loader
Picha

Vikosi ulinzi kupiga kura siku moja kabla

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imesema watu wenye mahitaji maalumu ikiwamo wapiganaji wa vikosi vya ulinzi, watapiga kura siku moja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu mengine ikiwamo ya ulinzi wakati wa uchaguzi huo.

Mkurugenzi wa ZEC, Thabit Idarous, alisema hayo mjini Unguja jana wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari kuhusu uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Alisema marekebisho ya Sheria ya Tume ya Uchaguzi Namba 4 ya mwaka 2018, yanatoa nafasi kwa makundi yatakayoshiriki katika harakati za uchaguzi, kupiga kura siku moja kabla ya uchaguzi wenyewe ili waweze kutekeleza majukumu mengine muhimu wakati wa uchaguzi huo.

Alisema marekebisho hayo yamekuja baada ya kubainika kwamba wapiganaji wa vikosi vya ulinzi, hawaitumii haki yao ya kidemokrasia kupiga kura na kuwachagua viongozi kutokana na kutingwa na majukumu ya kazi siku ya uchaguzi.

“Marekebisho hayo sasa yatawapa nafasi baadhi ya watendaji waliokabidhiwa majukumu muhimu siku ya uchaguzi kupiga kura siku moja kabla ya uchaguzi wenyewe kufanyika,” alisema.

Alisema kwa sasa wapo katika mchakato wa kutunga kanuni, kwa kuwashirikisha wadau ili kuwawezesha watu wa aina hiyo kupiga kura kabla ya uchaguzi. Idarous alisema kazi kubwa inayotarajiwa kufanywa na ZEC ni kuanza maandalizi ya kuandikisha wapiga kura wapya kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao na kufanya uhakiki katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

“Tunakusudia kuanza kuandikisha wapiga kura wapya wenye sifa kwa ajili ya uchaguzi mkuu na kuhakiki Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa ikiwamo waliofariki,” alisema.

Ofisa Mwandamizi wa asasi ya kiraia ya Tacceo inayojishughulisha na mambo ya uchaguzi, Martina Kabisama, aliwataka waandishi wa habari kuzingatia na kufuata maadili wakati wa kuripoti habari za uchaguzi na kutoa elimu kwa jamii kuhusu uchaguzi huo.

Alisema kipindi cha uchaguzi mkuu, jamii inatakiwa kupewa taarifa sahihi ambazo hazitakuwa na muelekeo wa kuhatarisha na kuvunja amani.

Mafunzo hayo yaliyoshirikisha waandishi wa habari 30, yametayarishwa na Tacceo kwa kushirikiana na Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo (Wahamaza) na yana lengo la kuwapiga msasa na kuwakumbusha majukumu yao kuelekea uchaguzi mkuu mwakani.

WANAWAKE wenye matatizo ya Fistula nchini wametakiwa kuacha kujifungia ndani ...

foto
Mwandishi: Na Khatib Suleiman

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi