loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Shule Msingi zaandaliwa mtaala kuhifadhi misitu

WIZARA ya Maliasili na Utalii imeanza mchakato wa kuandaa mtaala utakaowezesha wanafunzi wa shule za msingi kuwa na misingi bora ya uhifadhi wa misitu nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kilichowahusisha wadau mbalimbali wa uhifadhi na misitu, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Ezekiel Mwakalukwa alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kubainika kutokuwepo kwa uhusishwaji wa moja kwa moja kwa shule za msingi kuhusu uhifadhi wa misitu ukilinganisha na shule za sekondari na vyuo.

Alisema mitaala ya sasa ya elimu ya msingi na sekondari haijumuishi elimu ya usimamizi wa maliasili na kwenye shule za msingi hakuna masuala ya moja kwa moja ya misitu.

“Ukiwa na kizazi ambacho hakijafundishwa vizuri kuona umuhimu wa hiyo misitu, uhifadhi na kuitumia vizuri, unakuwa na kizazi kitakachoona kuwa misitu ni hatari,” alieleza.

Dk Mwakalukwa aliongeza: “ Sisi sote ni mashahidi ukiwa na msitu katika mji watu wanapiga kelele wakitaka uondolewe kwa madai kuwa ni vichaka vinavyoficha vibaka.

Alisema kwa mtazamo huu wa kizazi chetu, maendeleo ni kukata miti na kuwa na msitu jirani au miti ni kutoendelea. Alisema ili kufikia azima hiyo, wizara inatarajia kuja na mada tatu za kuanzia zitakazohusisha misitu, tabia nchi na maji.

Dk Mwakalukwa alisema kutekelezwa kwa mradi huo kutasaidia kuongeza mwamko na stadi miongoni mwa wananchi kuhusu usimamizi endelevu wa misitu na kuchangia kuhifadhi mazingira.

Alisema kuwa mradi huo ni shirikishi na umehusisha wadau mbalimbali katika utekelezaji wake ikiwemo Shirika la Chakula Duniani (FAO) ambao ndilo mdhamini mkuu wa mradi huo.

Ofisa anayeshughulikia masuala ya ufundi kutoka FAO, Dk Maria Decristofaro alisema elimu itakayotolewa itawajengea uelewa watoto kuhusu misitu na uhifadhi mazingira. Alisema kuwa katika kuhakikisha mradi huo unakuwa na matokeo chanya, watashirikiana na idara husika kuufanikisha.

KAYA zilizobainika kuwa na historia ya kutochukua mara ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi