loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Rushwa ya ngono vyuoni inaangamiza wengi

NOVEMBA 27, mwaka jana Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Vicensia Shule aliripotiwa kuandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, alitaka kutumia bango kufikisha ujumbe wake kwa Rais John Magufuli aliyekuwa amezuru chuoni hapo kufungua maktaba mpya iliyojengwa katika Kampasi ya Mlimani, jijini Dar es Salaam, lakini akawaogopa walinzi.

Akaandika: "Baba @Magufuli JP, umeingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufungua maktaba ya kisasa. Rushwa ya ngono imekithiri mno UDSM. Nilitamani nikupokee kwa bango langu ila ulinzi wako umenifanya ninyamaze…."

Agosti 14, mwaka huu (2019) mhadhiri wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Samson Mahimbo, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na shitaka la kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wa chuo hicho ili amuwezeshe kufaulu masomo yake.

Hizi ni dalili kuwa, katika taasisi za elimu ya juu, vipo vitendo vya kudai na kutoa rushwa hususani baina ya walimu wa kiume na wanafunzi wa kike.

Kimsingi, rushwa ya ngono ni moja ya matendo ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia yanayowaathiri zaidi wanawake kazini na hata walio masomoni katika taasisi za elimu ya juu kama vyuo japo hayasemwi hadharani.

Kwa mujibu wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), takriban asilimia 89 ya wanawake katika sekta ya umma, wamepata bugudha za kingono wakati wakitafuta kazi, cheo au huduma.

Gazeti hili limefanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa elimu kupata maoni yao mintarafu tatizo hili na namna ya kulimaliza.

Katika mazungumzo kwa nyakati tofauti, wadau mbalimbali wanasema ni vigumu kuthibitisha kuwa, kuna rushwa ya ngono vyuoni kwa kuwa hilo ni suala la kimaadili linalofanywa kwa siri.

Mhadhiri wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW), Nyangalesi Nyangele (siyo jina halisi) anasema kumekuwapo minong’ono inayosikika miongoni mwa wanafunzi na jumuiya ya wahadhiri katika taasisi mbalimbali kuhusu uhusiano wa ‘karibu sana’ kati ya mwanafunzi wa kike na mwalimu wa kiume, lakini hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kuwa rushwa hiyo ipo.

 “Kwa kuwa suala hili ni la kimaadili, lina usiri mkubwa hivyo, ni vigumu mtu kuthibitisha kama kweli lipo ingawa linaweza kuwapo endapo mamlaka husika ina upungufu wa kimbinu katika kushirikisha jumuiya za wanafunzi na walimu,” anasema Nyangele.

Anaongeza: “Mara nyingi mjadala wa rushwa za ngono unaibuliwa ama na wanaharakati ndani ya chuo, au wahadhiri wa jinsi ya kike ambao kwa namna moja au nyingine, hudai kupata taarifa kutoka kwa wanafunzi, wanaoweza kumtuhumu mwenzao wa kike ambaye kwa mtazamo wao, wanamwona dhaifu kitaaluma, lakini anakuwa na alama za juu zaidi yao kutoka kwa mwalimu anayeonekana kuwa na mahusiano naye kimapenzi...”

“Inasemekana pia kuwa, wanafunzi wa kike wanaweza kumtumia mwenzao wanayeamini ni mrembo ili amshawishi kimahaba mwalimu wa kiume anayeonekana ni mgumu na makini sana katika kutoa alama za somo lake linaloonekana gumu sana kwao.”

Nyangele anasisitiza kuwa, vyovyote iwavyo lazima uadilifu upewe nafasi sambamba na kuzingatia misingi ya kazi na hatua kali kuchukuliwa dhidi ya wanafunzi au walimu wanaothibitika kufanya hivyo.

Kwa upande wake, Dk Alfred Nchimbi aliyepata kufundisha katika Chuo cha Utumishi wa Umma, Dar es Salaam na sasa ni Mkutubi Msaidizi Mkuu katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, anasema ni vigumu kuthibitisha kuwa rushwa ya ngono ipo vyuoni kwa kuwa watu hawaisemi wazi labda kwa kuhofia hatima yao.

“Rushwa hii ni tofauti na ile ya pesa ambayo mtoaji anaweza kuwambia watu kuwa imebidi nitoe pesa nipate huduma hii, lakini siyo rahisi mwanamke kusema nimefanya ngono ili nipate kitu fulani ndiyo maana rushwa hii haisikiki kama ilivyo rushwa ya pesa na ni vigumu kuithibitisha,” anasema.

Mdau huyo wa elimu anasema madhara ya rushwa ya ngono yanaweza kuwa kisaikolojia na hivyo, kumfanya mwanafunzi husika kupata msongo wa mawazo na kulazimika kuhama chuo, au kujikuta akifanya vibaya katika masomo.

Ili kumaliza rushwa ya ngono vyuoni, Dk Nchimbi anashauri elimu ya maadili ifundishwe kuanzia katika familia, shule za msingi, sekondari, vyuoni na kazini.

“Watu wajue madhara ya utovu wa maadili kama rushwa ya ngono na wakubali kuwa tatizo lipo, hivyo lisemwe bila aibu wala woga na hatua madhubuti zichukuliwe,” anasema.

Mwandishi alipotaka kujua kama uongozi wa ISW umewahi kupata malalamiko kuhusu rushwa ya ngono ama kutoka kwa wanafunzi au kutoka kwa walimu, Mshauri wa Wanafunzi, Andrew Randa alisema atafutwe Mkuu wa Taasisi, Dk Joyce Nyoni.

Alipofika ofisini kwa Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Ijumaa iliyopita, aliambiwa hayupo na alipofika kwa Naibu Mkuu wa Taasisi (Fedha na Utawala), Dk Zena Mabeyo alisema hawezi kutoa tamko la taasisi, bila maelekezo ya mkuu wake.

Mtaalamu wa vyombo vya habari na mawasiliano kwa umma, Dk Joyce Bazira, anasema vyombo vya habari lazima vizingatie na kutoa taarifa zisizoongeza madhara kwa waathirika, bali zinazowasaidia na kuleta tija kwa umma ikiwa ni pamoja na kuhamasisha umma kuzungumzia na kuripoti dalili au vitendo vya rushwa ya ngono.

CHANZO CHA RUSHWA YA NGONO

Profesa wa uchumi (hataki kutajwa) anasema rushwa ya ngono vyuoni hutokea walimu (wahadhiri) wanapotaka kutumia nafasi zao kujinufaisha kwa ngono, huku wanafunzi wa kike nao wakitaka kunufaika kwa kupewa alama za bure katika mitihani.

Anasema viashiria vya walimu kutaka rushwa ya ngono kwa wanafunzi, ni pamoja na vitisho vya kitaaluma visivyo na msingi kwa wanafunzi.

Profesa huyo anasema: “Siyo wote, lakini wenye tabia hiyo silaha yao kubwa ni kuwatishia wanafunzi kuwa ‘atawakamata; kwamba watafeli wote; hizo siyo dalili nzuri.”

Kuhusu wasichana wanaotaka kutoa rushwa hiyo kwa walimu, anasema: “Mara nyingi mwanafunzi kama huyo darasani haulizi kitu hata kama hajaelewa, na anapotaka msaada wa mwalimu, hupenda kumfuata akiwa peke yake  na kwa muda usio wa kazi na wengine, hupenda kumpa mwalimu ofa hata za chakula na vinywaji.”

Anaongeza: “Hivyo ni viasharia vibaya kwani katika mazingira yote hayo, wengine huja wakiwa na mavazi ya ‘kutisha; karibu nusu uchi na mwenendo wao huonesha kuwa, huyu hahitaji msaada wa kimasomo, bali ana agenda yake ndiyo maana anakuja peke yake muda huu.”

“Ndiyo maana taasisi makini zimeweka utaratibu wa mavazi na kama mwanafunzi atavaa kinyume na mwongozo, hata getini hapiti maana walinzi watamzuia …”

Mwongozo wa Serikali kuhusu Mavazi katika Taasisi za Umma Na. 3 wa Mwaka 2007, unapiga marufuku walimu na wanafunzi kuvaa mavazi yanayobana na kuonesha maungo.

Mwongozo wa ISW wa Mwaka 2017/ 2018 na 2018/2019 katika kurasa za 123 na 146 unatoa maelezo na picha za mavazi yasiyoruhusiwa kwa walimu na wanafunzi zikiwamo suruali za mlegezo na kupiga marufuku nguo zinazoacha mabega, kifua na mapaja wazi kama gauni na sketi fupi na zenye mipasuo.

 

 

Mhitimu wa Shahada ya Pili ya Ustawi wa Jamii kutoka ISW, Safari Kitamogwa anasema: “Ubaya wa rushwa ya ngono katika chuo au taasisi yoyote ya elimu, ni kuwapo uwezekano wa wahitimu wa namna hiyo kurudi kufundisha vyuoni au shuleni maana vyeti vyao vitaonesha wamefaulu vizuri kumbe ni ufaulu wa kupewa, hivyo, vyuo vinakuwa na walimu mbumbumbu na kuzalisha wahitimu mbumbumbu…”

Mwalimu Pendo Matiko (siyo jina halisi) wa ISW, anasema: “Rushwa ya ngono ni hatari kwani nchi yoyote inapokuwa na vyuo ambavyo wahitimu wanapata vyeti kupitia rushwa ya ngono, inaweza kuwa na watu wenye vyeti vyenye ufaulu mzuri, lakini kiutendaji vichwani ni ‘weupe’ hivyo, kuifanya nchi irudi nyuma kimaendeleo na kiuchumi kwa kuwa hakutakuwa na uzalishaji wenye tija mahali pa kazi.”

Mwanafunzi wa kike katika taasisi hiyo aliyekataa kutajwa anasema: “Walimu wakuu, wakuu wa shule au maofisa elimu wasibanwe kuwa shule zao hazijafaulisha; kufanya hivyo kunawafanya wengine watumie njia chafu ili shule au wilaya zao zinaonekana zimefaulisha wanafunzi wengi na zinafanya vizuri.”

“Wanafunzi kama hao ndio wanapofika vyuoni, wanalazimika kujitoa hata kwa rushwa ya ngono ili wafaulu na kupata vyeti maana wao wanachokitaka ni cheti, kazi na cheo na siyo ubora,” anasema.

Kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation na Imamu Mkuu wa Masjid Mnyamani, Dar es Salaam, Mohammed Iddi Mohammed na Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (Prolife) Tanzania, Emil Hagamu wanasema nguvu za kiimani kupitia dini zinapaswa kutumika ili watu wamwogope Mungu kwa kuwatendea mema wenzao na kuepuka zinaa ikiwamo rushwa ya ngono.

“Jamii ijengwe katika kufichua uovu wa rushwa unaochangia ongezeko la utoaji mimba katika vyuo…” anasema Hagamu.

Naye Sheikh Mohamed anasema: “Rushwa ni dhambi na ngono yaani uzinzi ni dhambi, hivyo, rushwa ya ngono ni dhambi ndani ya dhambi inayopaswa kuondolewa kwa watu kuhimizwa kumtii Mungu.”

Anaongeza: “Hata wanaoajiriwa, inabidi uchunguzi makini ufanyike kuhusu historia ya uadilifu ya mtu anayetaka kuajiriwa.”

Katika mazungumzo na gazeti hili, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Avemaria Semakafu anasema: “Rushwa ya ngono ina madhara maradufu kwa kuwa inadhalilisha utu, na kuwanyima haki ya masomo kwa kufelisha wanafunzi wenye uwezo na kuwapa waliokubali kujidhalilisha kwa kutoa rushwa hii ili wapewe maksi (alama).”

“Hali hii inazalisha tatizo la taifa kuwa na ‘makanjanja’ na ‘vishoka’ wa elimu wanaolifanya taifa  kuwa hatarini kupata wasomi, viongozi, watendaji, wazalishaji na wafundishaji wenye uwezo duni hivyo, kutishia taifa kukosa nguvu za kitaalamu na kiuchumi,” anasema.

Anasisitiza kuwa, wanaotuhumiwa kufanya unyanyasaji huo, lazima wachunguzwe na hatua stahiki kuchukuliwa dhidi ya wanaobanika kufanya hivyo.

 

 

 

 

 

Hivi karibuni Tamw kiliendesha mafunzo kwa wanahabari kutoka mikoa ya Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam kujadili namna ya kuvunja ukimya huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben anasema: “Rushwa ya ngono ipo, lakini haizungumzwi maana inachukuliwa kama jambo la kawaida na lisilozungumzwa hadharani… Kwa kweli jambo hili ni gumu na linahitaji watu ‘wagumu’ na wanaojiamini kulimaliza.”

Mratibu wa Mradi wa Boresha Habari Zuia Ukatili unaofadhiliwa na Internews, Florence Majani anahimiza vyombo vya habari vishirikiane na jamii kukomesha rushwa ya ngono ili kuongeza ufanisi kazini na katika taasisi za elimu.

Anasema: “Inauma kama mwanao anahitimu chuo, anakuja na cheti chenye ufaulu mzuri, lakini kila anapoenda kuomba kazi, anaonekana hajui; anaachwa eti kwa sababu alipata maksi baada ya kutoa rushwa ya ngono…”

Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, Beatrice Mpembo anataja vikwazo katika vita dhidi ya rushwa ya ngono kuwa ni pamoja na waathirika kutokutoa taarifa kwa wakati, huku wengine wakificha ushahidi, uelewa mdogo wa jamii na tafsiri ya sheria kuhusu rushwa ya ngono.

Anasema ingawa zipo sheria zinazohusu masuala ya udhalilishaji kijinsia ikiwamo Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa Marejeo Mwaka 2002 katika Sura ya 15 inayohusu makosa dhidi ya utu, na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 / 2007 katika Kifungu Na. 25 kinachohusu rushwa ya ngono, ni watuhumiwa wachache wanaofikishwa mahakamani na kutiwa hatiani kutokana na kukosekana kwa ushahidi hali inayofanya kesi zao kufutwa au kutofikishwa mahakamani kabisa.

Anasema jamii isifumbie macho kosa hilo na iwe tayari kutoa taarifa na ushahidi ili kuwatia hatiani wahusika.

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi