loader
Picha

Jopo maalumu lamhudumia Askofu Mkuu Ruwai’chi

TAASISI ya Mifupa Muhimbili (MOI) imeunda jopo la madaktari na wauguzi saba, kumhudumia Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Thadeus Ruwai’chi (pichani) aliyefanyiwa upasuaji wa kuondoa damu kwenye ubongo, huku ikifafanua kwa kina tatizo lake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kiongozi wa jopo hilo, Profesa Joseph Kahamba ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, alisema pamoja na Askofu Ruwai’chi kuendelea kulazwa katika Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU), lakini anaendelea vizuri.

“Mpaka leo asubuhi tumemuona anaendelea vizuri, ameamka, anajitambua na kufuata maelekezo anayopewa, pia anazungumza kidogo akiulizwa,” alisema Profesa Kahamba.

Alisema jana walitengeneza jopo la madaktari saba, wanaohusika na tiba yake ikiwa ni daktari wa ubongo, wa usingizi, wa magonjwa ya ndani, wataalamu wa chakula na lishe, daktari wa mazoezi tiba na manesi.

Profesa Kahamba alisema askofu huyo kwa sasa anahitaji muda wa kutosha ili apumzike, hivyo waumini pamoja na ndugu ni vizuri kumpa nafasi ya kupumzika.

“Kwa sasa tungependa tumpe muda wa kupumzika tunashauri ndugu waandae kitabu ambacho watawapatia ndugu na watu wengine watakaokuja kumuona askofu wakija basi waandike humo kumtakia afya njema bila kumuona ili apate nafasi ya kupumzisha ubongo,” alisema.

Profesa Kahamba alisema tatizo linalomsumbua Askofu Ruai’chi linajulikana kitaalamu kama ‘Chronic Subdural Haematoma’ ambalo damu inakuwa imevuja kichwani na kusababisha mgandamizo kwenye ubongo.

Alisema vitu vinavyoweza kusababisha tatizo hilo havijulikani moja kwa moja, lakini inaweza kusababishwa na kuumia kichwani, shinikizo la damu kubwa linaloweza kusababisha mishipa kupasuka kichwani pamoja na matumizi ya baadhi ya dawa kwa muda mrefu.

“Tatizo hili usipopata tiba kwa haraka damu huendelea kuvuja kichwani na uzito wa damu kuzidi unaoendelea kuleta mgandamizo kwenye ubongo na athari kuongezeka hata kuleta kifo mgonjwa anapochelewa kupata huduma,” alisema.

Alizitaja dalili za tatizo hilo kuwa ni kichwa kuuma, kizunguzungu, kichefuchefu, upande mmoja wa mwili kukosa nguvu, kushoto au kulia.

Askofu Mkuu Ruwai’chi alifikishwa MOI usiku wa Septemba 9, mwaka huu, na baada ya uchunguzi alibainika kuwa anahitaji upasuaji mkubwa wa dharura, uliofanyika usiku huo kwa saa tatu.

Alipokelewa MOI akitokea Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi mkoani Kilimanjaro, alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kubainika kuwa anahitaji matibabu zaidi.

Viongozi mbalimbali na waumini wa kanisa hilo, walifika MOI kumjulia hali mgonjwa huyo. Rais John Magufuli ni alifika MOI juzi kumuona na kumuombea apone haraka.

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda amesema kama Rais John Magufuli ...

foto
Mwandishi: Regina Mpogolo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi