loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kikongwe wa miaka 94 ajinyonga

MKULIMA na mkazi wa Kijiji cha Gallu wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, Masatu Kezirahabi (94), amekufa kwa kujinyonga kwa kutumia mtandio siku sita tangu sehemu ya shamba lake itwaliwe na serikali ya kijiji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro amesema mwili wa mkulima huyo ulikutwa Jumapili saa 11 alfajiri ukining’inia juu ya mti wa mwembe, na umehifadhiwa Hospitali ya Nansio kwa uchunguzi zaidi.

Alisema wanaendelea kuchunguza sababu za kifo hicho kwa sababu hadi sasa sababu hizo Polisi hawana.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na mtoto wa marehemu, Obed Masatu na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Gallu, Bihemo Sebastian zilidai kuwa baada ya askari Polisi kupekua mwili wa Masatu walipata kipande cha karatasi kinachosadikiwa kuwa na ujumbe wa sababu za kifo chake, lakini hakijatolewa hadharani.

Kifo cha kikongwe huyo kimetokea siku sita tangu sehemu ya shamba lake inayokadiriwa kuwa ekari 200 kutwaliwa na Serikali ya Kijiji cha Gallu kwa madai kwamba alimiliki ardhi hiyo kinyume cha utaratibu.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Gallu, Bulemo Sebastian alisema mgogoro huo wa ardhi ulianza tangu mwaka 1992 baada ya Masatu kudai kumiliki ekari 200 za ardhi ya kijiji kinyume cha utaratibu.

“Tangu mgogoro huo uanze, Masatu alipotakiwa atoe vielelezo vya umiliki wa ardhi hiyo hakuviwasilisha tofauti na vielelezo vya umiliki wa ekari moja tu. Hivyo ndio sababu hapo Septemba 3, mwaka huu eneo hilo la ardhi lilitwaliwa na kumuachia ekari saba,” alisema Sebastian.

Mtoto wa marehemu, Obed amesema shamba lao halikuwa na ukubwa wa ekari 200 kama inavyoelezwa bali zilikuwa ekari 30, na baada ya sehemu ya shamba hilo kutwaliwa kinyume cha sheria wameachiwa ekari tatu.

Akifafanua alisema mgogoro wa umiliki wa shamba hilo kati ya baba yake na serikali ya kijiji uliamuliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza mwaka 1992 na baba yake kupata ushindi dhidi ya serikali ya kijiji.

Familia hiyo imesema haitakubali haki yao ipotee bure hivyo baada ya kumaliza matanga wanatarajia kutafuta haki yao hata ikibidi kwa njia ya kisheria kwa sababu nyaraka zote za umiliki wa ardhi hiyo zipo.

KAYA zilizobainika kuwa na historia ya kutochukua mara ...

foto
Mwandishi: Jovither Kaijage, Ukerewe

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi