loader
Picha

Spika azindua harambee ujenzi wodi mama na mtoto

SPIKA wa Bunge la Tanzania Job Ndugai amezindua harambee ya kuchangia ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya cha St. Lukes kilichopo wilayani Mpwapwa na kutoa wito kwa taasisi na wadau kujitokeza kusaidia ujenzi huo.

Akizungumza mara baada ya kuongoza maandamano yaliyofanyika jijini Dodoma ya kuchangia ujenzi wa wodi ya kisasa ya mama na mtoto, Ndugai alisema Kanisa la Anglikana ni miongoni mwa taasisi ambazo zimekuwa zikichangia katika kutoa huduma ya afya kwa wananchi, hivyo ni vyema taasisi, wadau kujitoa kwa hali na mali katika kufanikisha ujenzi huo.

Alisema kukamilika kwa hospitali ya rufaa kutasaidia wananchi kupata huduma za afya za kibingwa ikiwamo ugonjwa kansa ambao matibabu yake ni ghali na tiba zake hutolewa na hospitali chache.

Mganga Mkuu Kituo cha Afya cha St. Lukes, Dk Edwin Kiula alisema kituo hicho kina idara tano ikiwemo idara ya uzazi salama na mtoto, ambazo hutolewa bila malipo kama inavyoelekezwa kwenye mwongozo uliotolewa na serikali.

Alisema takwimu za miaka mitatu za kituo hicho, zinaonesha wagonjwa wa nje waliotibiwa katika kituo hicho ni takribani 8,000 kwa mwaka, huku waliofika kwenye kliniki ya mama na mtoto ni wastani wa 18,000 kwa mwaka.

Dk Kiula alisema akinamama waliojifungulia katika kituo hicho ni 400, waliofanyiwa upasuaji mkubwa ambao ni wadharura ni 250 na waliolazwa kwa mwaka ni watu 500.

“Kituo kina uhitaji mkubwa wa ongezeko ili kufikia mahitaji yaliyopo sasa, azima yetu ni kufanya upanuzi wa kituo cha afya kwa kujenga wodi yenye vitanda 40, lengo ni kufikia vitanda 60 kutoka vitanda 20 vilivyopo sasa ili kufikia mahitaji ya sasa,”alisema.

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa, Jacob Chimeledya alisema kanisa limekuwa likitoa huduma ya afya kwa wananchi ikiwa ni kufuata nyanyo za Yesu Kristo ambaye alifanya kazi tatu za kuhubiri, kufundisha na kuponya watu.

Uzinduzi huu wa Dodoma sasa utafuatiwa na harambee kubwa itakayoongozwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete itafanyika Jijini Dar es Salaam katika tarehe itayotangazwa hapo baadaye.

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi