loader
Picha

Mahitaji ya nazi yaongezeka

ZAO la nazi zinazozalishwa bado halikidhi mahitaji ya soko la ndani ya nchi kutokana na kuongezeka la matumizi yake ikiwemo ulaji wa madafu. Tanzania ni nchi ya 10 duniani kwa uzalishaji nazi ikiongozwa na Indonesia.

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni na Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Zaynab Vullu ambaye amesema zao hilo lina faida nyingi kuanzia mti na matawi.

Vullu amehoji ni lini serikali itatafuta soko la kudumu la zao hilo na ina mpango gani wa kuhamasisha kilimo cha zao kama ilivyokuwa zamani.

Akijibu swali hilo, Mgumba amesema soko la kudumu la zao hilo lipo nchini kwa sababu kiasi cha nazi kinachozalishwa hakikidhi mahitaji soko la ndani.

Alisema pia mafuta ya mwali yanayotokana na nazi yanaendelea kupata umaarufu kutokana na uhitaji wake kuwa mkubwa ndani na nje ya nchi ambapo lita moja inafikia hadi Sh 40,000.

"Bidhaa kama fagio, mbao, kamba na thamani za mti wa mnazi na uwezo wa zao hilo kutunza mazingira huongeza thamani ya zao la minazi," alisema.

Alisema kuimarisha soko la zao hilo nchini msimu wa mwaka 2018/19 wakulima 74 mikoa ya Lindi na Mtwara wamefundishwa kukamua mafuta ya mwali.

Alisema kikundi cha wanachama 50 katika wilaya ya Bagamoyo kimepewa mashine yenye uwezo wa kukamua lita 500 za mafuta mwali kwa mwaka.

"Aidha, serikali inaendelea kuimarisha masoko ya mazao yote ya kilimo likiwemo zao la nazi kwa kuwaunganisha wakulima na wanunuzi kupitia vyama vya ushirika, masoko ya moja kwa moja na viwanda vidogo vya kuongeza thamani ya zao la nazi," alisema.

Alisema, serikali inaendelea kutoa elimu kwa wazalishaji wa zao la nazi kupanda mbegu bora zenye ukinzani kwa magonjwa na zenye tija kubwa.

Alisema Tanzania ni nchi ya 10 duniani kwa uzalishaji wa nazi ikiongozwa na Indonesia na kwa Afrika ni ya kwanza ambapo huzalisha tani 530,000 za nazi kwa mwaka ikifuatia Ghana inayozalisha wastani wa tani 366,183.

Aidha, alisema serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha minazi ambapo imeanzisha shamba la hekta 54 kituo kidogo cha utafiti cha Chambezi wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani ili kuzalisha miche bora ya minazi yenye ukinzani kwa ugonjwa wa kunyong'onyea kwa nazi na kuisambaza kwa wakulima kwa gharama nafuu.

Mgumba alisema serikali inahamasisha kilimo cha minazi katika maeneo mapya ili kuongeza uzalishaji wa nazi nchini ambapo msimu wa mwaka 2018/19 ilizalisha na kusambaza mbegu 11,000 kwa wakulima Rukwa na Mwanza.

"Serikali inafanya mazungumzio na Jumuiya ya Asia (APCC), ambayo hutunza germplasm ya minazi kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora za minazi zenye kuongeza tija kwa wakulima,"alisema.

 TANGU mwishoni mwa wiki iliyopita bei ya gesi inayotumika kwa ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi