loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Naibu Spika: Wanawake gombeeni uongozi

NAIBU Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan Juma, amewataka wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi katika majimbo ya uchaguzi na kuacha tabia ya kuwapigia kampeni wanaume kwa ajili ya kugombea nafasi hizo.

Mgeni alisema hayo katika mkutano wa kuwahamasisha wanawake kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani.

Mkutano huo wa uhamasishaji ulifanyika Magomeni katika uwanja wa Mzalendo, ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Zanzibar.

Alisema bado ushiriki wa wanawake katika uongozi na vyombo vya kutunga sheria ni mdogo ikiwemo katika majimbo ya uchaguzi.

Alisema katika majimbo ya uchaguzi 54, wanawake watano ndio waliogombea uwakilishi kwenye majimbo ya uchaguzi Zanzibar. Aidha, kwa upande wa nafasi ya ubunge, ni wanawake watatu walioshinda na kuongoza majimbo ya uchaguzi kwa upande wa Zanzibar.

‘’Bado uwakilishi wa wanawake katika uongozi ni mdogo kwakuwa nafasi zote tumekuwa tukiwaachia wanaume,’’ alisema. Alisema yapo mafanikio makubwa katika Baraza la Wawakilishi ambapo baadhi ya kamati za baraza zinaongozwa na wanawake.

‘’Tunazo kamati tatu za Baraza la Wawakilishi zinazoshikiliwa na wanawake walioonesha uwezo na ujasiri katika kufuatilia mambo mbalimbali kwenye wizara na taasisi zake,’’ alisema.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) Professa Issa Haji Ziddy, aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele kugombea uongozi na hakuna vikwazo kwa dini ya kiislamu kwamba inawazuia wanawake kuwa viongozi.

Alisema hata katika zama za mitume walikuwepo wanawake watano mashujaa ambao wametajwa kuwa ni watukufu kutokana na kazi kubwa ya kuipigania dini ya Mwenyezi Mungu iweze kusimama.

Aliwataka baadhi ya watu kuacha kuzitumia vibaya aya katika kitabu kitakatifu cha Kurani kwa kuzitafsiri kwa malengo na madhumuni yao.

‘’Ipo suratul Nisaa aya ya (34) ambayo inatafsiriwa wanaume ni viongozi wa wanawake wakati tafsiri sahihi ni ‘’Wanaume ni wasimamizi wa wanawake,’’ alisema.

Baadhi ya wanawake walikiri kuwepo kwa vikwazo na vitisho kutoka kwa waume zao wakati wanapoonesha nia ya kutaka kushiriki katika uongozi. Miongoni mwa matishio yanayotajwa ni talaka.

Tamwa Zanzibar inaendesha kampeni kuwashawishi wanawake kujitokeza kuwania uongozi katika harakati za uchaguzi mwakani.

WAZIRI wa Nchi Ofi si ya Rais, Tawala za Mikoa ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi