loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mbinu za mataifa mbalimbali kulinda maslahi yao-2

Katika toleo lililopita, tuliishia katika kipengele kinachozungumzia matumizi ya nguvu kama moja ya mbinu za watendaji wa nchi mbalimbali katika kutekeleza malengo ya sera ya nje/kigeni (yaani, maslahi ya taifa).

Tuliona taifa moja linaweza kutumia nguvu kuendeleza maslahi yake ndani ya nchi nyingine. Endelea. Matumizi ya nguvu yanajumuisha: aina zote za uvamizi, utendaji wa taifa moja ndani ya eneo la taifa lingine bila ridhaa yake, vitisho vya aina yoyote, kulazimisha na utendaji wa kijeshi.

Kwa maana hiyo, vitendo vifuatavyo vinachukuliwa kama matumizi ya nguvu kuendeleza maslahi yake: uvamizi wa kijeshi; vita vya msituni; maandamano ya kulazimisha; kupanga mapinduzi; kufadhili na kupanga mauaji na hongo/rushwa; kuandaa, kutoa mafunzo ya kijeshi na kuwapatia silaha raia wa nchi kisha kuwarejesha nyumbani kwa lengo la kuiondoa serikali halali.

Mengine ni kutengeneza kashfa za kisiasa katika nchi nyingine; vitisho; kupenyeza asasi za hiari (NGOs) kwenye nchi nyingine na kuzitumia kupinga/kuvuruga serikali; na kufadhili migomo na vurugu/ ghasia nchi za nje.

Pamoja na watu wengi kupinga matumizi ya nguvu kuendeleza maslahi ya nchi, mbinu hiyo itaendelea kuwepo maadamu watawala wengi hawako tayari kukubali au kutafuta njia mbadala.

Aidha, matumizi ya nguvu yataendelea kuwepo kwa sababu ni moja ya mbinu ya muhimu kufikia malengo fulani (maslahi). Hata hivyo, njia hii hutumiwa kama chaguo la mwisho pale njia nyingine zinaposhindwa.

MATUMIZI YA PROPAGANDA

Propaganda inatafsiriwa kama juhudi za makusudi za serikali kuathiri tabia na mienendo ya watu au makundi ya watu (makabila, dini na kiuchumi) ya nchi nyingine kwa matarajio kwamba, watu au makundi hayo nayo yataathiri tabia na mienendo ya serikali yao.

Lengo kubwa la propoganda hizo ni kuilazimisha serikali husika ikubaliane na sera ambazo hazikubaliki nchini mwao. Kwa mfano, fuatilia juhudi zinazofanywa na nchi za Magharibi kuhusiana na masuala ya ushoga, haki za binadamu na aina ya demokrasia wanayoitaka.

Juhudi hizo zinalenga kubadilisha mawazo na mitazamo yetu na kutuaminisha kwamba mambo hayo ni mazuri. Je, ni kweli kwamba masuala hayo yana mchango mkubwa kwenye maendeleo yetu sawa sawa na uzito wa juhudi wanazowekeza? Ukifanya uchunguzi wa kina, utagundua kwamba kuna agenda ya siri inayolenga kutimiza maslahi ya mataifa yao.

Katika Karne ya Ishirini, propaganda imekuwa moja ya mbinu au njia ambayo imetumiwa sana na mataifa mengi hasa ya yaliyoendelea kuendeleza maslahi ya taifa husika. Vyombo vya habari (runinga, radio, mitandao, simu na magazeti) vya nchi zilizoendelea vimetumika kutoa habari za ushawishi wa mlengo wao, uongo, zenye nusu ukweli, na kuchafua mataifa mengine ili kutimiza maslahi yao.

Kutimiza hayo, nchi za Magharibi zimetengeneza mashirika ya habari ya kuwasemea na kuzisema vibaya nchi nyingine. Kwa bahati mbaya, nchi za Kiafrika hazina mashirika ya habari ya kuzisemea na kuwasema wao.

Ili mbinu ya propaganda ifanikiwe kutimiza malengo yake, kwanza, inahitaji maandalizi mazuri au mawakala na wafanyakazi walioandaliwa vizuri kufanya kazi hiyo.

Pili, propaganda ni gharama hivyo inahitaji pesa za kutosha kuanzisha vituo vya habari, maandiko na vipeprushi mbalimbali, matumizi ya vyombo vya habari na uhusiano.

Tatu, kutengeneza mbinu ya kupenya nchi nyingine. Nne, kufadhili maandiko ya bei nafuu na mwisho, kufadhili watu, safari za nje, maonesho ya biashara, utamaduni na teknolojia.

UKOLONI MAMBOLEO

Miradi ya biashara ya utumwa na ukoloni ilitumika kuendeleza maslahi ya mataifa ya Magharibi. Kipindi cha biashara ya utumwa, Waafrika walifungwa minyororo shingoni na mikononi na kutumikishwa, na kipindi cha ukoloni, Waafrika walitumikishwa kwa nguvu kwa maslahi ya wakoloni.

Kipindi hiki cha ukoloni mamboleo, tumefungwa minyororo akilini mwetu na tunatumikishwa kwa hiari kutimiza maslahi yao. Kimsingi, masalia ya fikra za kikoloni ndio utumwa mbaya zaidi.

Kwa vipindi vyote, hivyo tuliaminishwa kwamba, Uzungu ni bora kuliko Uafrika (African inferiority) na kwamba, kila kilichotoka Ulaya ni bora zaidi ya kinachozalishwa Afrika.

Kwa bahati mbaya, tulikubali na sasa tunawatukuza na kuwatumikia tena kwa hiari yetu. Afrika ndilo bara pekee ambalo hadi leo nchi zinajitambulisha kwa mabwana zao - Anglophone, Francophone, Lusophone, Arabophone, na karibuni tutaanza kujitambulisha kwa mabwana wapya, Chinophone! Ajabu na hatari.

Hebu angalia, tuna hospitali zetu lakini hatuziamini tunakwenda kutibiwa kwa mabwana zetu; tuna shule/ vyuo vyetu vizuri tu, lakini tunapeleka vijana wetu kwa waliotutawala ili wakafundishwe kinachodhaniwa kimakosa kuwa ni ustaarabu kama uzuri wa ushoga, licha ya madhara yake, haki za binadamu, demokrasia, kuzungumza lugha zao na kupata majina ya Kizungu.

Mengine yamelenga kupata lafudhi ya Kizungu, kubadilisha rangi ya ngozi na nywele ili eti watu wapendeze. Aidha, tuna timu zetu za michezo na wachezaji wazuri tu, wasanii wazuri, na maandiko mengi ya Kiafrika, lakini tunapendelea na kutukuza vya nje.

Tuna rasilimali nyingi, lakini tunakimbilia kwa mabwana zetu tukafanywe watumwa tena kwa kufanya kazi za aibu ambazo hatuwezi kuzifanya hapa nchini. Tuna uwezo wa kuzalisha chakula na bidhaa nyingi kwa matumizi yetu wenyewe, badala yake tunazalisha na kuuza malighali nje kwa bei nafuu kisha zinatumika kutengenezea bidhaa na kutuuzia kwa bei ghali. Mbaya zaidi, tunazalisha pamba na ngozi za kutosha kisha tunasafirisha nje.

Huko nje, wanatengeneza nguo na viatu, wanavaa wao kwanza, wakizichoka wanatuletea kama misaada. Haiingii akilini nchi tajiri kama Tanzania kuwa taifa la mitumba! Matokeo ya yote hayo, tunatumia tusichozalisha na kuzalisha tusichotumia.

Hatimaye, tunaendeleza uchumi wa nchi nyingine/nje kwa kuwauzia malighafi, kukuza ajira nchini mwao na kuwa soko la bidhaa zao ambazo tuna uwezo wa kuzizalisha nyumbani! Hayo ndiyo madhara ya masalia ya fikra za kikoloni ambayo yanatutafuna hadi leo.

Kwa maana hiyo, ukoloni mamboleo umetufanya kuwa vitendea kazi tu kwa manufaa ya mabwana zetu. Haiwezekani ukasomeshwa, ukatibiwa, ukavishwa mitumba, ukabeba majina yao, ukaongea lugha yao, ukaongea lugha yako kwa lafudhi yao, ukajivika rangi na nywele zao, ukakimbilia kwao na ukawa zana ya kuzalisha malighafi, kisha eti ukawa salama, huru na ukajitegemea.

Rais wa Ghana, Kwame Nkrumah alikuwa sahihi alipowaambia Waafrika: “Basi utafuteni kwanza ufalme wa kisiasa na mengine yatafuata baadaye”. Swali ni kwamba, miaka zaidi ya hamsini baada ya uhuru wa kisiasa, tumefanya nini kuhakikisha tunajitawala kifikra na kiuchumi?

MBINU NYINGINE

Kuunda muungano/ushirika wa nchi mbili au zaidi unaozifanya kuwa na wajibu wa kuendeleza na kulinda maslahi yao kwa pamoja.

Aidha, nchi moja inaweza kutumia mbinu za kisaikolojia na kisiasa ili kudhoofisha nchi nyingine au adui. Lengo la kudhoofisha nchi nyingine au adui ni kuiwezesha kuendeleza maslahi yake kirahisi.

HITIMISHO

Ni dhahiri kwamba, mambo mengi yanayotendeka katika uhusiano wa kimataifa ni mbinu za mataifa ya Magharibi kuendeleza maslahi yao. Wajibu wa nchi kama Tanzania ni kuungana ili kuwa na nguvu za pamoja kukabiliana na mbinu hizo.

Maana yake ni kwamba, kila tutendalo kwenye uhusiano wa kimataifa tujuilize: “Tunanufaikaje?”

Naamka asubuhi,  sioni kilongalonga, 
Napapasa kitandani,  hamadi hiki hapa,  

foto
Mwandishi: Na Prof. Kitojo Wetengere

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi