loader
Picha

Huduma hafifu maabara chanzo tiba kienyeji

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile amesema watu wamekuwa wakitibiwa kienyeji katika vituo vya kutolea huduma za afya kutokana na huduma za maabara kutofanya vizuri.

Dk Ndugulile ameyasema hayo wakati anazindua Bodi ya nane ya Maabara Binafsi za Afya jijini Dodoma.

Amesema kwa sasa vituo vingi vya afya vimekuwa vikitibu wagonjwa wengi kwa magonjwa yasiyosahihi kutokana na kukosekana kwa ufanisi katika huduma za maabara.

"Kwetu sisi kama wizara maabara ni moyo wa huduma za afya kwa sababu inatoa mwelekeo wa matibabu kwa mgonjwa, daktari anaweza kuwa na mitizamo mitatu, watu wa maabara wanajibu kwa kuthibitisha mgonjwa ana tatizo gani,”amesema.

Amesema kwa sasa huduma za maabara zimekuwa zikitumika kufanya biashara na kuwa chanzo cha mapato kwa vituo vya kutolea huduma, hivyo kuacha wajibu wa msingi wa kufanya uchunguzi wa magonjwa.

"Mgonjwa anaenda anaambiwa una malaria plus plus, hii maana yake ni nini, tunatibu wagonjwa wengi kwa magonjwa yasiyo sahihi, zaidi ya asilimia 70 ya homa wanasema ni malaria wala sio malaria, watu wanakunywa dawa sana pasipo kuzingatia misingi," alifafanua.

Aidha, Dk Ndugulile pia alikemea tabia iliyoanza kuibuka kwenye maabara ya kuacha kutoa huduma za kimaabara, badala yake kutoa tiba na hata kufanya upasuaji.

Dk Ndugulile pia ameitaka bodi hiyo kwenda kutafakari na kuona namna ya kuja na mchakato wa mabadiliko ya sheria ambayo ni ya muda mrefu ili iende na wakati.

Pia aliwataka kutafakari ili kuangalia namna ya kuongeza majukumu ya bodi kwa kutosimamia maabara binafsi pekee bali hata maabara za vituo vya kutolea huduma za umma, ambazo pia baadhi yake zimekuwa hazifanyi vizuri.

Pia aliitaka bodi hiyo kwenda kukabiliana na tatizo la uanzishwaji holela wa maabara kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kuangalia kuwa zinafanya usajili na kutoa huduma kulingana na matakwa ya sheria na utaratibu unaotakiwa.

Dk Ndugulile pia aliitaka bodi hiyo kuja na kanzidata ya maabara na maduka yanayouza vifaa vya maabara na vitendanishi, ili ifahamike yako mangapi na yanafanya nini.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi, Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Said Abood aliahidi bodi yake itakwenda kuzishughulikia changamoto zote alizozibainisha na zingine katika huduma ya maabara na maduka ya vifaa vya maabara ili kuhakikisha huduma hiyo inaimarika na kuleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma za afya hapa nchini.

Rais John Magufuli amepokea hati ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi