loader
Picha

Aliyenusurika ajali ya boti aeleza mbinu iliyomuokoa

MMOJA wa abiria aliyenusurika kifo baada ya boti ya Lulimbe waliyokuwa wakisafiria kutoka Kemondo wilayani Bukoba kuelekea Rushonga, Bumbire wilayani Muleba kuwaka moto ghafla, ameeleza jinsi mbinu ya kuvua nguo ilivyomsaidia kuwa mwepesi na kujiokoa kwa kuogelea kwa muda wa nusu saa.

Katika tukio hilo abiria wote 56 waliokuwa ndani ya boti hiyo walinusurika kifo baada ya boti hiyo kuwaka moto, kubadili uelekeo na kusababisha tafrani kubwa kwa abiria waliokuwamo ndani.

Hata hivyo, manusura watatu walikimbizwa katika Hospitali ya Mtakatifu Joseph Kagondo na kupatiwa matibabu, ambapo hali zao zinaendelea vizuri. Akisimulia namna alivyonusurika, Michael Dominick, mkazi wa Isamilo, Mwanza, alisema baada ya boti kuondoka Mwaloni umbali kidogo ghafla ulitokea mlipuko mkubwa eneo la nyuma kwenye injini na kusababisha moto mkubwa.

Alitukio hilo lilisababisha boti igeuze uelekeo kwa sababu ya upepo na kuelekea bandarini ilikotoka, huku abiria wakipiga kelele kuomba msaada na wengine kurukia majini kuogelea ili kujiokoa.

Alisema baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya alijitosa katika maji akiwa na begi lake na kuanza kuogelea kuelekea usawa wa ilipo gati ya Kemondo. “Niliogelea kwa muda wa dakika kama 20 baadaye begi langu likajaa maji na likaanza kunipa uzito. Baadaye nikaamua kuliachia, lakini nikaona nguvu zinaniishia na nikawa kama naanza kukata tamaa.”

“Likanijia wazo kuwa nivue nguo, kwa hiyo nikavua shati nikabaki na vesti (fulana) ya ndani, bado nikaona haitoshi nikavua suruali nikabaki na boksa nikaweza kuogelea hadi gatini na kujiokoa,” alisema Dominick.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi, alisema boti hiyo iliyokuwa imebeba abiria 56 na mizigo yao ilianza safari saa 8:00 mchana kutoka katika Bandari ya Kemondo, Septemba 16, mwaka huu. Alisema muda wa dakika kama 20 baada ya kuanza safari, boti hiyo ilishika moto ghafla na kubadili uelekeo kurudi bandarini ilikotoka na kuzua tafrani.

Kamanda Malimi alisema hata hivyo, abiria waliokuwamo waliokolewa na wananchi waliokuwa nchi kavu na wengine walijiokoa wenyewe kwa kuogelea majini.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, akiwapa pole manusura wa ajali hiyo na kuzungumza na wananchi katika eneo hilo la tukio, aliwasisitiza kuhakikisha wanazingatia usalama wao wakati wa kusafiri kwa kuvaa makoti maalum ya kuokoa uhai (Life Jacket).

Aliitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini (LATRA) kuwa na utaratibu wa kukagua kikamilifu vyombo vya usafiri majini kabla ya kuanza safari.

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020 utarejea tena Juni ...

foto
Mwandishi: Na Diana Deus

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi