loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vitunguu swaumu vyapata soko nje

MKAKATI wa Serikali kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania nje unaendelea kuzaa matunda ambapo kwa sasa vitunguu swaumu vimepata soko kwenye nchi tisa. Ilielezwa bungeni jana kuwa vinauzwa vikiwa ghafi.

Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba ndiye aliyesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay (CCM) aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kutafuta soko la vitunguu swaumu nje ya nchi.

“Vitunguu swaumu vinauzwa katika nchi ya Shelisheli, visiwa vya Comoro, Msumbiji, Zambia, Mauritania, Kenya, Uganda na Falme za Kiarabu,” alisema.

Mgumba alisema katika kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya kilimo vikiwemo vitunguu swaumu, serikali imekamilisha upatikanaji wa simbomilia (barcode)pamoja na kubainisha viwango vya ubora kwa kulitumia Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Aidha, wizara imeanzisha kitengo cha masoko chenye jukumu la kuyatafuta ndani na nje ya nchi ikiwemo ya vitunguu swaumu.

Alisema wanayatafuta masoko hayo wakiwa wanajua viwango vya ubora wa bidhaa, bei na muda wa kuhitajika mazao hayo sokoni.

Hayo yote yanafanyika ili kuwa na taarifa sahihi za kuwapa wakulima waweze kuzalisha mazao yanayokidhi mahitaji ya soko.

Alisema, serikali kupitia Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) ilivijengea uwezo vikundi vya wakulima katika bonde la Bashay na kuviwezesha kusindika vitunguu swaumu.

“Jitihada hizo zimesaidia kuongeza thamani ya zao la vitunguu swaumu, muda wa kuvihifadhi bila kuharibika na kuimarisha soko la bidhaa hiyo ndani na nje ya nchi,” alisema.

Alisema wakulima na wasindikaji wa vitunguu swaumu wa Mbulu huwezeshwa kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam kila mwaka kutangaza na kutafuta masoko ya vitunguu swaumu na bidhaa zake ndani na nje ya nchi.

Alisema serikali kwa kushirikiana na asasi isiyo ya serikali ya Global Communities iliandaa kongamano la vitunguu swaumu lililofanyika katika bonde la Bashay Aprili 16, mwaka huu katika AMCOS ya Didihama ambapo wafanyabishara kutoka sehemu mbalimbali za nchi walialikwa kwa lengo la kutafuta soko la vitunguu saumu.

WAZIRI wa Nchi Ofi si ya Rais, Tawala za Mikoa ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi