loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM ataka haki kwenye uchaguzi

RAIS John Magufuli ameshuhudia na kuzindua uandikishaji wa wananchi katika daftari la kupigia kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa, huku akiwataka wasimamizi wa uchaguzi huo kutenda haki kwa Watanzania wote bila kujali itikadi ya vyama vyao vya siasa.

Rais magufuli alishuhudia na kuzindua uandikishaji huo mjini Namanyere wilayani Nkasi mkoani Rukwa jana wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo, ikiwa ni siku ya kwanza ya uandikishaji huo utakaokamilika baada ya siku saba Oktoba 14, mwaka huu.

“Nimefurahi kushuhudia zoezi hili muhimu la demokrasia ambapo watanzania kwa mara nyingine wanashiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa,” alisema Rais Magufuli.

Pamoja na kuwapongeza wasimamizi wa uchaguzi huo chini kote, aliwataka wahakikishe wanatenda haki kwa watanzania wote, bila kujali itikadi zao ili wapate uhuru wa kuchagua viongozi wanaowataka.

Aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi, kujiandikisha kwenye daftari hilo la kupigia kura katika serikali za mitaa ili kutumia haki yao vyema na kuchagua viongozi bora.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alimshukuru Rais Magufuli kwa kuzindua uandikishaji huo.

Alimhakikishia rais kuwa uchaguzi huo, utakaofanyika nchini kwa mara ya sita sasa, utakuwa ni uchaguzi unaofanyika ukiwa na maandalizi makubwa katika kila hatua.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola aliwataka wananchi kuwa makini na kuchagua viongozi bora, kwa kuwa viongozi wa serikali za mitaa wapo wa halmashauri ya kijiji ambao ndani yake wana kamati ya ulinzi na usalama.

“Nawaomba Watanzania tumekuwa na tabia ya kuchagua kwa mihemko matokeo yake tunachagua kwa kuchanganya mahindi, maharage, maji na mchele, tunachanganya betri na magunzi matokeo yake tochi haiwaki,” alisema.

Mkoani Dar es Salaam, wananchi wamejitokeza kwa kiwango kidogo, kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura katika uchaguzi huo wa serikali za mitaa kutokana na mvua kubwa inayonyesha.

Katika kituo cha ofisi ya Mtendaji Kata Upanga Mashariki wilayani Ilala, Ofisa Mtendaji wake ambaye ni msimamizi msaidizi, Nashon Marwa alisema mwamko wa uandikishaji upo na watu wameonesha kuhamasika ukiacha changamoto ya mvua iliyoonekana kuzuia baadhi ya watu kujitokeza.

Kuhusu idadi ya waliojitokeza kujiakindisha alisema kwa sasa bado ni mapema kuweka wazi idadi ya watu wa waliojiandikisha, kwani bado hawajakusanya taarifa rasmi kutoka kwenye vituo vingine vya kata yake na ni lazima taratibu zifuatwe katika ukusanyaji na utoaji wa taarifa.

Akizungumzia changamoto zilizojitokeza alisema hakukuwa na changamoto kubwa za kuzuia kazi isiendelee zaidi ya mvua ambayo imesababisha idadi ya watu waliojitokeza kuwa ndogo.

Pia katika Kituo cha Mtaa wa Kitonga, hali ilionekana kuwa tulivu huku mmoja mmoja wakiwasili kujiandikisha. Katika kata ya Kitunda Relini, mwamko ulionekana kuwa mkubwa na watu wakiwa wamejitokeza mapema asubuhi kabla mvua kuanza kunyesha.

Wasimamizi walikuwa eneo la kujiandikisha tayari kwa kazi ya uandikishaji na hakukuonekana changamoto yoyote.

Kwa upande wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Mkoa wake Mrisho Gambo amezindua uandikishaji wapigakura na kuwataka wakuu wa wilaya zote katika mkoa huo, kuhakikisha wanahamasisha wananchi kujiandikisha.

Akizindua zoezi hilo katika kata yake ya Muriet jijini Arusha, baada ya kujiandikisha katika kituo cha Shule ya Msingi Kisimani, alisema zoezi hilo, ambalo limekosa mwitikio wa wananchi, wakuu hao wa wilaya wanapaswa kufanya mikutano ya hadhara ili kuhamasisha wananchi bila kubagua vyama vya siasa waweze kujitokeza kujiandikisha.

Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega alisema kuwa mkoa wa Arusha, unatarajia kuandikisha wapiga kura wa serikali za mtaa wapatao 1,099,289 kutoka katika wilaya zote za mkoa huo, huku jiji la Arusha wakitarajia kuandikisha wapigakura 328,000.

Alisema Mkoa wa Arusha una vijiji 390 , vitongoji 1,505 na mitaa 154 katika jiji la Arusha , ambapo katika Halmashauri ya Arusha kuna wapigakura 200,002, Karatu (144,000), Meru (100,000), Monduli (110,000), Longido (63,252) na Ngorongoro (148,815).

Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi katika jiji la Arusha, Msena Binna alisema wanatarajia kuandikisha wapigakura wapatao 328,605 katika vituo 154 katika jiji la Arusha, huku katika kata ya Muriet wakitarajia kuandikisha wapiga jura 17,300.

Msimamizi Msaidizi katika kituo cha cha uandikishaji cha shule ya msingi Kisimani kata ya Muriet, Amani Ngatuli alisema kuwa zoezi hilo limekuwa na mwamko mdogo kutokana na idadi ndogo ya watu kujitokeza. Alisema jana wameandikisha wapiga kura 48, hivyo ameomba hamasa iendelee kutolewa.

Zoezi hilo la kujindikishaji linatarajia kufikia ukomo Oktoba 14 mwaka. Kampeni zinatarajia kuanza Oktoba 22 mwaka huu na uchaguzi utafanyika Novemba 14 mwaka huu.

Kutoka Dodoma, watu wamejitokeza kiasi huku gazeti hili likibaini baadhi ya vituo vikiwa na mwangalizi mmoja kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) pekee, huku vituo vingine vikiwa na waangalizi kutoka vyama vya CCM na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Akizungumza katika kituo cha mtaa wa Uhuru, mwakilishi wa Chadema, Msafiri Abdallah alisema mpaka sasa uandikishaji unaenda vizuri. Mwangalizi wa CCM, Abdallah Anassy alisema hakuna changamoto iliyojitokeza mpaka sasa katika mwanzo wa uwandikishaji.

Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi na ambaye Mtendaji wa Mtaa ya Uhuru, Subira Zakayo alisema wamehamasisha vya kutosha ili watu wajiandikishe. Imeandikwa na John Mhala, Arusha, Anastazia Anyimike, Dodoma na Halima Mlacha, Ana Mwikola (Dar).

KAYA zilizobainika kuwa na historia ya kutochukua mara ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi