loader
Picha

Majaliwa atoa siku 14 visima vya maji viwe tayari

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kuelekeza matumizi ya Sh mil 70 za mapato ya ndani zilizokusanywa katika robo ya mwaka wa fedha, kuchimba visima vya maji safi na salama.

Visima hivyo vitachimbwa katika vijiji vya kata ya Ruaha kutokana na kilio kilichowasilishwa na wananchi na Mbunge wa Mikumi , Joseph Haule mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Kutokana na kilio hicho, Waziri Mkuu alimpa siku 14 hadi Septemba 30, mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauari ya Wilaya ya Kilosa, Asajile Mwambambale awe amekamilisha uchimbaji wa visima hivyo.

Waziri Mkuu alisema baada ya kumalisika kwa siku hizo atamtuma Waziri wa Maji kukagua na kuvifungua visima hivyo kwa matumizi ya wananchi. Alitoa agizo hilo juzi aliposimamishwa kwa muda na wananchi wa eneo la Darajani , kata ya Ruaha , Tarafa ya Mikumi wakati akiwa njiani akienda katika Kata ya Malolo iliyopo wilayani humo.

Wananchi hao waliwasilisha kero zao ikiwemo ya ukosefu wa maji wakiwa wameshikilia ujumbe ulioandikwa katika mabango yanayoonyesha jinsi wanavyoteseka kwa kukosa maji kwa muda mrefu licha ya mto Ruaha kupita katika vijiji vyao.

Akizungumza na wananchi hao, alisema Ruaha ni mji unaoendelea kukua na hivyo viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa walipaswa kufanya utafiti katika kila kijiji ili kubaini maeneo yanayopatikana maji na kuchimba visima.

Alieleza kuwa serikali imeweka mkakati wa kupeleka maji na Rais John Magufuli amesisitiza kutaka kuona maji yanapatikana vijijini kwa kuchimbwa visima vifupi na vya kati. Alisema gharama ya visima hivyo inaanzia Sh milioni 50 hadi 100 na kuelekeza halmashauri za wilaya ndio zichimbe visima hivyo na vile vinavyoanzia Sh milioni 200 vitachimbwa na wizara. “

Mnasema Ruaha hakuna maji wakati maji yanatiririka hapa, mna mapato ya ndani na mmesema mna Sh milioni 70, ingawa mna jukumu la kupanga matumiz , lakini watu hawana maji, ninaangiza fedha hizi zote ziletwe kuchimba visima vya maji hapa Ruaha, “ alisema Waziri Mkuu.

Mbunge wa Mikumi , alisema wananchi wa eneo hilo wana shida ya maji na licha ya kufika kwa Waziri wa Maji na kuwepo kwa mpango wa mradi mkubwa wa maji bado hali ya maji hairidhishi .

Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Kilosa, Joshi Chum alimhakikishia Waziri Mkuu kuwa uchimbaji wa visima vifupi unachukua muda wa siku mbili ama tatu na kwamba wataleta mitambo ya kuchimba visima hivyo .

Katika hatua nyingine , Waziri Mkuu akiwa mjini Ifakara wilayani Kilombero alitembelea kituo cha afya Kibaoni na kupokea taarifa ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara , Dk Happines Ndosi.

Katika taarifa hiyo, Dk Ndosi alieleza mafanikio na changamoto zinazokikabili kituo hicho ikiwemo ukosefu wa gari la wagonjwa, uhaba wa watumishi na wingi wa wagonjwa wanaohudumiwa na kulazwa kwenye kituo hicho.

Waziri Mkuu baada ya kupokea taarifa hiyo alitoa malekezo kwa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kupitia Katibu Mkuu wake kuratibu mgao wa pili wa ujenzi wa hospitali za wilaya na kutoa kipaumbele kwa kuipatia fedha Halmashauri ya Mji wa Ifakara ili kujenga hospitali ya wilaya.

Kuhusu ukosefu wa gari la kubeba wagonjwa katika kituo hicho, Waziri Mkuu alisema atamwagiza Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuleta gari la kubeba wagonjwa katika kituo hicho, ili kuwaondolea mzingo wananchi wa kukodi gari la wagonjwa kutoka hospitali binafsi kwa gharama ya Sh 800,000.

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020 utarejea tena Juni ...

foto
Mwandishi: Na John Nditi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi