loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Siri nyuma ya pazia TPA

ILI nchi iweze kujiimarisha vema katika uendeshaji wa bandari, hatua kabambe zinaendelea kuchukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kwa kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na ile ya serikali kupitia TPA kuipa kampuni ya China Merchant Holdings International iliyokuwa ijenge na kuendesha bandari mpya ya Bagamoyo muda mfupi wa kujitafakari ili kukubaliana na masharti ya serikali; ili iruhusiwe kujenga bandari hiyo.

Aidha baada ya danadana za muda mrefu, sasa ujenzi wa mita za kupima msukumo wa mafuta (flow meters) katika bandari ya Dar es Salaam na zile za Bandari za Tanga na Mtwara umefikia asilimia 50 na zitaanza kufanya kazi kuanzia Juni, mwakani.

Mkakati mwingine ni ule wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambayo itakamilika kabla ya kumalizika kwa kipindi cha uongozi wa Rais Magufuli na kuwezesha treni yenye uwezo wa kubeba mizigo sawa na malori makubwa (semi – trailer) 500 kutoka katika bandari ya Dar es Salaam, kuzinduliwa.

Upo pia mkakati wa kubadili mifumo ya kiutendaji ambayo imekuwa inasababisha viongozi mbalimbali wa TPA kuondolewa kazini kwa kudaiwa kutofanya kazi ipasavyo hususani kuwepo kwa takwimu ambazo zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka 15, mamlaka hiyo imeshaongozwa na Wakurugenzi Wakuu saba na Wenyeviti wa Bodi saba, hatua inayoathiri ufanisi.

Hayo yamebaika kutokana na mahojiano maalumu baina ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam juzi.

Bandari ya Bagamoyo Akizungumzia hatma ya zabuni ya ujenzi wa bandari ya Bagamoyo ambayo mwaka 2013, Tanzania ilisaini muundo wa mkataba na kampuni ya China Merchant Holdings International wa ujenzi wa bandari hiyo, Kakoko alisema kampuni hiyo imepewa muda zaidi wa kutafakari masharti ya serikali.Mkataba huo unagharimu Dola za Marekani bilioni 10.

Alisema maeneo ambayo kampuni hiyo sasa inatakiwa kuyaondoa katika mkataba huo endapo inataka kupewa zabuni ya ujenzi wa bandari hiyo ni masharti 11 tata ambayo ilitaka yawe sehemu ya mkataba ambayo yalikataliwa na serikali.

Alitaja baadhi ya masharti hayo kuwa ni pamoja na kampuni hiyo kutaka sheria za ardhi zibadilishwe ili iweze kukodishiwa ardhi kwa miaka 99 mfululilizo bila ya kuwepo na mazungumzo mapya baina yake na serikali, kinyume na sharti la serikali la kutaka kuikodishia kwa miaka 33, na baadaye kuwepo na mazungumzo mapya kuelekea miaka 66 na 99.

Mengine ni kampuni hiyo kutaka kutolipa kodi kwa kipindi chote cha uendeshaji wa bandari hiyo hadi pesa yake irudi, kulipwa fidia kama itapata hasara wakati wa uendeshaji wa bandari hiyo lakini huku ikitaka kutorekebishwa chochote endapo itapata faida na kupunguziwa gharama za umeme na maji. Alisema sharti lingine waliloshinikiza ni lile la kutaka kutofanyika kwa biashara katika Bandari ya Dar es Salaam na badala yake bandari ya Bagamoyo ndio iwe kitovu cha usafirishaji wa shehena majini.

Hatua hiyo ni kinyume na mpango wa serikali ambayo azma yake ni kuifanya bandari hiyo kuhudumia eneo maalum la uwekezaji viwanda Bagamoyo na bandari ya Dar es Salaam kuendelea kuwa bandari baba.

“Kwa hiyo tumewapa muda wajitafakari upya na kama bado watakuwa na mpango wa kujenga na kuendesha bandari hiyo basi waje tukae chini tena tukubaliane upya, wasipokuja kwa muda fulani tutatafuta mwekezaji mwingine anayeweza kuijenga bandari ile.

“Lakini pia lile litabakia kuwa eneo la TPA maana tulishalipa fidia kwa wananchi ili wapishe, kwa hiyo hata asipopatikana mwekezaji ikifika mwaka 2030 bandari ya Dar es Salaam itakuwa imelemewa hata tukijenga maghorofa haitasaidia kitu, hivyo tunaweza kulitumia eneo lile kujenga bandari mbadala,” alisema Kakoko.

Ujenzi wa flow meters Akizungumzia ujenzi wa flow meters, Kakoko alisema unakwenda vizuri baada ya kutumika kwa mbinu ya kutafuta mzabuni muafaka kutokana na awali suala hilo kugubikwa na mazingira ya udanganyifu, rushwa na udalali wa kutisha.

Alisema flow meters hizo zinajengwa na Kampuni ya Endress+Hauser ya Uswisi na Mkataba ulisainiwa Februari mwaka huu, huku ujenzi ukitarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 15.

“Ujenzi unafanyika katika maeneo mawili, kwanza ni kujenga maeneo ya ujenzi kwa maana ya bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na sehemu ya pili ni kuunganishwa vyuma vyenyewe na ujenzi huu unafanyika Uswisi.

“Ipo timu maalum ambayo inakwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa sehemu zote mbili na hadi hivi sasa muda ambao tayari umetumika ni asilimia 40 na kazi iliyofanyika ni asilimia 50,” alisema Kakoko.

JPM kuzindua treni ya SGR Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu huyo wa TPA alizungumzia mkakati wa ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR nchini ambayo itaunganishwa kwenye bandari ya Dar es Salaam kupitia njia za chini ya ardhi ambayo ujenzi wake utaanza mwakani.

Alisema mkakati uliopo ni kuhakikisha kuwa reli hiyo inakamilika kabla Rais Magufuli hajaondoka madarakani na kumuwezesha kuzindua treni ya mizigo ya umeme ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba mizigo sawa na semi-trailer 500 kwa wakati mmoja. Miaka 15, wakurugenzi 7 Akizungumzia hatua ya kupungua kwa ufanisi kunakosababishwa na kuondolewa mara kwa mara kwa wakurugenzi na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPA, Kakoko alikiri kitendo hicho kuathiri kwa njia moja au nyingine utendaji kazi.

“Ni kweli hilo tunalifanyia kazi ili kujaribu kuangalia zaidi mifumo badala ya watu, inawezekana kabisa kuwa mifumo ndiyo inayosababisha watu washindwe kufanya kazi kwa ufanisi.

“Kwa mfano kwa miaka 15, TPA imekuwa chini ya usimamizi wa Mawaziri 6 (Uchukuzi), lakini pia Wakurugenzi saba na Wenyeviti wa Bodi saba, tunajaribu kuangalia hili na hatua zinachukuliwa ili kuwezesha mamlaka kuwa na ufanisi zaidi.

“Sina maana kuwa nataka tukae muda mrefu maana hiyo nayo haina tija, kwa mfano hata mimi nikishakaa miaka kama mitano natakiwa kuondoka ili nisipazoee sana hapa,” alisema Kakoko.

WADAU wa kili- mo cha mwani wa Kata ...

foto
Mwandishi: Oscar Mbuza

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi