loader
Picha

TANCOAL kulipa bil 23/- za mrabaha

TUME ya Madini Tanzania imeitaka Kampuni ya Kuzalisha Makaa ya Mawe (TANCOAL) kulipa serikalini Dola za Marekani 10,408,798 sawa na Sh bilioni 23.9, ambazo ni mrabaha wa mauzo na usafirishaji wa makaa ya mawe na adhabu ya asilimia 50.

Akisoma taarifa kwa vyombo vya habari jijini Dodoma, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Prof Shukrani Manya amesema Tancoal inatakiwa kulipa fedha hizo za mrabaha, ambazo ni adhabu ya Septemba 2011 hadi Juni mwaka huu.

“Upembuzi na uchambuzi wa takwimu za mauzo na usafirishaji makaa ya mawe umebaini Tancoal inatakiwa kulipa dola 1,103, 594 sawa na Sh bilioni 2.53 ikijumuisha adhabu ya asilimia 50 kipindi cha Septemba 2011 hadi Juni 2014.

“Tancoal pia inapaswa kulipa dola 9,305,205 sawa na Sh bilioni 21.40 ikijumuisha na adhabu ya asilimia 50 kwa kipindi cha Julai 2014 hadi Juni 2019. Jumla ya malipo ya Septemba 2011 hadi Juni mwaka huu ni dola 10,408,798,” alisema.

Alisema tume hiyo pia inaitaka Tancoal kuacha kupotosha umma kwa taarifa za uongo, lakini pia kulipa madeni kwa mujibu wa sheria ya madini.

Prof Manya alisema kutokana na Tancoal kulalamikia madai ya mrabaha, inayotakiwa kulipa serikalini, iliundwa timu kuhakiki deni la mrabaha, unaojumlisha usafirishaji wa makaa ya mawe kati ya Septemba 2011 hadi Juni 2014.

Alisema upembuzi wa madai hayo, ulikuja baada ya Tancoal kusambaza taarifa za upotoshaji kwa tovuti www.miningreview.com Septemba 3 mwaka huu na mitandao mingine ya kijamii.

Prof Manya alisema taarifa hizo za upotoshaji, zilidai kuwa Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini, imeanza kuitoza Tancoal tozo ya mrabaha kwenye gharama ya usafirishaji wa makaa ya mawe kutoka mgodini hadi kwa mtumiaji wa mwisho wa ndani na nje ya nchi.

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof Idris Kikula alisema tume hiyo imekuwa ikitoa bei elekezi ya kuuza madini kila mwezi. Hivyo, alitoa angalizo Tancoal kutoongeza bei ya makaa ya mawe, kutokana na kutakiwa kulipa fedha hizo.

Alisema kama wataongeza, Tume itaichukulia hatua kali na za kisheria. “Tume inaweka bei elekezi ya madini yote na hiyo tunaitoa kila mwezi. Wasije wakachukua sababu hiyo wakaongeza bei ya makaa ya mawe, hiyo hairuhusiwi,” alisema Prof Kikula.

ILI kukabiliana na ugonjwa wa Covid- 19 unaosababishwa na virusi ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi