loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ufahamu wa falsafa ya Confucius na nafasi yake katika maendeleo ya kasi China

Tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1949, taifa hilo limeendeleza utamaduni uliojikita katika amani na kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kisiasa, ambayo yameinua hadhi ya nchi hiyo duniani.

La kuvutia zaidi ni uwezo wa viongozi wake na raia kuungana pamoja ili kufikia malengo na ndoto zao. Hii imekuwa sifa bainifu ya mafanikio yake kwa miaka mingi.

Mbali na uchumi wake kufuzu kwa upeo wa juu zaidi na kwa muda mfupi katika historia ya dunia, China imepiga hatua kubwa katika kupambana na rushwa. Katika kipindi hiki, China ilijenga jeshi la kisasa na kujenga mfumo wa kisiasa ambao unaihakikishia utulivu nyakati zote.

Aidha, mamilioni ya raia masikini wameweza kuondolewa kwenye hali ya umasikini wakati ambapo China ilitangazwa kuwa taifa la kwanza kufikia malengo mengi ya maendeleo ya milenia mwaka 2015.

Lakini ni nini hasa kimesababisha hali hii ya ukuaji wa haraka nchini China na kulifanya kuwa taifa la kuvutia wengi?

Ili kuelewa historia hii muhimu ya China, tunahitaji kutupia jicho falsafa ya Confucius iliyozaliwa miaka 2500 iliyopita. Akichukuliwa kuwa mwanafalsafa mwenye ushawishi mkubwa katika historia ya China, Confucius na mafundisho yake anaendelea kuweka ushawishi katika jamii ya Kichina. Falsafa ya Confucius inahusu vitendo vya uadilifu na maadili.

Confucius aliyezaliwa mwaka 551 K.K. anachukuliwa kama msomi mkubwa wa Kichina ambaye alikuwa hasa na haja ya kuendeleza utaratibu wa jamii na maelewano. Mawazo yake yanaonekana kama mwongozo wa kimaadili kwa jamii na serikali.

Aliamini kwamba wanadamu wangekuwa na uwiano na dunia kama kila mtu angeelewa nafasi yake katika jamii na kufundishwa tabia sahihi za cheo chake.Vivyo hivyo, aliamini kwamba usalama wa jamii ulitishiwa na watu waliposhindwa kutenda kulingana na majukumu yao yaliyopendekezwa.

Sehemu nyingine muhimu ya mawazo ya Confucius ilikuwa watawala lazima waongoze kwa kutoa mfano mwema. Alisema viongozi lazima wawe wakarimu ili kupata uungwaji mkono wa raia kwa kutawala mioyo na akili zao. Viongozi, kwa mujibu wa Confucius wanapaswa kuwa na tabia ya kujizuia na kukumbatia maadili ya juu.

Methali moja ya Kichina inasema kwamba "bila kujali ukubwa, boriti moja haliwezi kusaidia nyumba kusimama." Hii inasisitiza mwelekeo wa pamoja. Ikilinganishwa na sehemu nyingine za dunia, mfumo wa ujamaa una asili katika jamii zinazozingatia falsafa ya Confucius. Alisema, ili jamii ya China iweze kufanya kazi vizuri, ni muhimu kuweka matakwa ya mtu binafsi chini ya matakwa ya kikundi. Katika falsafa hii, dhana ya kwamba kila mtu mmoja anapofanya kitu huathiri wenzake ina uzito mkubwa.

Confucius anasisitiza umuhimu wa uhusiano wa jamii. Hii imetangamana na mawazo pamoja na malengo ya uongozi wa chama tawala cha Kikomunisti cha China wa kudumisha amani na utulivu wa jamii.

Februari 2005, Rais Hu Jintao wa China  akizundua kampeni ya nchi nzima ya kuendeleza jamii yenye masikilizano zaidi, harakati ambazo zilipata uungwaji mkono wa baadhi ya wasomi wa Kichina na umma.

Maadili mengi ya Confucius yana umuhimu kwa hali ya kisasa ya kisiasa nchini China. Mwanafalsafa huyo alishauri watu kufuata "amri ya dhahabu" ambayo ilikataza yeyote yule kumfanyia mwenzake kile ambacho yeye mwenyewe asingependa kufanyiwa. Alisisitiza mafundisho ya "njia ya kuwa kati kati" ambayo yalisisitiza uwepo wa kiasi na maelewano. Hii inaonekana wazi kwa njia ya viongozi wa China kuridhia  mashauriano juu ya suala lolote.

Mara tu baada ya kuchaguliwa rais mwaka 2012, kiongozi wa China, Xi Jinping alibainisha kwamba 'Confucius', pamoja na falsafa na tamaduni nyingine zilizoenea na kuongezeka nchini China, ni kumbukumbu ya matukio ya mambo ya kiroho, mawazo ya nchi na utamaduni ulioleta mafanikio ya taifa wakati taifa lilipopigania kupata utambulisho wake.

Lakini mojawapo ya masuala muhimu zaidi au labda urithi utokanao na falsafa hii ya Confucius, ni msimamo wake wa elimu na mafunzo ambayo ni ya msingi wa ndoto ya Wachina. Msisitizo wake juu ya elimu uliambatana na msimamo wake kuhusu mfumo wa ueledi. Mitihani ya huduma ya umma ilitoa fursa sawa, ikitoa ajira ya kuheshimiwa kutokana na tathmini ya malengo ya uwezo wa mtu. Hii ilikuwa ni njia ambayo iliiweka China tofauti na Ulaya, India, na Japan.

Katika ulimwengu wa kisasa, elimu na ueledi ni maadili yanayokubalika sana na yamethibitisha manufaa kwa kufaulisha demokrasia ya kisiasa na kiuchumi.

Confucius aliamini maslahi ya watawala na watu yanahusiana kwa karibu na yana manufaa ya pamoja. Alionya wale walio katika uongozi dhidi ya ukatili, ukandamizaji, na kuumiza.

Katika mtazamo wa Confucius, mtu muungwana anaweza kufanya kazi kwa pamoja na wengine bila ya kukubaliana nao. Hii inaonekana katika njia ambayo serikali ya China inashughulikia migogoro na mataifa mengine kama vile vita vya biashara na Marekani.

Katika vita na mbinu za kijeshi, utamaduni wa Confucius unamsifu mfalme ambaye alitegemea nguvu za kimawazo na kumkemea mtawala aliyetegemea nguvu za kimwili. Katika falsafa hii, ni nguvu za kimawazo tu na wala sio nguvu za kimwili zilizowafanya watu kuheshimu mamlaka.

 

Ingawa kuibuka kwa jeshi la China kumezua hofu katika maeneo kadhaa, serikali ya China daima imemhakikishia kila mmoja kupitia mawazo ya amani ya Confucius kwamba China haitamani kutumia nguvu ila itafuatilia maazimio ya amani.

 

Kutokana na mifano hii, ni dhahiri kwamba licha ya mabadiliko ya kitaasisi na kiuchumi katika China ya kisasa, maadili ya Confucius yatokanayo na historia ya muda mrefu ya China kama jamii yenye utamaduni wa kipekee, yataendelea kuweka ushawishi miongoni mwa idadi kubwa ya Wachina.

Katika hili, utambulisho wa taifa na fahari ya kiutamaduni vina umuhimu mkubwa. Kwa kuwa China imekuwa nchi thabiti zaidi, yenye mafanikio, na ya kujitegemea, Wachina wengi wanakuwa na faraja na fahari na utamaduni wa Confucius kama sehemu ya kudhihirisha maadili ya Kichina, mila na desturi.

Lakini ushawishi wa Confucius haujaonekana katika China pekee na watu wake, bali pia sehemu nyingine barani Asia kama vile Singapore, Korea, Japan, na Vietnam, kwa njia tofauti. Matokeo yake, imekuwa ni njia ya kusambaa  kwa maadili ya Confucius katika China na kwingineko. Kuna uwezekano kwamba hali hii haitabadilika.

Zaidi ya taasisi za Confucius 80 sasa zimejengwa maeneo mbalimbali duniani wakati ambapo falsafa hii inaendelea kupata wafuasi wengi.

 

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: MWANDISHI MAALUM

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi