loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tofauti ya diplomasia na sera ya nje

Japokuwa si rahisi kutofautisha diplomasia na sera ya nje, ni vema kufahamu diplomasia inaishia wapi na sera ya nje inaanzia wapi. Wakati sera ya nje ndiyo msingi wa uhusiano wa kimataifa, diplomasia ni mchakato au mfumo ambao sera ya nje inatekelezwa.

Diplomasia inaandaa mfumo na wataalamu au wafanyakazi kwa ajili ya utekelezaji wa sera ya nje.

Wakati sera ya nje ni chombo cha kutengeneza sheria, diplomasia ni chombo cha utekelezaji wa sheria hiyo. Nchi inapoimarisha uhusiano wake na nyingine, inafanikisha malengo yake na kuendeleza maslahi yake kupitia diplomasia.

Diplomasia ni moja ya mbinu bora za kukuza au kuboresha nafasi, uwezo, fahari na hadhi au sura ya nchi duniani. Sera ya nje na diplomasia zinategemeana, zinahusiana na zinafanya kazi kwa kushirikiana.

Zote zinajihusisha na kurekebisha au kupatanisha maslahi ya taifa na maslahi ya kimataifa ili kuzuia vita kwa kutumia akili, upatanishi na kubadilishana maslahi.

Diplomasia inaposhindwa vita hutokea, na vita inapotokea diplomasia inachukua sura mpya. Wakati wa vita, kazi kubwa ya diplomasia huwa ni kutafuta marafiki wa kuwaunga mkono na kupata misaada ya kivita.

Malengo ya diplomasia Kwa kawaida kila mbinu/ mkakati huwa na malengo. Vivyo hivyo, diplomasia ina malengo inayotaka kuyapata. Kwanza, diplomasia inalenga kuanzisha na kuendeleza urafiki, ushirikiano na uhusiano yenye tija kati ya mataifa.

Diplomasia inaepusha ugomvi, migogoro, na misuguano na mataifa mengine. Mwanaplomasia ambaye ndiye mtekelezaji wa diplomasia ana uwezo wa kubadilisha viashiria vya uvunjifu wa amani kuwa urafiki na ushirikiano.

Hivyo, lengo la mwanadiplomasia ni kujenga urafiki na wote na kuepuka uadui na yeyote. Kwa maneno mengine, diplomasia siyo chochote zaidi ya kupanga, kusimamia na kurekebisha uhusiano miongoni mwa mataifa. Ni wajibu wa diplomasia kuhakikisha nchi inajipatia marafiki wengi duniani kwa kadri inavyowezekana ili hatimaye inufaike na uhusiano huo.

Diplomasia inapotekelezwa vizuri, hutoa taswira ya nchi kwamba, watu wake wapo tayari kujenga urafiki na nchi nyingine. Hata pale kutoelewana au vita kati ya nchi na nchi vinapotokea, diplomasia ni njia sahihi ya kurejesha uhusiano.

Pili, kutatua migogoro au magombano ya kimataifa kwa njia na mbinu za amani. Diplomasia ni moja ya njia au mbinu ya kutatua migogoro duniani. Inaaminika kuwa njia bora zaidi ya kusimamia na kutunza amani duniani. Uwepo wa amani duniani ni kigezo cha muhimu kwa nchi kuendeleza maslahi yake.

Kusipokuwa na amani itakuwa vigumu kufanya biashara, uwekezaji na utalii. Diplomasia inatumia mbinu kama: mazungumzo yanayolenga kuleta uelewano, upatanishi, usuluhishi, ushawishi na ushirikiano.

Tatu, kulinda maslahi ya nchi. Diplomasia ni chombo cha kukuza/kuendeleza, kulinda na kuhifadhi maslahi ya nchi.

Lengo la diplomasia ni kulinda eneo la nchi, kulinda na kuendeleza uhuru wa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Maslahi hayo yanalindwa dhidi ya uwezekano wa vitisho vyovyote.

Kwa maana hiyo, diplomasia ni chombo cha kulinda na kuendeleza maslahi ya nchi. Nne, kumdhoofisha na kumgawa adui.

Kwa kutumia mbinu za kidiplomasia, nchi husika inahakikisha kwamba nchi adui haitishi sana, haiwi na nguvu/uwezo sana, haiwi na ushawishi mkubwa, na haiwi ya muhimu sana kulinganisha na nchi husika.

Aidha, diplomasia inatumika kuhakikisha kwamba kambi ya adui haiwi na nguvu sana, inahakikisha maadui wanagawanyika ili wasiweze kujiunga na kambi nyingine yoyote na kuhakikisha adui anakosa ushawishi na uwezo wa kuboresha taswira au sura ya nchi yake.

Kwa mfano, katika vita vya Bangladesh, India ilishiriki kuigawanya Pakstani kuwa nchi mbili, Pakistan ya Mashariki (Bangladesh ya leo) na Pakistan ya Magharibi (Pakstan ya leo). Wakati huo huo, kwa kutumia mbinu za kidiplomasia, India ilijenga uhusiano wa kirafiki na Bangladesh na uadui na Pakistan.

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Prof. Kitojo Wetengere

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi