loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Aliyevujisha barua ya kuvunja makundi asakwa

WAKATI Waratibu Elimu Msingi wakiagizwa kuvunja kwa makundi sogozi (WhatsApp group), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Dk Semistatus Mashimba, ametangaza kumsaka aliyevujisha barua inayoagiza kuvunjwa kwa makundi hayo.

Barua hiyo tangu Agosti 19, mwaka huu, imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionesha kuwaelekeza waratibu kata wote kuvunja makundi yote ya sogozi yanayojihusisha na mawasiliano kwa walimu.

Agizo la kuvunjwa kwa makundi sogozi kwa walimu linakuja ikiwa Chemba inakumbukumbu mbaya ya kufutiwa matokeo ya darasa la saba kwa shule zote wilayani humo.

Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), lilifikia uamuzi huo baada ya kubainika undaganyifu uliofanywa na maofisa elimu ambapo nyezo iliyotumika katika udanganyifu huo ulikuwa ni makundi sogozi.

Chemba ina shule za msingi 103 ambapo wanafunzi 5,362 walijiandikisha kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka jana wakati wanafunzi 5,171 ndio waliofanya mtihani uliofutwa na NECTA.

Dk Mashimba alisema hatua hiyo ilichukuliwa kuepuka yaliyojitokeza mwaka jana ambapo shule za wilaya zote zilifutiwa matokeo ya mitihani ya darasa la saba. Alisisitiza kuwa sasa wanamsaka aliyevujisha barua hiyo.

“Mwaka jana makundi ya ‘WhatsApp’ yalibainika kutumika kuwasiliana na kuvujisha mitihani, jambo ambalo si kweli.

Hata hivyo, hiyo ilisababisha shule zetu zote 103 zifutiwe matokeo. Kutokana na hayo, tumeamua kuvunja makundi sogozi yote ya Waratibu Elimu na si ya watumishi wengine.” Alieleza. Alisema kwa sasa ofisi yake inafuatilia nani aliyepiga picha na kurusha barua hiyo kwenye mitandao.

“Waratibu Elimu Kata Chemba wapo 26 hivyo tunafuatilia kujua nani aliyefanya hivyo kwakuwa wapo wachache. Akibainika hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake,”alisema.

Barua hiyo iliyosainiwa na Josephat Ambilikile kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chemba, inaelekeza kuvunjwa kwa makundi hayo ya ‘Whatsapp’ yanayojihusisha na kutoa au kupokea taarifa zozote zinazohusu utendaji wa taaluma na utaalamu, zinazomgusa mwalimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba katika utendaji wake wa kila siku hadi hapo watakapojulishwa vinginevyo.

Katika barua hiyo ambayo nakala yake ilipelekwa kwa Walimu Wakuu,Waratibu Elimu Kata wote walitakiwa kuvunja makundi hayo hususani yanayotumika kutoa au kupokea taarifa zozote zinahusu utendaji kitaaluma.

“ Pia ofisi imebaini kuwepo kwa mkundi ya whatsapp katika halmashauri yetu yanayotoa na kupokea taarifa mbalimbali za kielimu na kijamii,” alisema.

Barua hiyo imetaja makundi hayo kuwa ni ya Walimu Wakuu waliovuliwa madaraka na Walimu Wakuu wapya, Walimu Wakuu waliopo madarakani, maofisa elimu kata na Walimu Wakuu ngazi ya kata na wilaya na mengineyo yanayofanana na hayo.

KAYA zilizobainika kuwa na historia ya kutochukua mara ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi