loader
Picha

Unavyoweza kumtambua anayetaka kujiua

Hivi karibuni katika maadhimisho ya siku ya kupinga na kuzuia kujiua, msemaji wa jeshi la polisi nchini, David Misime alinukuliwa akisema kuwa, taarifa zilizopo zinaonesha Watanzania 666 wamejiua kati ya mwaka 2016 na 2019.

Kimsingi, kujiua ni tendo la kujisababishia kifo kwa kukusudia. Kwa mujibu wa Shirika la Afya la Duniani (WHO), karibu watu 800,000 hujiua kila mwaka sawa na wastani wa mtu mmoja kila baada ya sekunde 40.

“Hili ni janga kubwa sana, na bahati mbaya ndio chanzo cha pili cha vifo kinachoongoza miongoni mwa vijana walio na umri wa kati ya miaka 15 hadi 29,” anasema Mtaalamu wa Saikolojia katika Kituo cha Afya cha Somedics Polyclinic cha Upanga jijini Dar es Salaam, Saldin Kimangale.

NJIA WALIZOTUMIA KUFANYA KOSA HILO

Msemaji huyo wa polisi anasema kati ya watu hao, 219 walijiua kwa kujichoma visu, 367 walijinyonga, 75 walijiua kwa kunywa sumu na watano walijipiga risasi.

Kimangale anasema: “Wengi hujiua kwa kutumia vidonge ili kukatiza uhai wao.”

SABABU ZA WATU KUJIUA

Wataalamu mbalimbali wa mambo ya kijamii wanakitazama kitendo cha kujiua kama tatizo la kiafya.

Wanasema mara nyingi watu wanaojaribu kujiua, kiuhalisia huwa hawataki kufa, bali hutaka kuepukana na matatizo yanayowakabili na kwamba, kama wangeona njia ya kuachana na tatizo hayo, wasingejiua.

Wanazitaja sababu mbalimbali zinazowasukuma watu kufanya kosa hilo kuwa ni pamoja na dosari au kubomoka kwa uhusiano wa kimapenzi, ugomvi wa kifamilia, kukumbwa na matatizo kazini, ugumu wa maisha na hata kujaribu kukwepa aibu kutokana na jambo fulani kama msichana kupata mimba akiwa shuleni.

Misime anasema watu wenye msongo wa mawazo wasaidiwe kuonana na wataalamu wa saikolojia ili wasaidiwe kwa kuepushwa kufikia uamuzi mbaya kama wa kujiua ambao ni kinyume cha sheria za nchi.

Mtaalamu wa Saikolojia katika Kituo cha Afya cha Somedics Polyclinic cha Upanga jijini Dar es Salaam, Saldin Kimangale, anazitaja sababu za mtu kuamua kujiua kuwa ni pamoja na magonjwa ya akili, kukosa mbinu za kukabiliana na changamoto, historia ya kujiua katika familia, mtu kujikataa, maradhi ya muda mrefu na ugomvi ndani ya familia.

Akifafanua anasema bado jamii haijapata elimu ya kutosha juu ya magonjwa ya akili na namna ya kukabiliana nayo.

Anasema asilimia 50 ya wagonjwa wa akili hupatikana na dalili kabla ya kufika miaka 14, sonona, magonjwa ya wasiwasi na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo pombe.

Aidha, anasema pia kuwa sababu nyingine ni kukosa mbinu sahihi na muafaka za kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha ikiwemo ugumu wa maisha, maradhi, uhusiano, misiba na ukatili.

“Sababu nyingine ni kuwepo historia ya kujiua katika familia tabia ambayo hurithiwa, pia mtu kujikataa; unajua ni watu wengi sana wameficha mambo mengi na mazito katika vifua vyao. Mambo hayo yanawatafuna ndani kwa ndani na hawasemi.”

Anasema maradhi hasa yale ya muda mrefu yanayoambatana na maumivu makali kama saratani ni sababu nyingine zinazowafanya watu kufanya uamuzi mbaya wa kujiua.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, wengine hufikia uamuzi huo baada ya familia kukosa mwelekeo.

“Mara kadhaa imeripotiwa mama kuua watoto wake kisha naye kujiua, lengo ni kujiua yeye, lakini anaua na watoto kwa kuwa anawaonea huruma hataki wateseke,” anasema Kimangale.

Anasema watu wanaweza kuwa wanapitia hali zinazofanana, lakini mmoja akaamua kujiua na mwingine akaamua kupambana.

“Binadamu hatufanani, kwa hiyo hata kuvumilia na kutafuta majawabu ya maswali magumu tunatofautiana, na ndiyo maana huwa tunasisitiza kuwa, siyo kila atakayepatwa na sababu miongoni mwa zillizotajwa atajiua, hapana,” anasema.

Anasema mtu ambaye kinga yake ya uvumilivu iko chini ndiye anayeweza kuchukuwa hatua hiyo mbaya na hatari.

KUMTAMBUA ANAYETAKA KUJIUA

Mtaalamu huyo wa saikolojia anazitaja dalili za mtu anayetaka kujiua kuwa ni pamoja na kuwa na mawazo mengi kuhusu kifo na hata kuzungumzia kifo mara kwa mara, huzuni kupita kiasi, kujitenga, kutumia dawa za kulevya na pombe kwa ghafla na mtu kujiona hana thamani.

Anasema: “Dalili nyingine ni mhusika kupata shida ya usingizi, kugawa vitu vyake ikiwemo kulipa madeni, kukosa nguvu ya mwili, kupoteza uwezo wa kufikiri sawasawa na kubadilika hali ya kula.”

Kwa mujibu wa Kimangale, ni vema mtu anayeonesha dalili hizo kuwahishwa kwa wataalamu ili kupata msaada unaostahiki.

YAPASAYO KUFANYIKA

Jamii kujengewa uelewa watu waelewe tatizo kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, mijumuiko mbalimbali izungumzie kadhia hiyo.

“Kuna dhana imejengeka nyuma ya fahamu zetu kuwa halinihusu au haliwezi kunifika yaani huwa tunahisi wao tu ndio wanaweza kupata kwa sababu hawachukui tahadhari,” anasema Kimangale.

Alisema waajiri kazini, katika familia wawe na ufahamu wa kutosha juu ya dalili na viashiria vya mtu anayetaka kujiua ili wachukue haraka hatua stahiki wanapoona dalili hizo mapema.

Aidha, anasema kwa sababu mawazo au fikra au jaribio la kutaka kujiua inaweza kuwa ni dalili ya changamoto nyingine hasa za afya ya akili, basi watu wajengewe tabia ya kuzungumza wanapopata matatizo kuliko kukaa na mambo kichwani.

“Tujifunze kufunguka kila wakati tunapojihisi tofauti tuwashirikishe wapendwa wetu na watu wetu wa karibu. Ukipata huzuni kupita kiasi, mawazo, kukosa utulivu, kukosa hamu ya kula, basi jitahidi mshirikishe mtu wako wa karibu naye haraka achukuwe hatua,” anasema.

Anasema pia kuwa ni vizuri kuweka mbali vifaa vinavyoweza kurahisisha tendo hilo la kujiua hasa dawa, sumu, silaha, kamba na vifaa vingine pamoja na kuwepo na udhibiti wa kutosha kwa maduka ya dawa na maduka mengine vinapopatikana vifaa hivi.

TANGU maambukizi ya virusi vya corona yabishe hodi nchini Machi ...

foto
Mwandishi: Regina Mpogolo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi