loader
Picha

'Mawakili wamelundikana mijini'

JAJI Mkuu Mstaafu, Othman Chande amesema licha ya ongezeko la mawakili kila mwaka nchini, bado kuna upungufu wa mawakili wa kujitegemea katika mikoa ya Lindi, Rukwa, Katavi, Ruvuma, Kigoma na Mara huku wengi wakitajwa kurundikana mijini.

Amesema mpaka Julai, mwaka huu, kuna mawakili wa kujitegemea 6,750 nchini lakini kuna wakili mmoja pekee kwa Mkoa wa Lindi, mawakili wanane kwa Mkoa wa Katavi, 20 (Ruvuma), 29 (Kigoma) na 38 (Mara).

Akitoa mhadhara kwa wanafunzi wa Shule ya Sheria jana jijini Dar es Salaam, Jaji Chande alisema mawakili wanatakiwa kwenda kufanya kazi vijijini na kama maofisa wa mahakama wakasaidie katika utoaji haki.

Alisema kwa makadirio ya Tanzania yenye watu milioni 58 mpaka sasa, wakili mmoja anahudumia watu 82,857 wakati Afrika Kusini wakili mmoja anahudumia watu 2,500. Jaji Chande alisema asilimia 70 ya kesi zipo Mahakama ya Mwanzo lakini wananchi wanajiwakilisha wenyewe kwani hakuna mawakili.

“Tunao mawakili wengi lakini asilimia kubwa wapo mijini kuliko vijijini, hivyo ni jukumu lenu ninyi wanasheria vijana kuhakikisha mnawafikia wananchi waliopo vijijini ili kuwasaidia katika masuala yao ya kisheria na kusaidia mahakama katika utoaji haki,”alieleza. Alisema mikoa saba ya Tanzania Bara haina mahakama kuu ikiwemo Lindi, Katavi, Morogoro, Simiyu, Manyara, Pwani, Singida and Songwe na wilaya 28 hazina mahakama za wilaya kama vile Mkinga.

“Kutokuwepo kwa mahakama ni kikwazo kikubwa katika utoaji wa haki na masuala ya sheria hususani kwa mawakili wachanga. Hivyo, tutaendelea kuishauri serikali kuharakisha ujenzi wa miundombinu ya mahakama ili watu waweze kupata haki zao,” alisema.

Kwa mujibu wa Jaji Chande, mwaka jana mahakama kuu zimepokea kesi 37,471 na mahakama za hakimu mkazi na za wilaya zimepokea kesi 51,161.

Alifafanua kuwa katika ripoti ya dunia ya mwaka huu kuhusu utoaji haki inaonesha watu milioni 230 wanaoishi katika mazingira mbalimbali wanakosa haki, huku watu bilioni 1.5 wanashindwa kutatua matatizo yanayowakabili yanayohusu haki na watu bilioni 4.5 wametengwa na fursa zitolewazo na sheria.

Pia inaonesha kutokuwepo kwa usawa au ufikishaji sawa wa haki kwa wote na ukosefu mkubwa wa uwakilishi wa kisheria.

Jaji Chande alisema katika miaka mitano iliyopita zaidi ya asilimia 50 ya mawakili wamepokelewa nchini kufanya kazi, hivyo anaamini wataendelea kubadilisha muundo na taasisi ya sheria.

Hata hivyo, aliwataka mawakili hao kuhakikisha kuwa wanafuata maadili yao kwa kuwa wakweli na kuepuka vitendo vya rushwa.

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi