loader
Picha

Tafakarini wingi wa vifo vya wanawake, watoto-Mahenge

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amewataka watendaji wa sekta ya afya, kujitafakari upya kutokana na kuwepo kwa miundombinu bora ya afya zikiwemo hospitali na vifaa, lakini bado vifo vya wanawake na watoto vipo juu.

Dk Mahenge alitoa kauli hiyo wakati akizindua Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2019/24) wa mkoa huo wa kuboresha huduma za uzazi na mtoto jijini hapo.

Alisema alitegemea vifo vya wajawazito mkoani humo vingepungua, lakini takwimu zinaonesha kwamba mwaka 2014 vilitokea vifo 69, mwaka 2015 vifo 64, mwaka 2016 vilishuka hadi vifo 49, mwaka 2017 vifo 60 na mwaka 2018 vilitokea 67.

“Pia nilitegemea vifo vya watoto wachanga kwa mwaka vingekuwa vikipungua lakini takwimu zinaonesha kwamba mwaka 2014 vilikuwa 715, mwaka 2015 vifo 484, mwaka 2016 vifo 517, mwaka 2017 vifo 555 na mwaka 2018 vilitokea vifo 512,” alisema.

Dk Mahenge alisema inashangaza kuona vifo hivyo mkoani vipo juu, licha ya kuwepo kwa rasilimali zote, yakiwemo majengo, vifaa tiba na wahudumu wa afya.

“Haiwezekani mjamzito amefuata maelekezo ya kwenda kliniki, vifaa vya kutolea huduma vipo, majengo yapo na watendaji wapo, lakini anafariki dunia kwa uzazi pingamizi na matatizo mengine akiwa hospitalini,” alisema.

Alisema wahudumu wa afya wanatakiwa kujitafakari na kusimamia kikamilifu na kuokoa maisha ya wanawake na watoto, kwani hakuna sababu ya kutokea kutokana na uwepo wa nyezo zote za kufanyia kazi.

Alisema vifo hivyo vinaendelea kutokea mkoani humo licha ya Rais John Magufuli kuongeza bajeti ya dawa katika mkoa huo kutoka Sh milioni 900 hadi Sh bilioni nne kwa mwaka.

“Pia Rais Magufuli ametoa fedha takribani shilingi bilioni 10.5 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 21, kwa kila kituo ni kati ya Sh milioni 400 na 500.

Pia mkoa umepata bahati ya kujengwa hospitali tatu za wilaya tatu na hospitali ya taifa ya Uhuru ambazo zinafikia gharama ya takribani shilingi bilioni saba,” alisema.

Alisema vifo hivyo vinaendelea kutokea kutokana na baadhi ya watendaji wa afya kutowajibika vizuri, kama wangesimamia vizuri na wakatoa huduma za afya, basi vifo vingepungua au kuondoka kabisa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Maduka Kessy alisema chimbuko la mpango huo ni Dira ya Taifa 2025, inayolenga kupunguza vifo vya wanawake na watoto nchini.

Alisema mkoa wa Dodoma upo chini kuzidi wastani wa kimataifa wa vifo 70 katika vizazi 100,000, hivyo, kuandaliwa kwa mkakati huo kunatakiwa kuwa jibu la kuondoa changamoto hiyo.

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020 utarejea tena Juni ...

foto
Mwandishi: Na Magnus Mahenge

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi