loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Juhudi binafsi kutuletea medali Doha 2019

MASHINDANO ya 17 ya Dunia ya Riadha yalitarajia kuanza jana Doha, Qatar, huku Tanzania ikiwakilishwa na wanariadha wanne, watatu wa kiume na mmoja wa kike.

Mashindano haya ndio michezo mikubwa zaidi ya riadha inayoshirikisha mchezo mmoja tu ukiondoa ile ya Fifa ya Kombe la Dunia na ile Olimpiki, ambayo hushirikisha michezo mingi.

Wanariadha wa Tanzania wanaoliwakilisha taifa ni mwanamke pekee, Failuna Abdi ambaye alianza kampeni zake jana kwa kushiriki marathon kwa wanawake, huku wengine ni Alphonce Simbu, Augustino Sulle na Stephano Huche, ambao nao watakimbia marathon Oktoba 5.

Timu hiyo ya marathon ya akina baba, itaondoka nchini Oktoba 2 ili kujaribu kukwepa kuathirika na hali ya hewa ya joto kali na unyevunyevu huko Doha, Qatar.

Kocha wa timu hiyo, An drew Panga alisema juzi kuwa, timu hiyo haitaathirika na hali ya hewa ya joto kwa kuwa watakaa hapo kwa siku chache, kabla ya kutimua vumbi katika barabara za Doha Oktoba 5.

Pamoja na maelezo mazuri ya kocha huyo wa riadha, wazo langu ni kwamba wachezaji hao wangeweza kuwahi Doha, bila shaka kungewasaidia kuzoea hali ya hewa ya joto kali au wangepiga kambi jijini Dar es Salaam au Zanzibar, ambako kuna joto kali ili kuzoea hali kama ya Doha.

Lakini tatizo wanariadha wetu walikaa Arusha, ambako kuna baridi kali, ambako walipiga kambi ya kila mtu kivyake ili kujaribu kusaka medali kutoka katika mashindano hayo makubwa kabisa ya mchezo huo.

Hadi sasa ni wanariadha wawili tu wa Tanzania, ambao wamewahi kutwaa medali kutoka katika michuano ya Dunia ya Riadha, ambao ni Christopher Isegwe aliyeleta medali ya fedha mwaka 2005 mashindano hayo yalipofanyikia Helsinki, Finland na Simbu aliyetwaa shaba 2017 jijini London.

Sasa ni wakati wa wanariadha kutuletea medali nyingine kutoka katika mashindano hayo, kwani mbali na kuliletea sifa taifa letu, pia watapata donge nono, ambalo hutolewa na Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) kwa washindi wa medali.

Pamoja na kocha Panga kusema kuwa maandalizi yao yalikuwa na changamoto nyingi kutokana na ukata, lakini aliahidi kuwa vijana wake bado wana nafasi ya kufanya vizuri huko Doha.

Wanariadha na kocha wao wana matumaini makubwa ya kufanya vizuri, lakini kutokana na ukubwa wa mashindano yenyewe nafikiri kuwa tuna nafasi finyu ya kutwaa medali, kwani tunakutana na wanariadha waliojiandaa vizuri zaidi kuliko sisi.

Sawa ninachokiona hapa ni tusubiri tu kudra za Mwenyezi Mungu kupata medali, kwani tunapoenda kushindana nao wamejiandaa vizuri licha ya kupeleka timu kubwa ya watu wengi.

Kilichobaki ni kusubiri na kuona vijana wetu watavuna nini kutoka katika mashindano hayo ya 17 ya dunia ya riadha yanayofanyika Doha, Qatar.

UZURI wa ngozi huanzia ndani. Hivyo unavyoitunza ngozi yako kwa ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi