loader
Picha

Kampuni za Misri zawekeza tril 2/- Tanzania

SERIKALI imesema kampuni 22 kutoka nchini Misri zimewekeza nchini zaidi ya Dola za Marekani milioni 900 sawa na Sh trilioni 2.068 hali iliyosaidia kuongeza ukuaji wa biashara na uchumi.

Aidha, biashara kati ya Tanzania na Misri imekua kwa asilimia 75 baada ya Misri kuingiza nchini, bidhaa mbalimbali zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 42 (Sh bilioni 97) kutoka bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 24 mwaka 2017.

Pia mzunguko wa biashara kati ya Tanzania na Misri ni Dola za Marekani milioni 78.

Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, wakati akifungua Wiki ya Biashara ya Misri iliyoanza jana hadi Septemba 14, mwaka huu.

Balozi Mwinyi alisema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuhamasisha kampuni nyingi za Misri kuwekeza nchini kwa lengo la kuboresha mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizo.

Alisema sekta binafsi ina mchango mkubwa katika biashara na uwekezaji hivyo wamesaidia kuinua uchumi.

“Maonesho haya yatakuwepo kwa siku tano na wataonesha bidhaa zao ili kupata wabia kutoka Tanzania na bidhaa walizonazo ni za dawa na vifaa tiba, vifaa vya umeme, vifaa vya ujenzi na kemikali,” alisema Mwinyi.

Alisema maonesho hayo ni fursa muhimu kwa wafanyabiashara wa Tanzania kujionea na kufanya mazungumzo na kampuni za Misri ili kujenga ushirikiano wa kibiashara kwa sababu mahusiano hayajafikia viwango wanavyotaka.

Mkurugenzi wa Huduma za Wanachama na Usimamizi wa Sera kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Zachy Mbenna amesema uwekezaji uliofanywa na Misri wa Dola za Marekani milioni 900 umesaidia kutengeneza ajira na kuongezeka kwa biashara na uwekezaji kwa nchi zote mbili.

Mbenna alisema kampuni zao zimewekeza katika viwanda vya dawa na kemikali, viwanda vya kuchakata chakula, nguo, sukari, vifaa vya ujenzi, viwanda vya nyama na ngozi pamoja na kilimo na vifaa vya umeme.

 TANGU mwishoni mwa wiki iliyopita bei ya gesi inayotumika kwa ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel na Lovin Kefa, Tudarco

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi