loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ukame Bonde la Kati uchochee uangalifu matumizi ya maji

MOJA ya vitu ambavyo vinaelezwa kuwa huenda vikaibua vita ya tatu ya dunia ni maji.

Maji, moja ya mahitaji makubwa ya binadamu yanazidi kupungua kwa jinsi binadamu wanavyoongezeka na pia anavyozidi kuharibu mazingira.

Kiukweli wakati bindamu wanazidi kuongezeka na shughuli zao kuongezeka, matumizi ya raslimali maji yanazidi kuongezeka huku vyanzo vyake vikiendelea kudidimia.

Kutokana na ukweli huo sisi tunaungana na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo ya kuwasihi wakazi wa Bonde la Kati kuhakikisha wanatumia kwa uangalifu mkubwa maji yaliyopo ili yatosheleze wakati wote.

Rai hiyo ya Profesa Mkumbo aliyoitoa juzi mjini Singida wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Wadau wa Bodi ya Maji wa Bonde la Kati linalojumuisha mikoa ya Dodoma, Manyara, Singida, Tabora, Arusha, Shinyanga, Kilimanjaro na Simiyu lenye ukubwa wa jumla ya kilometa za mraba zaidi ya 143,000, ni hadhari tosha kwa wananchi na watu wengine kuona umuhimu wa kuhifadhi maji na vyanzo vyake.

Ni kweli kuwa Bonde la Kati ni kame,lakini pamoja na ukweli huo kuna ongezeko la mahitaji ya rasilimali hiyo kwa matumizi ya majumbani na kilimo hivyo wakazi wa mikoa husika hawanabudi kuyatumia vizuri maji yaliyopo na kudhibiti uharibifu na uchafuzi wa vyanzo vyote vya maji.

Mfano uliotolewa wa lita 100 zinazotumika kwenye umwagiliaji kwamba lita 30 tu ndizo zinazotumika vizuri huku lita 70 zikipotea, si tu mfano, bali elimu tosha ya kuanza kuangalia taratibu zetu za kutumia rasilimali hii haba duniani.

Ni kweli kama, alivyosema Katibu Mkuu hali hii ya uharibifu, matumizi yasiyo na uwiano wala ufanisi yanaweza kusababisha migogoro ya maji ya mara kwa mara hasa kipindi cha kiangazi hivyo ni vyema tukatuliza vichwa vyetu na kuwa makini katika kupanga na kutumia maji.

Tunapaswa kutambua kwamba Bonde la Kati linapata mvua kwa siku 50 tu kwa mwaka ambayo ni sawa na milimita 400 - 600 katika eneo la Kusini la Bonde mikoa ya Tabora, Dodoma, Singida na Shinyanga ambako eneo la Kaskazini la Bonde mikoa ya Manyara na Arusha ni milimita 800 -1,200 tu kwa mwaka, hivyo kufanya masikhara ni kuua maisha yetu.

Pamoja na takwimu hizo kuonekana kuwa za kawaida, ukweli ni kuwa mvua hizo huzalisha kiasi cha maji mita za ujazo milioni 6,970 tu kwa mwaka ambayo kiuhalisia hayatoshi kwa idadi ya watu milioni 7.13 wanaokadiriwa kuwepo ndani ya Bonde la Kati.

Japokuwa maelekezo yanatakiwa kuhusu namna bora ya utumiaji wa maji iko haja ya msingi na ya wazi kabisa kwa wananchi kujifunza kutumia Kilimo tofauti cha umwagiliaji na matumizi ya maji, msingi mkubwa ukiwa ni kuhifadhi vyanzo vya maji na pia kutumia raslimali hiyo kwa utaratibu endelevu.

UCHAGUZI Mkuu wa madiwani, wabunge, wawakilishi, Rais wa Zanzibar na ...

foto
Mwandishi: Tahariri

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi