loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Msiishie kujiandikisha, ombeni uongozi’

JANA Watanzania nchi nzima walianza kujiandikisha kwenye daftari la orodha ya wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu.

Kwa mujibu wa kanuni ya uchaguzi huo, uandikishaji na uandaaji wa orodha ya wapigakura utaanza siku ya 47 kabla ya siku ya uchaguzi na utafanyika kwa muda wa siku saba kwa kutumia fomu maalumu. Inakadiriwa kwamba Watanzania 26,960,485 watajiandikisha kwa ajili ya uchagizi huu, wanaume wakiwa ni 12,852,328 na wanawake ni 14,108,157.

Makadirio hayo ya idadi kubwa ya wanawake kujiandikisha kulinganisha na wanaume yanaakisi pia matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2102 yaliyoonesha kwamba wanawake ni wengi kulinganisha na wanaume.

Wakati wanawake wanaotarajia kujiandikisha ni kubwa kuliko wanaume na uzoefu umeonesha kwamba hata kwenye kupiga kura wanawake huwa wanajitokeza kwa wingi kupiga kura kuliko wanaume, lakini kwenye kugombea uongozi hali imekuwa ni tofauti. Wanawake ambao kuomba nafasi za uongozi kuanzia kwenye vyama vyao hadi kwenye uongozi wa jamii imekuwa ndogo kulinganisha na wanaume.

Ni katika muktadha huo, wanawake wanahimizwa kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, siyo hizi serikali za mitaa pekee bali hata ndani ya vyama vyao na chaguzi zinazofuata. Wakati mwaka huu nchi inafanya uchaguzi wa serikali za mitaa, mwaka kesho kutakuwa na uchaguzi mkuu na baadhi ya vyama ikiwemo chama kikuu cha upinzani nchini, Chadema, kinatazamiwa kufanya uchaguzi wake Desemba mwaka huu.

Ofisa programu kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Deogratius Temba, anasema ni vyema wanawake wasibaki kuwa wapiga kura na kuamini kwamba pengine nafasi za uongozi zanawastahili wanaume zaidi, jambo ambalo siyo kweli. Temba anatoa takwimu zinazoonesha kwamba wanawake katika serikali za mitaa waliopata uenyekiti kwa nchi nzima katika uchaguzi uliopita ni asilimia 3.3 tu, idadi anayosema ni ndogo sana.

Temba anasema mwaka 2015 uteuzi wa wagombea katika nafasi ya udiwani, wanaume walikuwa 10,046 huku wanawake wakiwa 670, sawa na asilimia 6.6. Anasema wanaume waliochaguliwa kuongoza kata ni 3,742 huku wanawake wakiwa 204, sawa na asilimia 5.6. Anasema ni vyema jamii ikaangalia tatizo liko wapi kama ni wapiga kura kutowachagua wanawake au wanawake kutojitokeza? Lakini anasema takwimu hizo zinaonesha kwamba wanawake wanaojitokeza kuwania nafasi za uongozi ni wachache.

Kuhusu ubunge, Temba anatumia takwimu za ofisi ya bunge zinazoonesha kwamba kuna wabunge wanawake waliopambana kwenye majimbo na kufanikiwa kupata nafasi za uongozi 25 tu, sawa na asilimia tisa ukilinganisha na wabunge wanaume waliogombea majimbo na kupita, ambao ni 239, sawa na asilimia 91. Kuhusu jamii, Temba anakiri kwamba imekuwa na mtamzamo hasi kuhusu kuongozwa na mwanamke.

Anasema bado kuna watu katika jamii ambao wanamwona mwanamke kama anayepaswa kubaki nyumbani akilea familia, kwamba ni mtu wa kuolewa na mambo kama hayo na hivyo kuitaka jamii kuondokana na mtazamo huo hasi. Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi, anasema wanapozungumzia ushiriki wa wanawake katika uongozi, jamii inatakiwa iangalie kwa mapana yake kwa kuwa ushiriki wa wanawake katika uongozi umekuwa na manufaa mengi wakati wote.

Lakini anasema tatizo pengine linaanzia pia kwenye vyama kwani katika vyama vya siasa 19 vilivyosajiliwa nchini hakuna ambacho kwa sasa mwenyekiti wa ngazi ya taifa ni mwanamke. Hata hivyo, Liundi anashukuru kwamba kwa mara ya kwanza tangu nchi ipate uhuru tuna makamu wa Rais mwanamke, Samia Suluhu Hassan na kwamba hiyo ni hatua ya kupongezwa.

Liundi anashukuru pia kwamba wakati wa bunge la kumi, nchi ilipata spika wa kwanza mwanamke kuliongoza, Anne Makinda na bunge la sasa la 11 lina naibu spika ambaye ni mwanamke, Dk Tulia Akson.

“Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazofanya vizuri katika ushiriki wa wanawake kwenye uongozi ukilinganisha na takwimu za Inter-Parliamentary Union (IPU) za hadi Januari 2019,” anasema Liundi Liundi anafafanua kwamba Tanzania inashika nafasi ya pili kwa nchi za Afirika Mashariki na nafasi ya 25 duniani kwa kuwa na asilimia 36.9 ya wanawake wabunge huku Rwanda ikishika nafasi ya kwanza hadi ya kidunia kwa kuwa na asilimia 61.3 ya wabunge.

Anasema hadi Januari 2019 takwimu zilikuwa zinaonesha kwamba maspika wanawake ni asilimia 19.7 na manaibu spika wanawake ni asilimia 28.2 duniani kote. Anasema kulingana na takwimu hizo wabunge wanawake katika nchi zote duniani walikuwa asilimia 24.3 hadi kufikia Januri hadi mwaka 2017 huku kwa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara kukiwa na wastani wa asilimia 23.7 za wabunge wanawake.

Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo mkoani Shinyanga, Siri Yassin anawashauri wanawake wenzake kutoogopa kujitokeza kuwania nafasi za uwakilishi wa wananchi kwenye serikali za mitaa kwani wanaweza. Yassin anasema amekuwa akijitahidi kuhamasisha wanawake kuchangamkia nafasi za uongozi lakini tatizo limekuwa ni wengi kutojiamini na wengine kukosa elimu ya kutosha kuhusu wajibu wa kiongozi.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Kishapu (CCM), Shija Ntelezu, anasema moja ya jambo ambalo wamekuwa wakisisitiza ni usawa katika uongozi na hivyo wanahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kuwania nafasi ya uenyekiti. Anakiri kwamba kwa sasa wilaya nzima hakuna mwenyekiti wa kijiji au kitongoji ambaye ni mwanamke.

Diwani wa kata ya Usule iliyopo halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Amina Bundala, anakiri kwamba alipoanza kugombea ilikuwa changamoto kutokana na jamii kumnyapaa, baadhi wakiwa na wasiwasi kwamba asingeweza kuongoza Anasema alianza kugombea nafasi huyo ya udiwani mwaka 2010 akisimama na wanaume watatu, yeye akiwa wanne na kwamba walimpitisha kwenye kura za maoni kama majaribo kuona kama mwanamke anaweza kufanya vizuri. Anasema kutokana na kufanya vizuri ndio maana mwaka 2015 wakamapatia tena ridhaa ya kuwaongoza.

Anakiri kwamba mwanamke anapoanza kuonyesha nia ya kutaka kugombea anakumbana vikwazo vingi ambapo hata watu wake wa karibu humkatisha tamaa mbali na manyanyaso ya kijinsia anayoweza kukutana nayo. Anasema katika kata yake yenye watu 5680 na vijiji vinne, hakuna mwenyekiti wa kijiji wala kitongoji lakini amekuwa akihamasisha wanawake wenzake kugombea nafasi za uongozi.

Getruda Masanja, mwenyekiti wa kijiji cha Buganzo, kata ya Ntobo katika halmashauri ya Msalala anasema alipata nafasi hiyo kwa kujaribu lakini baada ya kupita ametekeleza mengi na anaamini wananchi watamrejesha tena.

Mkuu wa wilaya ya Kahama, Annamringi Macha anawahimizi wanawake kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na kisha mwakani kwania nafasi za udiwani na ubunge. Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko naye anawahimiza wanawake kutolala na kudhani nafasi za uongozi zimeumbiwa wanaume na kwamba wanawake wengi wameonekana kuongoza vizuri kuliko hata baadhi ya wanaume.

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Kareny Masasy

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi