loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JKCI kujenga jengo jipya Mloganzila

SERIKALI kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), imejizatiti kuboresha na kupanua miundombinu ya JKCI ili kuifanya taasisi hiyo kuwa taasisi mahiri ya tiba ya magonjwa ya moyo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Akizungumza na waandishi wa habari walipotembelea Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, kupata taarifa zinazohusu eneo litakapojengwa jengo jipya kwa ajili ya upanuzi wa taasisi hiyo, Ofisa Mipango wa JKCI, Vida Mushi alisema kwa sasa taasisi ina ufinyu wa eneo, ukilinganisha na idadi ya wagonjwa wanaopata matibabu katika taasisi hiyo.

“JKCI inaona wagonjwa kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, ujenzi wa upanuzi wa jengo jipya la JKCI katika eneo la Mloganzila umelenga kuifanya JKCI kuwa taasisi mahiri ya tiba ya magonjwa ya moyo Kusini mwa Jangwa la Sahara,” alisema Mushi.

Aidha, alisema kwa sasa JKCI imewapokea wawakilishi kutoka China Academy of Building Research, waliokuja kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu eneo la Mloganzila ikiwa ni maandalizi ya ujenzi wa jengo jipya la JKCI.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori aliipongeza serikali kupitia JKCI, kuhakikisha matibabu ya magonjwa ya moyo, yanapewa kipaumbele ukizingatia magonjwa ya moyo ni magonjwa yanayokua kwa kasi.

“Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya matibabu ya watu wenye magonjwa ya moyo nje ya nchi, huduma hizi kusogezwa karibu na wananchi ni jambo la neema na itawasaidia wananchi wengi kutokulazimika kutumia gharama nyingi kwenda kutibiwa magonjwa ya moyo nje ya nchi,” alisema Makori.

Aidha, Makori alisema Manispaa ya Ubungo imewapokea wataalamu kutoka China Academy of Building Research kupata taarifa zinazohusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa upanuzi wa JKCI wa awamu ya pili eneo la Mloganzila na kutoa ushirikiano kwa kuwapatia taarifa zilizojitosheleza ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

“Baadhi ya taarifa walizotaka kufahamu wakati wa upembuzi wa eneo la Mloganzila ni pamoja na miundombinu iliyopo katika eneo la Mloganzila, upatikanaji wa maji, upatikanaji wa umeme na vibali vyote vinavyohusika na ujenzi, tutaendelea kutoa ushirikiano katika hatua zote za ujenzi wa mradi huo kwani ni mradi wa maendeleo kwa nchi yetu katika utoaji wa huduma za afya,” alisema Makori.

WAZIRI wa Nchi Ofi si ya Rais, Tawala za Mikoa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi