loader
Picha

KOMBE LA DUNIA QATAR 2022

TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, wiki iliyopita ilikata tiketi ya kucheza hatua ya pili ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar 2022 baada ya kuifunga Burundi kwa penalti 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ilibidi kuamriwa kwa mikwaju ya penalti tano tano baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Bujumbura, Burundi na ule wa marudiano Jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa.

Baada ya timu hizo kucheza katika muda wa kawaida wa dakika 90 na kuwa sare kwa kufungana bao 1-1 na hata baada ya kuongezewa dakika 30 matokeo yakaendelea kuwa hayo hayo na utaratibu wa penalti ndio ukatumika kumpata mshindi wa jumla wa mchezo huo.

SHANGWE KILA KONA Watanzania baada ya ushindi huo walilipuka kwa furaha huku kipa Juma Kaseja akiwa gumzo kutokana na uhodari wake wa kuokoa penalti ya kwanza ya Warundi, ambayo aliipangua.

Baada ya Kaseja ku pangua penalti ile, wachezaji watatu wa Tanzania walipata penalti zao huku wapinzani wao wakiendelea kukosa na hivyo kuishia kupiga penalti tatu tu kwani hata wangepata mbili zilizobaki, wasingeweza kuwafikia Taifa Stars, ambao tayari walikuwa mbele kwa penalti 3-0.

Shangwe zilitimka kila kona kuanzia uwanjani, barabarani, majumbani na kila sehemu wakifurahia timu yao kutinga hatua ya makundi ya kusaka nafasi ya kucheza kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia, ambazo zitafanyika Qatar 2022.

Wengine walishangilia wakifikiri kuwa tayari Tanzania imefuzu kucheza kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar, ukweli ni kwamba tumevuka kizingiti cha kwanza na vimebaki viwili mbele yetu kabla ya kwenda Qatar.

HATUA YA AWALI Tanzania pamoja na nchi zingine 27, zilitakiwa kwanza kucheza raundi hiyo ya awali ya kufuzu kabla ya kutinga hatua ya makundi baada ya nchi yetu kuwa miongoni mwa mataifa yaliyopo katika viwango vya chini vya ubora wa soka katika Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) katika mwezi Julai.

Baada ya kumalizika kwa hatua ya kwanza ya kufuzu, timu 14 zitaungana na zingine 26, ambazo hazikucheza katika hatua hiyo ya awali na kuweka katika makundi 10, ambapo kila kundi litakuwa na timu nne.

KAZI BADO KUBWA Tunaweza kusema kuwa kazi ndio kwanza imeanza katika mbio hizo za kusaka tiketi ya kucheza fainali za 22 za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar kuanzia Novemba 21 hadi Desemba 18, 2022.

Kazi ndio kwanza imeanza kwani katika hatua hiyo ya makundi, ambayo itashirikisha mataifa 40 kwa Kanda ya Afrika, ambayo yatapangwa katika makundi 10 yenye timu nne kila moja, ambapo mshindi wa kila kundi, atacheza raundi ya tatu ya kufuzu.

Raundi ya tatu ya kufuzu ndio ya mwisho, ambayo itakuwa na jumla ya timu 10 na timu hizo kila moja itacheza mechi mbili, ya nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla wa mechi hizo mbili, ndio atakuwa amefuzu kwenda Qatar 2022.

RATIBA YA MAKUNDI Ratiba ya makundi bila shaka itakuwa ngumu zaidi kuliko ile ya awali, ambapo Taifa Stars ilicheza dhidi ya Burundi na kuiondoa kwa penalti.

Bado hatutajua katika makundi Taifa Stars ita pangwa na nani na hakuna shaka kuwa huenda ikaangukia kwa vigogo wa soka barani Afrika kama Algeria, Misri, Nigeria, Cameroon, Ivory Coast, Senegal na zingine.

Sasa tunachotakiwa kufanya ni kujiweka tayari kwa kukabiliana na yeyote bila kujali ukubwa au umaarufu wao, hivyo maandalizi ya mapema na ya uhakika yanatakiwa kwa timu yetu kwa ajili ya hatua hiyo ya makundi.

Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) lazima lianze maandalizi mapema kwa kushirikiana na serikali ili kuhakikisha wanapata fedha mapema kwa ajili ya maandali hayo hata ikiwezekana yafanyikie nje ya nchi.

Mfano wa ugumu wa mechi hizo za kufuzu tumeona baada ya Burundi, ambayo wengi walikuwa wakiidharau, kututoa jasho hadi mshindi akapatikana kwa mikwaju ya penalti.

Hivyo, tujipange vizuri tusije kuwa kapu la magoli. RAI KWA WOTE Kwa umoja wetu tunatakiwa kuungana na kushirikiana ili kuhakikisha Taifa Stars inapata kila kinachotakiwa kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo ya kufuzu ili tuvuke hatua inayofuata.

Hilo linawezekana kama tutahakikisha tunapata ushindi kwenye mechi zetu zote za nyumbani na kupata matokeo ya kuridhisha kwenye mechi za ugenini ili kujikusanyia pointi.

Tunatakiwa kuhakikisha tunapata mechi za kutosha za kirafiki tena zile za maana (kucheza na timu zenye viwango vya juu) ili tuweze kutumia na kujua wachezaji wengine ambao hawajapata nafasi ya kucheza na pia itatusaidia kupata muunganiko mzuri kwenye timu yetu ya taifa.

Rai yangu kwa Watanzania, tuungane kwa pamoja na kuipa hamasa kwa kujaza Uwanja wa Taifa kila timu yetu inapocheza kwenye uwanja huo, iwe mechi za kirafiki au za kimashindano ili kuwatia moyo wachezaji wetu.

Hamasa imekuwa chachu ya ushindi katika soka mfano mzuri ni klabu ya Simba katika msimu uliopita kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, hamasa waliopewa na mashabiki wao iliwafanya wafanye vyema hadi kufikia robo fainali ya michuano hiyo.

Kikubwa TFF kwa kushirikiana na Serikali kuhakikisha wachezaji wanapata huduma bora ili kuongeza chachu ya kufanya vizuri ili kuandika historia mpya katika soka letu kwa kufuzu kucheza mashindano hayo makubwa kabisa duniani.

foto
Mwandishi: Bernard Kweka, Turdaco

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi