loader
Picha

Kiswahili Uganda sasa rasmi, EAC yapongeza

KAMISHENI ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA), imeipongeza Serikali ya Uganda kutokana na kuridhia kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la nchi hiyo litakalokuwa na dhamana ya maendeleo ya lugha hiyo.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni hiyo yenye dhamana ya kukuza na kuendeleza lugha adhimu ya Kiswahili ili kuwaunganisha wananchi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Profesa Keneth Simala alitoa pongezi hizo alipozungumza na HabariLEO Afrika Mashariki.

Alisema hiyo ni hatua nzuri kwa sababu kile ambacho serikali imekifanya ni kile kilichoamuliwa na Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki kuwa, nchi zote za EAC zijitahidi kuendeleza Kiswahili kupitia hatua mbalimbali na miongoni mwa hatua hizo ni kukitumia Kiswahili katika nyanja maalumu na nyanja rasmi.

Juhudi hizo ni pamoja na kuanzisha mabaraza ya Kiswahili kwa nchi zile ambazo hazina mabaraza hayo.

Simala alisema hatua ya Uganda ya kuruhusu kuanzishwa kwa baraza la Kiswahili kumerahisisha kazi kwa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki .

Mbali ya juhudi za Uganda kuamua kukibeba Kiswahili kinachotarajiwa kusambaa hadi shuleni, nchi nyingine za Afrika Mashariki zilizoelekeza nguvu katika Kiswahili ni Tanzania na Kenya ambazo zimeifanya lugha hiyo kuwa ya taifa, pia Rwanda, Burundi na Sudan Kusini zilizoingia Kiswahili katika mitaala yake shuleni.

Simala alisema uundwaji wa baraza hilo utafanya shughuli za maendeleo na ukuaji wa lugha ya Kiswahili nchini Uganda kuratibiwa na chombo ambacho kinatambuliwa rasmi.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Dk Selemani Sewange alisema ruhusa ya kuundwa kwa baraza la Kiswahili nchini Uganda ni juhudi za muda mrefu za wadau wa Kiswahili Afrika Mashariki ikiwemo Bakita.

Alisema kuundwa kwa Baraza la Kiswahili nchini Uganda ni kwa mujibu wa Itifaki iliyoanzisha Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Dk Sewange, itifaki hiyo inasema kila nchi inatakiwa kuwa na baraza la Kiswahili. Wiki iliyopita Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Uganda Ofwono Opondo aliwaambia waandishi wa habari kuwa Baraza la Mawaziri nchini Uganda limeridhia kuundwa kwa baraza la Kiswahili la nchi hiyo, hatua inayoonyesha nia na dhamira ya serikali ya Uganda ya kuenzi lugha ya Kiswahili.

Mpaka sasa nchi ambazo tayari zimeunda mabaraza ya Kiswahili na yanafanya kazi ni Tanzania Bara na Zanzibar. Nchi ambazo bado hazijaunda, lakini zipo katika hatua za mwisho za kuanzisha ni Kenya na Sudan Kusini

NCHI za Tanzania na Kenya zimeafikiana kuwa madereva ...

foto
Mwandishi: Na Selemani Nzaro

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi