loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Madaktari wanavyotaka kuhongwa ngono

“WAKATI nikiwa form three (kidato cha tatu), tulikuwa na mwalimu mkali kweli, ukishindwa mtihani wake, unapata adhabu wakati maswali yenyewe ni magumu ya kuua mtu, akawa anawaita wanafunzi wanaofeli mitihani yake mmoja mmoja ofi si kujieleza kwanini wanafanya mchezo mpaka kufeli mitihani.”

“Kumbe ndugu yangu, ikifika zamu yako, ukiingia anaanza kukuuliza akusaidieje na mwisho, anakwambia siku za wikiendi uende nyumbani kwake akufundishe topic (mada) ijayo, lakini cha ajabu, wavulana hawaambiwi hayo.”

Anasema Mary Matiko (si jina halisi), msichana aliyehitimu elimu ya sekondari katika shule moja jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na mwandishi wa makala haya.

Anaongeza: “We acha tu kaka yangu! Siyo siri wakati nikiwa huko shule, si nami nikajilengesha kwa huyo mwalimu, mara kitu hicho; mimba.”

Anasema kutokana na kuogopa kuachishwa masomo, kutimuliwa nyumbani na kunyooshewa vidole na wanafunzi, wanajamii na waumini wenzake, aliamua kutoa mimba katika zahanati moja jijini humo, lakini aliyokutana nayo, ni sawa na kuruka maji na kuangukia kwenye tope.

“Ndugu yangu, nilitamani kuondoka, lakini ndiyo nimeisha ngia kwa ajili ya kutoa hiyo mimba, lakini ‘daktari’ akaanza kunitaka kwanza akisema lazima tusaidiane maana mimba hiyo ikionekana, nitapata matatizo makubwa”.

“Kilichonisaidia, nikumkubalia lakini nikamwambia sipo tayari hapo, labda atafute sehemu na siku nyingine jambo hilo likiisha… Tangu siku hiyo, sikupokea tena simu yake na nikasema makosa hayo sitayarudia,” anasema na kuongeza kuwa, suala hilo hakuwahi kumwambia mtu. Hayo yakamfanya mwandishi wa makala haya kumtafuta Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Uhai (Prolife) Tanzania, Emil Hagamu.

Hagamu anasema rushwa ya ngono ni kosa la kisheria na kimaadili linalopaswa kukomeshwa kwa kuwa linachangia ongezeko la utoaji mimba na mateso ya kisakolojia kwa wanawake maishani.

Mkasa huo wa Mary unaonesha kwamba rushwa ya ngono ni kosa la kisheria linalofanywa hata ndani ya kosa lingine katika sekta mbalimbali ikiwamo sekta ya afya kwa baadhi ya watumishi au wataalamu.

Kushiriki kutoa mimba ni kosa na kudai, kushawishi au kupokea/ kutoa rushwa ikiwamo ya ngono, pia ni kosa. Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoa wa taasisi hiyo wa Kinondoni, Elly Makala, anasema rushwa ya ngono ni tatizo lililopo katika sekta mbalimbali ikiwamo ya elimu katika shule za msingi, sekondari, vyuo na vyuo vikuu.

Anasema licha ya Kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11/ 2007 kutoa adhabu kwa mtu anayetiwahatiani, bado kumekuwa na changamoto katika kuziendesha kesi zinazohusu rushwa hiyo.

Hata hivyo, katika mafunzo kwa wanahabari kutoka mikoa ya Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam yalioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kupitia mradi wa Boresha Habari Zuia Ukatili yaliyoandaliwa kwa ufadhili wa Internews na kufanyika Dar es Salaam hivi karibuni, hilo lilizungumzwa.

Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, Beatrice Mpembo, anasema ni watuhumiwa wachache wanaofikishwa mahakamani na kutiwa hatiani kutokana na kukosekana kwa ushahidi hali inayofanya kesi zao kufutwa au kutofikishwa mahakamani kabisa.

Anataja vikwazo katika vita dhidi ya rushwa ya ngono kuwa ni pamoja na waathirika kutokutoa taarifa kwa wakati, huku wengine wakificha ushahidi, uelewa mdogo wa jamii na tafsiri ya sheria kuhusu rushwa ya ngono.

Mratibu wa Mradi wa Boresha Habari Zuia Ukatili wa Tamwa, unaofadhiliwa na Internews, Florence Majani, anahimiza vyombo vya habari kushirikiana na jamii kukomesha rushwa ya ngono ili kuongeza ufanisi kwa viongozi mbalimbali wakiwamo wa kisiasa, kazini na katika taasisi za elimu.

Mtaalamu wa masuala ya habari na mawasiliano kwa umma, Dk Joyce Bazira, anasema wanahabari wanapaswa kuwa makini namna ya kupokea, kuchunguza na kuripoti habari kuhusu rushwa ya ngono ili kuusaidia umma.

Katika mazungumzo na Mkuu wa Takukuru wa mkoa wa taasisi hiyo wa Temeke, Donasian Kessy, hivi karibuni, anasema:

“Kweli kuna minong’ono ya kuwapo madai ya rushwa ya ngono katika baadhi ya vyama ili wanawake wapate uteuzi katika nafasi mbalimbali au majina yao yapitishwe kugombea nafasi za uchaguzi hasa udiwani na ubunge.”

Elly wa Takukuru yeye anasema moja ya changamoto hizo ni mwamko duni wa watu kutoa taarifa na hata kutoa ushahidi ili wahusika watiwe hatiani.

“Rushwa hii ya ngono imeshika kasi sana katika taasisi za elimu tangu shule za msingi hadi vyuo vikuu, sababu kubwa ni watoto kutojitambua na pia, kuhofu kutoa taarifa au kukataa maana hawajui hatima yao itakuwaje,” anasema Elly.

Anaongeza: “Inabidi watoto wetu wajengwe kujitambua na kuwa jasiri kutoa taarifa na kusimama imara kutoa ushahidi dhidi ya wahusika.”

Anakwenda mbali na kusema hata katika ajira na utumishi sehemu mbalimbali, watu wengi wamekuwa wakifanya au wanawake kutakiwa kufanya unyama huu, lakini hawasemi kwa kuwa baadhi ya wanawake, kwa kutaka upendeleo au kukosa sifa zinazohitajika, hushawishi watoa huduma wenye mamlaka ili wanawake hao watoe rushwa ya ngono wakiamini itawawezesha kupata wanachokitaka kwa wakati wanaoutaka.

“Hapa napo baadhi ya maofisa wasio waadilifu, hutumia changamoto za uhaba wa ajira na udhaifu wa waombaji, kudai rushwa ya ngono kwa waombaji kazi… Hali hii ni hatari kwani inaweza kusababisha mwenye uwezo wa kufanya kazi akaachwa, na akachukuliwa asiyejua wala kuweza kitu,” anasema.

Anaongeza: “Pamoja na wengine kuwa dhaifu kiasi cha kuamua kutoa ngono kama rushwa, bado hukosa hiyo nafasi. Hebu fikiria mtu anavyoumia.”

Katika maeneo ya kazi, rushwa ya ngono ina mianya katika uombaji ajira, uteuzi wa wafanyakazi kuhudhuria mafunzo, masomo au safari za kikazi zinazowavutia wafanyakazi wengi na hata katika uhamisho ukiwamo wa baadhi ya watumishi kama walimu.

Elly anasema: “Wakati mwingine unakuta mtumishi, labda tuseme mwalimu wa kike anapangwa katika maeneo ya vijijini sana anakoona hakupendwi na wengi kutokana na mazingira ya huko yalivyo, na wakati mwingine kabla hata mtumishi huyo hajaombwa rushwa ya ngono, anajipendekeza na kujipeleka mwenyewe ili apate ajira, apandishwe cheo, au apangiwe kituo anachodhani ni kizuri na wengine wanatumia mavazi yenye utata kujaribu kuwarubini mabosi wao…”

Ofisa huyo wa Takukuru Kinondoni anasema hata katika siasa, ugonjwa wa madai ya rushwa ya ngono upo na unatishia kuwaweka wananchi katika hatari ya kupata viongozi wasio na sifa wala uwezo wa uongozi.

“Baadhi ya watu wanatumia mianya kadhaa kuwalaghai wanawake katika uongozi wa kisiasa kwa madai ya watu hao kutumia ushawishi wao kuwafanya wateuliwe katika nafasi maalumu au wateuliwe kugombea pamoja na kuwapigia kampeni ili washinde,” alisema.

Kwa mujibu wa Elly, katika kipindi cha miaka mitano, yameripotiwa malalamiko matano kuhusu rushwa ya ngono kwani mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu kulikuwa na malalamiko mawili, mwaka 2018 moja na mwaka 2017 mawili. Mwaka 2016 na 2017 hapakuwa na malalamiko.

“Katika hizo, kesi moja ya mwaka huu imefikishwa mahakamani,” anasema Elly na kuongeza;

“Jamii inapaswa kushiriki kikamilifu kupiga vita rushwa ya ngono kwa kuwalea na kuwasimamia watoto katika misingi ya maadili na kutoa taarifa wanapokutana na vitendo hivyo.” Hivi karibuni gazeti hili lilimnukuu Profesa wa uchumi (hataki kutajwa) anasema rushwa ya ngono vyuoni hutokea walimu (wahadhiri) wanapotaka kutumia nafasi zao kujinufaisha kwa ngono, huku wanafunzi wa kike nao wakitaka kunufaika kwa kupewa alama za bure katika mitihani.

Kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, baadhi ya walimu hudai rushwa ya ngono kwa wanafunzi wa kike kwa njia ya vitisho vya adhabu na ofa ya maksi (alama) au kuwapa majibu ya maswali katika mitihani.

Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, katika Kamisheni ya Ushirikishaji wa Jamii ya Jeshi la Polisi, Englibert Kiondo anasema mara nyingi walaghai na wapenda rushwa, huona njia rahisi ya kuwanyanyasa wanawake wanaotaka huduma katika maeneo yao ni kudai rushwa ya ngono. Kiondo ambaye pia ni mtaalamu wa saikolojia ya jamii anasema:

“Rushwa hii imesambaa katika idara na sekta mbalimbali na wanawake wengi wanaumizwa, japo hawataki na hawawezi kusema kutokana na mfumo dume katika jamii kuyafanya mambo mengine japo ni mabaya na yapo, lakini yasisemwe. Wanateseka sana kwa msongo wa mawazo na sonona, lakini hawasemi…

” Anaongeza: “Rushwa ya ngono ni tatizo kubwa linalowaumiza sana wanawake wengi hata katika viwanda mbalimbali ambapo kila siku wanawake wanaenda kuomba kazi hivyo, supervisor (wasimamizi) wengine, wanaitumia nafasi hiyo kuwapa nafasi ya kazi kwa sharti la kubadilishana na ngono,” anasaema Kiondo.

Katika kongamano kuhusu rushwa ya ngono wakati wa Tamasha la 14 la Jinsia lililofanyika Mabibo, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Chama cha Wajane Tanzania (Tawia), Rose Sarwatt, anasema baadhi ya viongozi wa kiroho nao wanakengeuka na kudai rushwa ya ngono kwa waamini wanaotafuta misaada na huduma mbalimbali zikiwamo za kiroho na masomo.

Anasimulia namna mwanamke mmoja alivyomwelezea kuhusu mchungaji aliyemsaidia kwa kumhifadhi nyumbani kwake, kisha akamtaka kimapenzi kwa madai kuwa ataendelea kumsaidia kwa hifadhi katika makao yake eneo la kanisani.

“Sasa huyo dada amepata maambukizi ya VVU na anasema hawezi kumwambia mama mchungaji wala Kanisa, lakini tayari mambo yamemharibikia,” anasema Sarwatt.

Hata katika maeneo yenye shida ya usafiri, rushwa ya ngono imekuwa ikiwanyemelea baadhi ya wanawake hasa ambao shughuli zao zinahusu kusafiri mara kwa mara ili kuwafanya wajihakikishie usafiri kila inapohitajika.

Wanafunzi ni sehemu ya waathirika wa tatizo la usafiri na hujikuta wakiangukia mikononi mwa wanaume mafedhuli wanaotoa lifti za magari yakiwamo mabasi (daladala) na bodaboda kuwarubuni mabinti hao.

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi