loader
Picha

Meli kuleta magari 600,000 Dar

UTEKELEZAJI wa mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam katika gati jipya la kuhudumia meli za magari la Ro-Ro, unaiwezesha bandari hiyo kupokea magari 600,000 kwa mwaka kutoka magari 163,000.

Katika kudhihirisha uwezo huo, juzi saa nne usiku kwa mara ya kwanza, bandari hiyo ilipokea meli kubwa ya kwanza iitwayo Grand Duke ikitoka Kenya, iliyotia nanga bandarini hapo kupakua magari 1,347 mengi yakitoka China na Japan.

Akielezea mafanikio hayo kwa waandishi wa habari jana, Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko, mbele ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, aliyefika bandarini hapo kujionea meli hiyo, alisema mafanikio hayo yanaiweka bandari hiyo pazuri na ni juhudi za Serikali ya Rais John Magufuli.

Akifafanua kuhusu gati hiyo mpya, Kakoko alisema, “Leo tumepokea meli inayotoa magari 1,347. Hii ni mara ya kwanza kwa meli kubwa namna hii kutia nanga hapa kwetu na inatokana na utekelezaji wa upanuzi wa bandari yetu. Gati hili jipya limejengwa kwa zege, lina urefu wa meta 320”.

Kakoko alisema kukamilika kwa gati hilo, linaloitwa pia sifuri (Zero)likiwa maalum kwa kushusha magari, kunaiwezesha bandari hiyo sasa kupokea magari 600,000 kwa mwaka. Alisema mwaka jana bandari hiyo ilipokea magari 163,000 pekee.

Kwa mujibu wa Kakoko, upanuzi huo umefanyika kwa miaka miwili na leo, Septemba 16, mkandarasi ataikabidhi TPA mradi huo ili kuendelea kupokea meli. Alisema sasa meli itashusha mzigo wa magari kwa saa 12 na kuipisha meli nyingine na malengo ni meli zitoke nchi za Ulaya na Asia (China na Japan) moja kwa moja mpaka bandari ya Dar es Salaam. “Gati hili ni kubwa, la kisasa, litakuwa na taa kubwa.

Kazi itafanyika kwa siku saba kwa saa 24. Juhudi za Rais Magufuli zimetufikisha hapa. Huwa anatufuatilia hazipiti wiki mbili hajasema bandarini kuna nini, au kutuuliza miradi imefikia wapi,” alisema Kakoko.

Kwa upande wake, Waziri Kamwelwe alisema ukarabati wa bandari hiyo umefanikisha magati mawili kati ya manane kukamilika na gati hilo sifuri lililo maalum kwa magari linawezesha bandari hiyo kutimiza malengo ya kupokewa mizigo tani milioni 25 kutoka mizigo tani milioni 17 ya sasa.

Kamwelwe alizitaka nchi za SADC kuitumia bandari hiyo kikamilifu na kusisitiza kuwa bandari hiyo ni yao na maboresho mengine yote yanaendelea ikiwamo bandari kavu na mifumo ya huduma za kimtandao (soft ware service).

 TANGU mwishoni mwa wiki iliyopita bei ya gesi inayotumika kwa ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi