loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uwezo wa China kubadili jangwa kuwa hifadhi ya misitu

Kwa muda sasa, China imepata mafanikio makubwa katika uhifadhi wa mazingira. Taifa hilo lenye watu wengi zaidi duniani, linaongoza katika harakati za kuongeza maeneo yenye mimea,kutokana na mpango wake kabambe wa upandaji miti na kufanikisha kilimo bora. Takwimu zilizopo zinaonyesha eneo la misitu nchini humo kumeongezeka kutoka asilimia 12.5 miaka ya 1950 hadi asilimia 21.7 mwaka 2017.

Pamoja na mafanikio hayo , mamlaka ya misitu ya China imeapa kuongeza eneo hilo hadi asilimia 26 ifikapo mwaka 2035. Miradi kama ile ya kupambana na jangwa kubwa la Kubuqi, mkoa wa Mongolia ya Ndani, inabaki kuwa mfano katika jitihada za kuhifadhi mazingira nchini China. Hii ni hatua kubwa, kwani kulingana na wataalamu, majangwa husababisha changamoto kubwa katika maendeleo ya uchumi kutokana na kukosekana kwa misitu, hali ya mazingira isiyotabirika, uwezo wa chini wa uzalishaji, pamoja na miundombinu mibovu.

Lakini licha ya hali hiyo, China ilikubali changamoto ya kukabiliana na jangwa hilo, ambalo baadaye limekuwa mfano wa maendeleo katika misitu. Shirika la Mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) limepongeza juhudi za China katika kugeuza mojawapo ya majangwa makubwa zaidi kuwa sehemu ya misitu. Zaidi ya kilomita 6,000 za mraba katika jangwa la Kubuqi tayari limerejeshwa katika hali nzuri. Kubuqi ni jangwa la saba kwa ukubwa nchini China.

Jangwa hilo lipo kilomita 800 kutoka Beijing na lilikuwa chanzo cha dhoruba ya mchanga iliyokuwa ikiupiga mji mkuu wa China, Beijing, kwa muda mrefu. Jangwa la Kubuqi lipo katika mkoa wa Mongolia ya Ndani na lina ukubwa wa kilomita za mraba 20,000 . Kihistoria jangwa la Kubuqi halikuwa limefunikwa kwa mchanga kutoka mwanzo. Kwa mujibu wa kumbukumbu za kihistoria, sehemu hii ya nchi ilikuwa makazi ya watawala katika karne ya nyuma na ilikuwa na ardhi yenye rutuba nyingi.

Katika siku hizo, inasemekana Kubuqi ilikuwa imejaa rangi ya kijani, mji mahiri na wa kusisimua. Hata hivyo karne ya malisho iliyofuata ilisababisha kuharibiwa kwa mimea yote ardhini. Miaka 200 iliyopita, shughuli hizi za malisho ziligeuza sehemu kubwa ya ardhi yenye rutuba, kuwa jangwa na kumaliza vyote vilivyofanya eneo hilo kuwa la kuvutia. Sehemu yote ya ardhi karibu na Kubuqi ilibaki kuwa kame.

Wenyeji walibatiza sehemu hiyo kama “bahari ya mauti” kutokana na hali ngumu sana ya maisha wakati huo. Lakini miaka 30 iliyopita, juhudi za kupigana na jangwa na kulirejesha eneo hilo katika hali yake ya awali zilianza. Kwa uratibu za serikali za mitaa na makampuni, pamoja ushiriki wa wakulima na wafugaji, kwa kuzingatia sayansi na teknolojia, eneo hilo lilianza kurutubishwa Hivyo haikuwa jambo la kushangaza wakati ripoti ya UNEP ilipoonyesha kupungua kwa dhoruba ya mchanga iliyokuwa ikipiga Beijing, kutoka 50 mwaka 1988 hadi moja tu mwaka 2016.

Aidha, jitihada za kuboresha ardhi ya misitu kwa mujibu wa ripoti hiyo pia zilisaidia zaidi ya watu 102,000 katika eneo hilo kujikwamua kutoka kwenye umasikini. Hiyo iliwezekana baada ya Shirika la China la Elion Resources Group, likishirikiana na wenyeji na serikali ya Beijing, kuwa na lengo moja la kuzuia kuenea kwa jangwa na kurejesha mazingira.

Kwa miongo mitatu, kampuni hiyo pamoja na wanasayansi na wenyeji waliungana katika moja ya miradi kabambe zaidi ya kupambana na jangwa katika karne ya 20. Wakiwa wamejihami na teknolojia shirikishi, mashine na kemikali, waliobebeshwa jukumu hili walifanya kazi bila kuchoka katika juhudi za kugeuza jangwa kuwa ardhi ambayo sasa ina uwezo wa kukuza matunda na miti.

Katika mradi huo wa urejesho, wenyeji walipewa motisha kwa kupanda mmea aina ya susi au licorice ambayo haihitaji maji mengi na pia inaweza kuuzwa kwa matumizi ya dawa ya jadi ya Kichina. Mpango huu ulikuwa na mafanikio kwani mmea huo uliendana na hali ya mazingira ya Kubuqi.

Mwaka 2013, kutokana na dhana ya maendeleo ya sekta ya mchanga ya “ nuru zaidi, maji kidogo, teknolojia ya juu, na faida nyingi”, kampuni ya Elion iliinua mpango huu hadi kiwango kingine baada ya kuwekeza mamilioni ya dola na kutumia teknolojia mpya ya germplasm na teknolojia ya upandaji kutokana na uzoefu wake wa zaidi ya miaka 27 ya kurejesha ikolojia kuboresha hali ya Kubuqi. Kwa sasa, eneo hilo lina hekta 3,500 ambayo hasa inatumika katika kukuza nyasi na miti yenye thamani ya juu ya dawa za jadi za Kichina.

Hii iliashiria uzinduzi wa uzalishaji na upandaji wa susi na spishi nyingine kwa njia kubwa. Ili kupima rutuba kwa udongo wa jangwa baada ya mafanikio ya susi, kampuni hiyo ilifanya majaribio ya maendeleo ya kilimo cha kisasa ikilenga kulima matunda na mbogamboga katika eneo hilo la kiikolojia. Mchakato wa uhifadhi uliifanya kampuni hiyo kuanzisha vyumba vya vioo vya kisasa katika eneo la kiikolojia ambavyo vitatumiwa hasa kukuza miche ya susi. Mradi mwingine wa kulea miche ya matunda na mboga pia ulianzishwa.

Tangu wakati huo, theluthi moja ya jangwa imerejeshwa na sehemu ya ardhi yenye mchanga inaendelea kupungua. Elion ni kampuni maarufu katika juhudi za kurejesha ardhi iliyoharibika. Shughuli yake kubwa ni marejesho ya mazingira, na kuzalisha nishati safi.

Kampuni hiyo ilitunukiwa tuzo ya taifa ya kuboresha mazingira kutoka kwa serikali ya China na pia ilitambuliwa kama bingwa wa nchi kavu na mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na kuenea kwa jangwa (UNCCD).Takwimu kutoka serikali za mitaa zinaonyesha kwamba juhudi za kuongeza misitu katika jangwa la Kubuqi zimebadilisha maisha ya wakulima na wafugaji zaidi ya 100,000.

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalum

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi