loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mabibo yana faida kuliko korosho

“MABIBO huwa hayana thamani kubwa hapa kwetu kama korosho. Labda thamani yake kubwa ni kwa wanaotengeneza pombe ya gongo au uraka na hii gongo kama unavyijua ni haramu,” anasema Mohamedi Ching’umba, mkulima wa korosho kutoka kata ya Kitama, wilayani Tandahimba, Mtwara.

Anaongeza: “Kimsingi, mabibo huwa tunakula, hususani watoto na yanayobaki tunatupa maana hatuna kazi nayo. Hata yanayotumika kutengenezea pombe ni machache tu.”

Akijibu swali kuhusu faida ya mabibo anayoifahamu, mkulima mwingine wa korosho wilayani humo, Halima Saidi, anasema kwamba kwa kawaida mkulima anachoangalia kimpe faida ni korosho ghafi na wala siyo bibo.

“Hapo awali, faida ya mabibo hapa kwetu labda ilikuwa ni kutengenezea pombe ya uraka na gongo. Kinachofanya mtu ashughulikie shamba la korosho kwa maana ya kutegemea faida ni kutoka kwenye korosho wakati wa msimu unapofika na siyo kutengeneza gongo ambayo hata uuzaji wake ni wa kujificha ficha,” amesema Halima.

FAIDA ZA MABIBO

Wakati wakulima wakiona mabibo kama kitu kisicho na thamani, utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kilimo (TARI), kituo cha Naliendele unaonyesha kuwa mabibo yanaweza kumpa mkulima faida kubwa kuliko korosho.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ya Tari, kituo cha Naliendele, Dk Fortunatus Kapinga, anafafanua kwamba tunda la bibo lina faida nyingi moja wapo ikiwa ni kutoa mvinyo ambao mtu anauza bila kujificha kwa sababu ni kinywaji halali tofauti na gongo.

Pili anasema kwa kutumia mabibo, wasindikaji wanaweza kutengeneza juisi au jamu lakini pia mabaki yake yanatumika kama chakula cha mifugo.

Ni katika muktadha huo, Dk Kapinga anasema endapo watatokea wawekezaji wa kuliongezea bibo thamani kwa kuzalisha bidhaa hizo; mvinyo, juisi jamu na chakula cha mifugo. wakulima wa korosho watunaufaika maradufu.

“Mbali na manufaa kwa mkulima mmoja mmoja, pato la taifa litaongezeka sambamba na utoaji wa ajira kwa Watanzania,” anasema na kuongeza kwamba nchi inapojielekeza katika uchumi wa viwanda, ni vyema wenye mitaji wakachangamkia uwekezaji katika eneo hilo.

Dk Kapinga anasema kama korosho na bibo hufanya asilimia 100, basi asilimia 10 ya korosho ndio humpa faidia mkulima kwa kupimwa ikiwa ghafi huku asilimia 90 ambayo ni bibo ikitupwa.

Anafafanua kwamba tunda la bibo likikamuliwa, katika kila kilo tisa hupatikana lita 6.3 za juisi na kwamba kila lita moja inauzwa wastani wa shilingi 4,500 na hivyo mkulima atapata zaidi ya shilingi 28,000 kwa hizo lita 6.3.

Kwa upande wa mvinyo utokanao na mabibo, Dk Kapinga anasema katika kila kilo moja ya mabibo, kwa mujibu wa utafiti, huweza kutoa wastani wa lita moja ya mvinyo ambayo huuzwa shilingi 11,300 na hivyo kilo tisa za mabibo kuzalisha faida ghafi inayofikia Sh 101,700.

“Kwa hiyo unaweza kuona thamani ya mabibo ni kubwa ikilinganishwa na korosho na hivyo uwekezaji huo utakapofanyika korosho itakuwa na manufaa makubwa sana,” anasema.

Anasema kimahesabu faida iliyopo kwenye mabibo ni mara saba ya faida ya korosho ghafi ambayo katika soko la sasa kilo inauzwa shilingi elfu 3,300.

Kapinga anasema baada ya kufanya utafiti, elimu hiyo wameanza kuifikisha kwa wakulima wa korosho kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo makongamano, mikutano, majarida na vyombo vya habari.

Anasema kituo chao pia kiko katika utaratibu wa kuanzisha kiwanda kwa ajili ya kuzalisha bidhaa zitokanazo na mabibo.

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Sijawa Omary

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi