loader
Picha

Viongozi wa serikali wazingatie maadili

RAIS John Magufuli juzi alitengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, waliokuwa wakigombania miradi.

Alichukua hatua hiyo baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuagiza tume ichunguze tuhuma za kuhusika kwao na uchakachuaji miradi ya maendeleo iliyoko wilayani humo.

Hatua ya Rais Magufuli kutengua uteuzi huo ni mfululizo wa hatua nyingine kama hiyo kwa watendaji wengine wa serikali uliofanyika. Tumesikitishwa na habari hizo za ukiukaji miiko, zinazohusisha viongozi wenye dhamana ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Malinyi.

Tunaungana na Rais Magufuli na Waziri Mkuu, Majaliwa kusisitiza umuhimu wa watendaji wa serikali kuzingatia maadili na miiko ya uongozi. Ni aibu tena aibu kubwa kwa viongozi kama hao, kugombana hadharani kwa sababu yoyote.

Ni aibu zaidi kwa sababu baada ya uteuzi huo, serikali iliwapa semina elekezi ya uongozi. Ndio maana tunasema tunaungana na Rais na Waziri Mkuu kukemea vitendo vya utovu wa nidhamu, vinavyooneshwa na watendaji nchini.

Tunaomba kutenguliwa kwa uteuzi wa viongozi hao wa wilaya ya Malinyi, iwe fundisho pia kwa viongozi wengine wanaotumia nafasi zao ovyo. Wako viongozi na watendaji wengine wa kada tofauti serikalini, wamekuwa na tabia mbaya katika utendaji kazi za serikali na za familia.

Wamekuwa wakigombana hadharani na kuwa mfano mbaya kwa wananchi wanaowaongoza na wengine kufikia kiasi cha kutishiana uchawi. Katika kuwasaidia, viongozi wa mikoa, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, Samia Suluhu na hata Rais mwenyewe wamekuwa wakiwaonya wazi. Hata hivyo, wahenga walisema ‘Sikio la kufa halisikii dawa’.

Pamoja na kuonywa, baadhi yao wameendelea kugombana kwa sababu binafsi. Ni kutokana na kuwa na masikio ya aina hayo, tunampongeza Rais Magufuli kwa kuchukua hatua kali dhidi ya wasiotaka kujirekebisha.

Tunapongeza jitihada zinazochukuliwa pia na Waziri Mkuu, Majaliwa na Makamu wa Rais, Mama Samia kuhakikisha kuwa wana nidhamu.

Ni matarajio yetu kuwa kutenguliwa kwa nafasi za watendaji mbalimbali serikalini, kutasaidia waliobaki kubadilika na kuzingatia maadili. Serikali isiyofuata maadili na miiko ya kazi siku zote haiwezi kuwa na tija katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya maendeleo inayofanya.

Ndio maana tunasema, iko haja kwa Rais na viongozi wengine wakuu nchini, kuendelea kuwaadhibu wote wanaoshindwa kujiheshimu. Viongozi wote kuanzia ngazi ya shina, tawi, mtaa, kijiji, kata, tarafa, wilaya hadi mkoa kote nchini, wajue wanawajibika kusimamia maadili.

WATU wa makundi tofauti wamezungumzia hotuba ya Rais Dk John ...

foto
Mwandishi: TAHARIRI

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi