loader
Picha

Watendaji wapunguzieni kazi Rais, Makamu na Waziri Mkuu

SERIKALI ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, itatimiza miaka minne ya utawala wake hivi karibuni huku nchi ikijivunia hatua mbalimbali za maendeleo.

Mbali na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, serikali hii imejikita kuhakikisha inaboresha maisha ya Watanzania kwenye ngazi mbalimbali. Ili kuhakikisha hilo, viongozi wakuu wa serikali akiwemo Rais Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wamekuwa wakifanya ziara za mara kwa mara kuangalia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Ni dhahiri kuwa kasi ya maendeleo kwa serikali hii, inajionesha wazi kwa kutokuwa na masihara kwa yeyote anayeonekana kurudisha nyuma juhudi za maendeleo hususan kwa wananchi, kukusanya mapato ya serikali na kusimamia taasisi za umma.

Katika miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Magufuli, wapo wakurugenzi, wakuu wa wilaya, mawaziri, wakuu wa mikoa na mameya wanaelewa dhahiri kile ambacho uongozi wa nchi unataka, lakini mara kwa mara wananchi wamekuwa wakishuhudia mambo tofauti na inavyotakiwa.

Ni wazi kuwa watendaji hao wanapochaguliwa, wanatakiwa kusaidia viongozi hao wakuu katika utendaji kazi. Lakini, kwa siku za karibuni badala ya kusaidia, wamekuwa wakwamishaji wakubwa wa juhudi hizo.

Nasema hivyo kutokana na ukweli kuwa wapo baadhi kwenye masuala mbalimbali ya kusimamia na kuhakikisha yanaenda sawa, hawafanyi hivyo, badala yake wanasubiri Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, wawaambie wayasimamie au kukaa hadi wanapofanya ziara na kukuta uozo au changamoto, zinazosababisha wawe wakali kwao ndipo waanze kuyafanyia kazi.

Jambo hilo si sahihi, kutokana na ukweli kuwa viongozi hao wakuu, huwa wameongezewa kazi mara mbili. Kutokana na hilo, haina maana kuwachagua watendaji kusimamia kazi au miradi katika maeneo waliyopewa. Mbali na mengi yaliyoshuhudiwa katika ziara za viongozi hao wakubwa, ni tukio lililotokea wiki hii katika Machinjio ya Vingunguti.

Pamoja na kuchelewa kujengwa kwa machinjio ya kisasa, kumekuwa na uchafu uliokithiri, ambao ni hatari kwa maisha ya wakazi wa Dar es Salaam. Mara baada ya kupita kwa Rais Magufuli katika machinjio hayo, akitokea kwenye uzinduzi wa kiwanda cha mabomba katika maeneo hayo, aliwaagiza viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, kukamilisha ujenzi wa machinjio ya kisasa.

Rais aliagiza ujenzi huo uanze, kwani licha ya serikali kuu kutenga Sh bilioni 12.5 kwa ajili ya ujenzi huo, hakuna kilichofanyika hadi sasa. Alitaka kufikia Desemba mwaka huu, wahakikishe ujenzi huo umekamilika.

Alisema atarudi ili kujiridhisha. Jambo la kushangaza na kuonekana kuwa suala hilo lilikuwa linawezekana, viongozi wa jiji na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) siku moja baadaye, waliamkia katika eneo hilo na kuahidi kukamilisha ndani ya muda ulioagizwa na Rais.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Dk Mulid Banyani, Katibu Tawala wa Mkoa, Abubakari Kunenge, Meya wa Manispaa ya Ilala, Omari Kumbilamoto na viongozi wengine, walikutana katika eneo hilo kujadili hatua muhimu za ujenzi.

Kwa mfano huu ni kuwa viongozi hao, walikuwa na uwezo wa kuanza ujenzi wa machinjio hayo mara baada ya kupewa fedha, bila kusubiri Rais atoe maagizo baada ya kufika kwenye eneo hilo.

Lakini walisubiri aseme. Hali hiyo ni kumuongezea Rais kazi bila sabababu za msingi. Hivyo watendaji hawana budi kujirekebisha na kuwapunguzia kazi viongozi hao wakuu.

Ninaona ni vyema watendaji wasimamie kazi zao ipasavyo na pale viongozi wakuu wanapopita au kutembelea miradi mbalimbali, watumie kuja kwao kama fursa ya kupata utatuzi wa changamoto zinazowakabili; na si kuelekezwa majukumu yao.

WATU wa makundi tofauti wamezungumzia hotuba ya Rais Dk John ...

foto
Mwandishi: NA THEOPISTA NSANZUGWANKO

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi