loader
Picha

Songea wapata Naibu Meya mpya

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, limemchagua Asia Chikwale kuwa Naibu Meya mpya wa manispaa hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja.

Meya wa Halmashauri ya manispaa hiyo, Abdul Mshaweji ameongoza kazi ya uchaguzi wa Naibu Meya katika mkutano wa Baraza la Madiwani hao uliofanyika kwenye Ukumbi wa Manispaa ya Songea.

Kikao hicho pia kimewashirikisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Tina Sekambo na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema pamoja na watumishi wa idara na vitengo wa manispaa hiyo.

Mshaweji alieleza umuhimu wa uchaguzi katika kulijenga Taifa kwa kuwa kiongozi anayechaguliwa atashirikiana vyema na viongozi wa serikali na wananchi kuleta maendeleo ya Manispaa ya Songea na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Naibu Meya aliyemaliza muda wake, Judith Mbogoro alitoa shukrani kwa madiwani wote na viongozi mbalimbali wa Manispaa ya Songea kwa ushirikiano aliupata katika kipindi chote alichokuwa Naibu Meya na ameahidi kuwa atakuwa pamoja na kiongozi aliyechaguliwa ili kuhakikisha manispaa hiyo inasonga mbele.

“Najitambua na kujijua nitatoa ushirikiano daima,” alisema Mbogoro. Naye Naibu Meya mpya, Asiah Chikwale alisema nafasi aliyoipata ataitumia vizuri kwa kushirikiana na viongozi wengine kuleta maendeleo ya Manispaa ya Songea, Mkoa na Taifa kwa ujumla wake.

Manispaa ya Songea ina kata 21 na mitaa 95 ikiwa na jumla ya madiwani 28. Wakati huo huo, Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma imekagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Ruvuma katika Manispaa ya Songea na kuridhishwa na hatua za ujenzi unaotarajiwa kukamilika wakati wowote.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Oddo Mwisho alisema serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ukiwemo wa vituo vya afya ili kusogea huduma kwa wananchi.

Aliagiza watendaji wa manispaa kuhakikisha wanaanza huduma mara moja katika kituo kwani wananchi wanachosubiri ni kuanza kupata huduma jirani hali itakayopunguza msongamano Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Dk Mamerita Basike alisema walipokea fedha kutoka serikalini Sh milioni 400 kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Ruvuma Juni 24, 2018.

Dk Basike alisema mradi huo umekamilika kwa kazi zote ambazo ziliainishwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI na kwamba kinachosubiriwa hivi sasa ni ununuzi wa vifaa tiba na dawa ili huduma zianze kutolewa.

Aliyataja majengo manne yaliyokamilika katika kituo hicho kuwa ni la wagonjwa wa nje, la mama na mtoto, la upasuaji, la maabara, ujenzi wa shimo la choo na shimo la kondo la nyuma na ujenzi wa kichomea taka.

“Halmashauri imeomba vifaa na madawati kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI ili kituo cha afya kianze kutumika kituo hiki kitahudumia wananchi wa kata za Ruvuma, Mateka, Majengo, Subira, Mfaranyaki na Lizaboni,” alisema.

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Maalumu, Songea

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi