujiletea ukombozi wa kiuchumi.” Anaendelea kugongelea msumari wa moto kwa kusema:

“Tuna mawazo ya utegemezi kwa watawala wa kikoloni huku tukijua wazi kuwa hawawezi kuwa wakombozi wetu kiuchumi”.

Kimsingi, kauli kama hizi zikiambatana na matendo vitakukomboa upya kiuchumi mama Afrika hadi kufikia kiwango cha kujitegemea kabisa.

Ndiyo, Afrika kujitegemea yenyewe bila kutegemea ‘wajomba’ kutoka magharibi au mashariki ni jambo linalowezekana kabisa. Ni suala tu la kuamua na kutenda kwa dhati na uzalendo wa hali ya juu.

Amka Afrika, uanze kukimbia, kama bado umelala. Sema, hapana imetosha! Afrika una kila kitu cha kukuendeleza mwenyewe; watu na raslimali tele. Sasa unakwama wapi Afrika? Ninakuombea uongozi mwema, bora na madhubuti kusimamia utajiri wako kwa maendeleo ya watu wako.

Mungu akuepushe na vibaraka wa watesi wako ili watoto wako wote wafaidi maziwa na asali yao, ambayo Mungu amewabariki katika ardhi yao ya ahadi, Mama Afrika. Hivyo, siku zote akili za kuambiwa changanya na za kwako.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili.

Anapatikana katika gorwewm@gmail. com au +255 762 380 283.

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: Gorwe Machage

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi