loader
JPM ameshinda mtihani wa kusamehe na kusahau

JPM ameshinda mtihani wa kusamehe na kusahau

BINADAMU ameumbiwa mitihani mingi, lakini moja kati ya mitihani hiyo ni kupewa uwezo wa kuhisi maumivu na hasira huku akiagizwa na Muumba wake kumsamehe anayemkosea na kumwombea mema adui anayepanga kumdhuru.

Huenda mtihani huu ndio uliosababisha mpigania uhuru wa India na mmoja kati ya wanafalsafa ambao fikra zao zinaishi ingawa miili yao ‘imelala’, Mahatma Gandhi kusema;

“Watu dhaifu hawawezi kusamehe, kusamehe ni kielelezo cha tabia ya watu imara.”

Falsafa hiyo ya Gandhi inaongezwa nguvu na mtu anayesamehe siyo kwa sababu hana namna ya kumwadhibu aliyemkosea, bali ana mamlaka yote na nguvu za kumuadhibu, lakini ameyavumilia maumivu na kumsamehe aliyemuumiza. Hivi karibuni, Rais John Magufuli ameonesha uimara wa hali ya juu, akiwasamehe watu ambao wameonekana au kusikika hadharani wakimkashfu au kumtukana.

Licha ya kuwa na nguvu kubwa anayopewa na Katiba ya Nchi kama Rais na Amiri Jeshi Mkuu, amejishusha akawakumbatia waliomtukana na kuwasamehe, ingawa amekiri kweli ‘inauma’.

Septemba 4, 2019, Rais Magufuli alipokuwa akifungua Mkutano wa Mwaka wa pamoja wa Wahandisi na Wasanifu Majenzi jijini Dar es Salaam, aliweka wazi kuwa amewasamehe Januari Makamba na William Ngeleja ambao walimkejeli na akajiridhisha kwa asilimia zaidi ya 100 kuwa, walitenda kosa hilo.

Januari Makamba amewahi kuwa mmoja wa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Tano uinayoongozwa na Rais magufuli, huku akiwa akliyewahi kuwa mmoja wa mawaziri katika serikali ya awamu ya Nne iliyoongozwa na Jakaya Kikwete.

Kama hiyo haitoshi, siku chache baadaye mbunge wa Mtama, Nape Nnauye naye alipokea msamaha wa Rais Magufuli kwa kosa kama hilo. Rais alimwalika Ikulu, akamsikiliza, akamsamehe hadharani na zaidi akampa ushauri wa namna ya kupiga hatua kwenye maisha yake ya kisiasa.

Akamtia moyo na kumwondoa wasiwasi! Hii ni ishara kuwa, Rais Magufuli amefanikiwa kuushinda mtihani ule wa binadamu, ameonesha uimara na kuyaashi maandiko ya Mungu anayoyasoma, ingawa anakiri inauma.

“Inauma, kusamehe kunaumiza, lakini ninasema kwa dhati kabisa kwamba nimemsamehe,” anasema Rais Magufuli akitangaza msamaha wake.

Katika Biblia Takatifu, neno ‘msamaha’ kwa lugha ya Kigiriki limeandikwa zaidi ya mara 146, na kwenye Quran Takatifu msamaha umetajwa zaidi ya mara 100 na rehema (ambayo huzaa neno ‘huruma’) takribani mara 200.

Hii inaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anasisitiza kusameheana. Ni maneno matatu makuu yanaweza kuiokoa dunia nzima, ‘msamha, upendo na rehema’.

“Unisamehe makosa yangu, kama ninavyowasamehe walionikosea.”

Huu ndio mstari wa Biblia Takatifu, unaopatikana kwenye sala maarufu ya ‘Baba Yetu’ anayoifundisha Yesu Kristo kwa wanafunzi wake, mstari ambao Rais Magufuli alieleza kuwa aliutafakari alipokuwa anausema anaposali na akaamua kuwasamehe waliomkosea. Je, kukasirika ni dhambi? La hasha, kukasirika siyo dhambi kwani hataMwenyezi Mungu hukasirika.

Watu humuudhi Mungu, na watu huudhi watu, lakini Mungu aliyesema hata kama dhambi zako ni nyekundu kama bendera zitakuwa nyeupe kama theluji atakapokusamehe na anatutaka tuishi hivyo katikati ya maudhi na hasira. Lakini matunda ya hasira yanaweza kuwa dhambi.

Biblia inasema, “kuweni na hasira lakini msitende dhambi, jua lisichwe na uchungu wenu bado haujatoka (Waefeso 4:26).”

Katika Quran Tukufu pia, inaeleza jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anampenda mtu anayeweza kudhibiti hasira zake na kuwasamehe wenzake (Kurani: Surat Imran: 133-134). Kurani pia inasema katika Kuran: “...Na kusameheana ndiko kulio karibu zaidi na uchamungu. Wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda. (Surat Baqara: 263).

Mwenyezi Mungu pia anasema: “Kauli njema na usamehevu (kusamehe) ni bora kuliko sadaka inayofuatiliwa na maudhi. Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kujitosha na mpole. (Surat Baqara: 263). Kila mtu ‘akivaa viatu’ vya Rais Magufuli ni dhahiri atahisi maumivu aliyoyapata kutokana na lugha za ukakasi, lakini kwa ungwana na unyenyekevu wa kiroho, akaamua kwamba ‘jua lisichwe akiwa hajatoa uchungu wa maumivu’. Ukiacha mbali kusamehe saba mara sabini kama alivyoeleza Bwana Wetu Yesu Kristo, Mwenyezi Mungu anatuagiza kusamehe na kusahau.

Rais Magufuli ameonesha hilo pia anasema: “Nimawasamehe Nape, Makamba na Ngeleja na nimesahau.”

Kwa kutamka hivyo, Rais anaonesha kuwa hajabaki na chembe ya kinyongo na tena amemwalika Ikulu Nape kama mgeni wake wa heshima na siyo mtu anayetaka kumpigia goti.

Mwanafalsafa mmoja alipata kusema: “Dunia ingekuwa sehemu salama zaidi ya kuishi kama watu wangekuwa wanasameheana.” Hata hivyo, Nape, Makamba na Ngeleja waliokosea wametufundisha somo kubwa la uwazi. Kwanza, kukosea tumeumbiwa binadamu. Hata Petro aliyepewa hadhi na Yesu kuwa ndiye ‘Jiwe’ ambalo juu yake atajenga Kanisa lake, alimkosea Yesu, lakini alipojuta na kutubu, alisamehewa. Mafundisho ya vitabu pia yanasema hata Baba yetu Adam na mkewe Hawa walikosea kwa kula tunda walilokatazwa, lakini wakaomba toba na kusamehewa. Marehemu Bruce Lee, aliyekuwa mcheza karate na kung fu, aliwahi kusema: “Makosa husamehewa daima, kama mkosaji atakuwa na ujasiri wa kuyakiri.”

Makamba, Ngeleja na Nape walikuwa na ujasiri wa kuyakiri makosa yao na kuomba msamaha kwa dhati. Nape amekuwa funzo zuri, ni kama Mungu amemtumia pia kutukumbusha binadamu siyo tu kuomba msamaha, bali pia kuitafuta kwa dhati nafasi adhimu ya kuomba msamaha kwa tuliowakosea.

“Nape amekuwa akiomba msamaha, akiandika messages (ujumbe mfupi wa mandishi) hata usiku wa manane, alikuwa anaomba anione… anione. Hata wasaidizi wangu wamekuwa wakiliona hili,” anasema Rais Magufuli.

“Amehangaika sana, ameenda hadi kwa Mzee Mangula [Philip Mangula], amefika mpaka kwa Mama Nyerere, amehangaika kweli lakini baadaye… Ni katika hiyohiyo kwamba sisi tumeumbwa katika kusamehe. Na leo umemuona asubuhi amekuja hapa, nikaona siwezi kumzuia kuniona, kikubwa anachozungumza ni ‘naomba Baba unisamehe,” anaongeza Rais Magufuli.

Wengine wasio na busara wameeleza utetezi wa kufunika makosa kuwa eti makosa yale yalifanywa kwenye faragha hivyo aliyeyafichua ndiye mkosaji!! Wanasahau kuwa hata Mungu wetu anajua kuna faragha, na Mungu pia yuko sirini. Hata hivyo, kuwa sirini hakumpi mtu yeyote ruhusa ya kufanya makosa. Kosa ni kosa haijalishi umelifanya kwa mazingira yapi, muhimu ni kukiri, kujuta na kuomba msamaha kama walivyofanya wanasiasa hao. Kufanya kosa hakukuondolei hadhi yako endapo utakiri, kujuta na kuomba msamaha, bali litabaki kuwa fundisho kwa wengine.

Mfano, katika Biblia, Mungu alimfanya Mfalme Daudi kuandika makosa yake mwenyewe na hadi leo tunayasoma. Aliyafanya, alikiri, akajuta, akatubu, akasamehewa na akabaki kuwa ni mteule wa Mungu.

Kwa haya yaliyotokea, ni dhahiri Rais Magufuli ameyaishi Maandiko Matakatifu na ameongoza kwa kuwa mfano bora zaidi. Tuendelee kumuombea rais wetu. Tupo wengine huku mtaani, mbavu mbili tu na hata uongozi wa darasa hatujawahi kupata, lakini tunavyopania kulipa visasi ni kama tuna mkataba na shetani. Tujifunze kwa rais wetu, vitabu vyote vitakatifu vinaelekeza kusamehe na kuepuka visasi. Mwandishi wa makala haya kutoka mtandao wa Dar24 ni mchangiaji wa gazeti hili

foto
Mwandishi: Joseph Muhozi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi