loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hii ndiyo dawa ya wavamizi wa ardhi

HIVI karibuni, vyombo vya habari vimeripoti kuhusu hatua iliyochukuliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi dhidi ya watu waliovamia eneo moja mkoani Arusha.

Watu hao wapatao 100 walivamia eneo lenye ukubwa wa ekari nane katika Kata ya Sinoni jiji la Arusha ambalo ni mali ya bibi Nasi Murua mwenye umri wa miaka 98. Waziri Lukuvi ametoa miezi mitatu watu hao wamlipe bibi huyo Sh milioni 500 kama fidia ya eneo.

Alitoa uamuzi baada ya kuzungumza na wavamizi hao. Hata hivyo, serikali imetumia busara za kutoona haja ya kuwavunjia nyumba wavamizi hao badala yake ikawataka wamfidie. Hatua hii aliyoichukua inapaswa kupongezwa na kila mpenda haki.

Ni hatua ninayotamani iwe endelevu dhidi ya watu wote waliodhulumu maeneo ya wanyonge. Natamani kuona uamuzi huu ukifanyika kwa watu wengine wanaopigania haki yao dhidi ya waliovamia maeneo yao bila mafanikio!

Hata hivyo, uamuzi wa Waziri Lukuvi ni ujumbe tosha kwamba haki ya mtu haipotei.

Hata ipite miaka lukuki, haki iliyopindishwa inaweza kurejea kwa mwenye nayo. Mfano mzuri ni wa huyu bibi ambaye imeelezwa kuwa mgogoro wa ardhi kati yake na wavamizi ulidumu kwa miaka 43.

Tunaelezwa bibi huyo alikwenda mahakamani, lakini hakupata haki yake.

Inawezekana wavamizi walimbeza na kutamba kuwa ndiyo washindi. Ishukuriwe serikali ya awamu ya tano kupitia Waziri Lukuvi imeingilia kati na kutoa haki stahiki kwa bibi huyu. Kama nilivyosema awali, hatua hii aliyochukua Waziri Lukuvi ni ujumbe kwa watu wote waliovamia maeneo ya watu wengine.

Lakini pia ujumbe huu ufikie mamlaka zote za serikali zenye tabia ya kupindisha haki za wananchi kwa makusudi kutokana na ushawishi wa aina mbalimbali ikiwamo fedha.

Serikali za mitaa, mabaraza ya kata ni miongoni mwa mamlaka zinazonyooshewa vidole kutokana na kudhulumu haki za watu wanyonge kwa kutotoa uamuzi stahiki.

Mwaka jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipoita wananchi wenye malalamiko juu ya migogoro ya ardhi kwa lengo la kuwapa msaada wa kisheria, mabaraza ya ardhi yalibainika kuwa chanzo cha tatizo.

Makonda aliweka bayana kwamba mabaraza mengi ya kata yamekuwa yakilalamikiwa kwa kushindwa kutekeleza majukumu ya kuhudumia wananchi na kutenda haki kwa walengwa waliowasilisha mashauri yao katika ofisi hizo.

Nakumbuka alisimamisha shughuli zote za mabaraza ya kata katika mkoa wa Dar es Salaam na kutangaza kuwa kesi zote zilizopo katika mabaraza hayo ziwasilishwe kwa makatibu tarafa.

Miongoni mwa watu waliofika kwa mkuu wa mkoa, walilalamikia pia viongozi na watendaji wa serikali za mitaa kwa kushirikiana na wavamizi wa maeneo.

Yupo mmoja wa waathirika alikaririwa na gazeti hili akieleza alivyokata tamaa ya kufuatilia kiwanja chake kilichovamiwa na watu wawili katika eneo la Madale, Manispaa ya Kinondoni.

Baba huyo mkazi wa Tegeta, anasimulia kuwa eneo lake liliuzwa na aliyekuwa mjumbe wa nyumba kumi. Alisimulia alivyokosa ushirikiano katika ofisi ya serikali ya mtaa kwa maana ya kufahamu majina ya watu waliouziwa eneo lake.

Lakini pia, alieleza alivyozungushwa na baraza la ardhi la kata, ikiwa ni pamoja na kutakiwa kutoa kile alichoelezwa ni nauli ya wazee wa baraza.

Matokeo yake, baba huyo amesema hajapata haki yake kwa sababu hana rasilimali fedha za kufuatilia ikiwamo gharama za kumlipa mwanasheria kwa ajili ya kufungua kesi.

Kwa hiyo amepokwa haki yake. Kwa kurejelea tukio la huyu bibi aliyepata haki yake baada ya miaka 43, ni wazi kuwa watu wote waliovamia maeneo ya watu sambamba na mamlaka zinazowakingia kifua zikidhani wameshinda, zinapaswa kujitafakari.

Vinginevyo hatua iliyochukuliwa na Waziri Lukuvi ndiyo dawa halisi ya wavamizi wote wa ardhi na inapaswa iwe endelevu ili wanyonge wapate haki yao

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

1 Comments

  • avatar
    kaliwa tito mkina
    15/09/2019

    mimi naipongeza sana selikali ya awamu ya tano kwa maamzi yake sahihi kwa wale wote wanaopenda kuitumia rushwa kuwakandamiza wanyonge naomba huo moto au hayo aliyoyaonyesha lukuvi yaendelee kutumiwa na viongozi wengine

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi