loader
Picha

CHINA KWA MACHO YANGU: Juhudi za China kutokomeza umasikini uliokithiri zaonyesha mafanikio

Tangu sera ya mageuzi na kufungua mlango ilipoanza kutekelezwa mwishoni mwa mwaka 1978, China imepata mafanikio makubwa katika kupunguza umasikini.

Kwa mujibu wa vigezo vya kimataifa vya kupunguza umasikini, idadi ya watu wa China wanaokumbwa na umasikini imepungua kwa kiasi kikubwa. Takwimu za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa, mwaka 1981, asilimia 84 ya watu wa China waliishi chini ya mstari wa kimataifa wa umasikini wa matumizi ya dola 1.25 kwa siku.

Hata hivyo, hadi kufikia mwaka 2018, wachumi walitangaza kuwa China iliwakomboa watu milioni 700 kutoka kwenye umasikini. Ikiwa nchi kubwa zaidi inayoendelea duniani, China kwa sasa imeshuhudia mabadiliko yaliyoletwa na jitihada za kuondoa mamilioni ya raia wake kutoka kwenye umasikini.

Mipango ya China ya kupunguza umasikini, imefanikisha ndoto ya kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo yaliyokuwa na umasikini, imepunguza pengo la maendeleo kati ya mikoa mbalimbali na kuboresha uzalishaji na hali ya maisha ya watu masikini.

Ama kwa hakika, suala la kuwatoa watu katika umasikini limekuwa jambo linalopewa kipaumbele kwa mfululizo tangu mageuzi yalipoanza kuongozwa na kiongozi mkuu wa zamani wa China, Deng Xiaoping.

Rais wa sasa wa China Xi Jinping, ameweka mwaka 2020 kama mwaka ambao nchi yake inatarajia kutokomeza umasikini na kujenga jamii yenye maisha bora kwa pande zote ijulikanayo kwa lugha ya kichina kama “Xiaokang” maana yake ni maisha bora ya kiwango cha kati. “Hakuna yeyote atakayeachwa nyuma katika safari ya kuelekea ‘Xiaokang’” Rais Xi amekuwa akisisitiza.

Ndoto hii imenakiliwa vizuri katika kitabu chake kiitwacho “Kuondoa Umasikini” ambapo anasema kwa vyovyote vile “lazima tutokomeze umasikini unaopatikana katika akili zetu kabla ya kuuondoa katika mikoa tunayoongoza, kabla ya kusaidia watu na taifa kujikomboa kutoka kwenye umasikini na kurejea kwenye njia ya ustawi.”

Ni rahisi kuona kwa nini hili lilibaki kuwa lengo kuu. Kwa miaka mingi, China ilikabiliwa na umasikini uliokithiri kutokana na historia, asili yake na hali ya kijamii. Umasikini uliokuwepo ulitajwa kuwa kizingiti kikubwa katika nia ya China ya kujenga jamii yenye maisha bora.

Watu masikini hawakuishi tu kwenye umasikini kutokana na kipato cha chini, bali walikuwa wanakabiliwa na matatizo kama vile kupata maji, barabara, umeme, elimu, matibabu na mikopo.

Jamii masikini iliishi katika vijiji vilivyokumbwa na hali ngumu ya maisha, kwenye maeneo yaliyokumbwa na majanga ya asili na sehemu zilizokuwa na miundombinu duni. Kiasi cha uwekezaji na msaada kutoka serikalini hakikuweza kutatua tatizo la kimsingi.

Baada ya muda, serikali ya China ilifanya utafiti kuhusu sera za kupunguza umasikini kwa kuzingatia viwango anuwai, kutoka kwa watu masikini pamoja na vijiji, wilaya na mikoa iliyozongwa na ufukara.

Juhudi zilizoongozwa na serikali za kuondoa umasikini zikageuzwa kutoka misaada ya kiuchumi katika miaka ya 70 na 80, na kuanza kuzingatia kuboresha uwezo wa watu masikini kujiendeleza ili kuondoa umasikini na kuwezesha vijiji na jamii zao kupata maendeleo.

Mwaka 1986, kwa mfano, serikali ya China ilianzisha taasisi maalum kwa ajili ya kupambana na umasikini.

Ilipoanza kutekeleza mipango mahususi ya kupunguza kiwango cha umasikini, vita dhidi ya umasikini nchini China iliingia zama mpya. Muda mfupi baadaye lengo likabadilika kutoka kupunguza umasikini kupitia msaada hadi kupunguza umasikini kwa njia ya kujiendeleza.

Moja kwa moja China ikaanza kuchunguza miradi ya kusaidia kupunguza umasikini kimaendeleo. Mbinu hii ililenga kutumia maliasili katika maeneo masikini kuongeza uzalishaji na serikali kutoa msaada kwa familia masikini.

Watu katika maeneo haya walipozidi kujiendeleza na kujifunza jinsi ya kuongeza uzalishaji, waliweza kujitoa katika umasikini wao wenyewe.

Kujiendeleza kwa kupunguza umasikini pia kujihusisha hatua nyingine mbalimbali kama vile kuboresha miundombinu, kukuza maendeleo ya elimu na huduma za afya pamoja na utoaji wa sera za mikopo zenye upendeleo kwa wenyeji.

Eneo la Xiangxi kwenye Jimbo la Hunan, kwa mfano, lilikuwa sehemu masikini zaidi ambapo watu zaidi ya milioni 1.5 waliishi chini ya mstari wa umasikini katika miaka ya 80. Asilimia 84 walikuwa wakiishi maisha ya dhiki, na kuondokana na umasikini kulikuwa ndoto ya kila mtu aliyeishi katika eneo hilo.

Marekebisho yaliyotekelezwa kwa utaratibu maalum, yaliwezesha kupunguzwa kwa hali ya umasikini kwa kuongeza tija na kuboresha miundombinu ya msingi katika maeneo ya vijijini. Hii ilifanyika kupitia kwa mfumo wa kuleta mageuzi kwa bei ya mazao ya kilimo na maendeleo ya miji na vijiji.

Tangu mwaka 2000, vijiji vya mbali vilivyokuwa na umasikini zaidi vililengwa kwa ajili ya kupunguza umasikini. Wakati huu, mkakati ulihusisha maendeleo ya viwanda, miundombinu, ikolojia na mafunzo ya kazi. Miradi mikubwa ya viwanda ilipewa kipaumbele katika maeneo ya vijijini.

Kwa ujumla, hii ilisababisha maendeleo ya viwanda ikiwa ni pamoja na kilimo cha kiwango kikubwa cha matunda ya kiwi, chai, maua, tumbaku na mitishamba ya tiba ya jadi ya Kichina iliyochukua maelfu ya hekari.

Historia ya kupunguza umasikini katika eneo la Xiangxi ya zaidi ya miaka 30 ni mfano wa jinsi China ilivyopigana na janga la umasikini kwa ujumla. “China ni nchi ya kwanza kufikia malengo ya maendeleo ya milenia. Maendeleo yake, hasa katika suala la kupunguza umasikini ni mchango mkubwa kwa ulimwengu,” Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon alisema.

Baada ya miongo ya majaribu na matatizo, vita ya kupunguza umasikini nchini China imepata matokeo yanayoleta matumaini.

China kamwe haitakoma kujaribu kufikia lengo lake la kuwa na jamii isiyo na umasikini ifikapo mwaka 2020.

TUME ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) imevitaka vyuo vikuu vyote ...

foto
Mwandishi: MWANDISHI MAALUM

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi