loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mitishamba yatajwa vifo vya wajawazito

WAKATI Kanda ya Ziwa ikitajwa kuongoza kwa vifo vya wajawazito, imeelezwa kuwa matumizi ya mitishamba ni chanzo kikuu cha ongezeko la vifo vya wajawazito mkoani Mwanza.

Hata hivyo, mkoa huo umeanza kufanya ukaguzi wa mitishamba kwa wajawazito wawapo wodini ili kuzuia kuitumia.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutachunzibwa wakati wa mahojiano maalum na HabariLeo.

Rutachunzibwa amesema ili kupunguza idadi ya vifo hivyo kutoka kwenye tarakimu tatu hadi tarakimu mbili na baadaye moja, inahitajika mkakati wa pamoja kati ya jamii na serikali.

Alisema vifo vingi ya wajawazito, vinasabishwa na utumiaji wa mitishamba ikiwemo mizizi ya bangi, mizizi ya tango, mwarubaini, mizizi ya mti wa muosha fedha na mizizi ya mgagani.

“Kwa kawaida mwenendo wa uchungu unatakiwa uje na kukata, kidogo kidogo ndani ya saa 10 na iwapo inatokea uchungu pingamizi labda mtoto amekaa vibaya au uchungu umekata, ndio tunamuongezea uchungu kwa taratibu,Sasa wao wanatumia mizizi ya mitishamba wasichelewe kuzaa, wapo wanaofanikiwa, lakini wapo wengi wanaopoteza maisha au kuzaa watoto wenye mtindio wa ubongo au watoto wenye matatizo ya upumuaji” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, vifo mkoani humo kuanzia mwaka 2016 vilitokea vifo 151, mwaka 2017 vifo 195 na mwaka jana 151.

Alisema kwa mwaka huu tangu Januari hadi Oktoba, tayari wajawazito 151 wamepoteza maisha, hiyo ina maana kila mwezi wastani wa wanawake 10 hadi 11 wanapoteza maisha.

“Ukiangalia takwimu hizo ni kubwa, mkakati wetu kama mkoa kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa (John Mongela) tumeanzisha kampeni ya kutoa elimu kwa jamii kufika kliniki kwa wakati ikiwemo madhara ya utumiaji wa mitishamba, tunatoa elimu pia kwa waganga na wakunga wa jadi,”alisema.

Alisema wanatoa elimu pia ya uzazi wa mpango, kwa kuwa matumizi ya uzazi wa mpango kwa mkoa huo, yapo chini kwa asilimia 22.

Kwa upande wake, Mratibu wa Afya Mkoa wa Mwanza, Cecilia Mrema alisema mkakati mwingine wanapambana kwa kufanya ukaguzi na kukamata dawa za mitishamba, ambazo wajawazito wanatumia wanapokuwa wodini kusubiri kujifungua.

“Baadhi ya ndugu wanawawekea kwenye chai au uji baada ya kubaini mizizi huwa tunaikamata, sasa tunachofanya mtu akileta chakula au chai, chochote anacholeta kwa mjamzito tunamlazimisha kuonja kwanza, akigoma tunambana mpaka anasema,” alisema Mrema.

Alisema madhara mengine ya matumizi ya mitishamba ni kupasuka kwa miji ya mimba na mama kupoteza maisha kwa kutokwa damu nyingi.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela alisema wanafanya kampeni kubw aya wananchi kuacha kutumia miti shamba kwenye kujifungua.

“Huku Mwanza kuna wanazengo, tunawatumia hao kuelimishana iwapo wataona mjamzito basi wamfuatilie kuhakikisha anahudhuria kliniki na pia kuacha matumizi ya mitishamba. Tunawapa elimu na mbinu wakunga wa jadi maana kuna watu bado wanawaamini na wanawatumia,”alisema.

Alisema pia ujenzi wa vituo 352 ndani ya miaka mitatu ndani ya mkoa huo, pia unasaidia huduma ya afya ya mama na mtoto kupatikana kwa urahisi, ingawa kuna changamoto hiyo ya imani katika jamii.

Kitaifa takwimu za Hali ya Vizazi na Vifo za mwaka 2018, zinataja mkoa wa Mwanza kuongoza kuwa na vifo vya wajawazito 151 ukifuatiwa na Morogoro (125), Geita (80), Kigoma (79), Mtwara (76), Mbeya (75), Tabora (69), Dodoma (67), Pwani (66) na Arusha (65).

KAYA zilizobainika kuwa na historia ya kutochukua mara ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi