loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Miaka minne ya JPM na wingi wa mafanikio

SIKU zinakimbia! Tena zinakimbia mithili ya maji yatiririkayo kwenye maporomoko ya bonde refu. Wakati siku zikikimbia, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli nayo iko mbio kujenga mafanikio kwa vizazi na vizazi.

Haya ni mafanikio yasiyoweza kufutwa kwa kalamu wala maneno, maana pamoja na kila jicho kuona, hata visivyoonekana bila shaka vinashuhudia na vijavyo vitayaishi mema haya.

Lengo la mbio hizi ni kutufikisha katika mageuzi makubwa ya kutupeleka kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025 na kuna dalili za nchi hii kuwa nchi mfadhili katika kipindi chake cha uongozi.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na baraza la mawaziri, wanamsaidia kwa karibu kuhakikisha mbio hizi zinazofanyika kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zinakamilika kwa ushindi wa medali ya dhahabu. Katika siku takriban 1,460 za Rais Magufuli na serikali yake tumeshuhudia mageuzi makubwa yakitamalaki nchini katika sekta ya afya, elimu, miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, usafiri wa anga, majini, sera ya uanzishwaji wa viwanda, ukusanyaji wa kodi na ulinzi wa rasilimali za taifa kama madini na maliasili kwa maslahi mapana ya Watanzania.

Serikali hii inazielekeza halmashauri zote nchini kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Hatua hii ipo kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290 katika Kifungu cha 37 (a), inayolenga kutoa mikopo isiyo na riba ili kuyajengea makundi hayo uwezo kiuchumi kwa kufanya shughuli za ujasiriamali.

Halmashauri ya Mji wa Kibaha imeitikia agizo hili na kutekeleza kwa vitendo kwa kutoa kwa walengwa zaidi ya Sh milioni 400. Mafisadi waliozoea kujimilikisha rasilimali za Watanzania kinyemela sasa wamebaki na kauli za kubeza baada ya mianya ya rushwa kuzibwa.

Albert Einstein, mshindi wa tuzo ya Nobel mwaka 1921, Mjerumani mbobezi wa Fizikia aliyezaliwa Machi 14 mwaka 1879 na kufariki Aprili 18, 1955 aliwahi kusema: “Jitahidi kila unachofanya kisikupe mafanikio tu, bali kikupe thamani”.

Kauli hii inadhihirisha wazi kuwa, Rais Magufuli katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake ameonesha siyo tu mafanikio, bali thamani ya Tanzania na Mtanzania katika anga za kimataifa kwenye nyanja mbalimbali.

MAPATO YA KODI

Mwanaharakati wa nchini Marekani, Helen Keller amewahi kusema: “Mlango mmoja wa furaha ukifungwa, mwingine hufunguliwa, lakini binadamu huangalia kwa muda mrefu mlango uliofungwa na hawezi kuona ule uliofunguliwa kwa ajili yake.”

Serikali ya Awamu ya Tano ilipofunga mlango wa ufisadi na kusisitiza kila Mtanzania kulipa kodi, hakika huu ulikuwa kama utamaduni wa kigeni kwa walio wengi tena usiotekelezeka.

Neema za sera ya elimu bure, kuboreshwa kwa huduma za afya, ununuzi wa ndege, ujenzi wa barabara, reli, madaraja na bwawa kubwa la kufua umeme la Julius Nyerere Hydropower Rifiji, lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 na neema nyingine nyingi, zilifunguliwa.

Ni kipindi hiki ambacho makusanyo ya mapato ya kodi yameongezeka maradufu kutoka wastani wa Sh bilioni 850 mpaka wastani wa Sh trilioni 1.3 kwa mwezi.

Kwa mfano, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Septemba pekee imevunja rekodi kwani tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996 kwa mara ya kwanza imekusanya Sh trilioni 1.767 kwa mwezi.

Aidha, ukusanyaji kodi kwa ufanisi katika utawala huu unaendelea kuonekana katika halmashauri 195 nchini baada ya kukusanya asilimia 90 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ikilinganishwa na asilimia 81 ya mwaka 2017/2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia tisa. Sh bilioni 661.4 zimekusanywa kati ya malengo ya kukusanya Sh bilioni 723.7.

Hivi Karibuni, akiwasilisha makusanyo na matumizi ya mapato hayo kwa waandishi wa habari, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo alionesha kufurahishwa na hatua hiyo hasa kwa Sh bilioni 211.6 sawa na asilimia 32 kutumika kwenye miradi ya maendeleo. VIWANDA Sekta ya Viwanda imeendelea kukua kwa kasi.

Mwaka 2015 ilikuwa kwa asilimia 6.5 na kuchangia Pato la Taifa (GDP) kwa asilimia 5.2 wakati mwaka 2018 ilikuwa kwa asilimia 8.3 na kuchangia pato la taifa kwa asilimia nane.

Serikali imeongeza juhudi za kufufua viwanda vya zamani na kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vipya kwa kuweka sera na mazingira rafiki. Katika kutekeleza hilo, Serikali iliagiza kila mkoa kuhakikisha unakuwa na viwanda visivyopungua 100 na utekelezaji unaendelea.

Mathalani katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuna viwanda vikubwa na vidogo vipatavyo 42 na viwanda vidogo sana vikiwa zaidi ya 200.

Vyote vikiajiri Watanzania zaidi ya 6,000. Takwimu zinaonesha kwa sasa kuna viwanda 53,876 nchini. Kati yake 251 ni vikubwa, 173 ni vya kati, 6,957 ni vidogo na 46,495 ni viwanda vidogo sana.

AFYA

Miaka minne ya Rais Magufuli imeleta neema ya matibabu kwa Watanzania vijijini na mijini. Mbali na kupeleka wataalamu wengi kwenye hospitali mpaka zahanati, tumeshuhudia mapinduzi makubwa ya uboreshaji wa miundombinu kwenye sekta ya afya ambapo serikali imetoa Sh milioni 500 kwa ajili ya upanuzi wa vituo vya afya.

Rais Magufuli amewezesha upanuzi wa vituo 352 vya kutolea huduma za afya vilivyopo katika hatua mbalimbali ya ukamilishwaji na kufanya jumla ya vituo vya kutolea huduma kufikia 7,284.

Kwa mujibu wa mpango wa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya ya msingi katika mamlaka za Serikali za Mitaa uliochapishwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), mwaka 2019 unaonesha kuwa vituo 304 vitatoa huduma ya dharura na upasuaji. Vituo vya afya 119 vimekamilika, kati ya hivyo 58 vimeanza kutoa huduma za upasuaji.

Halmashauri ya Mji Kibaha imenufaika na mpango huo kwa kupata kiasi cha Sh bilioni mbili ambapo Sh milioni 500 kwa ajili ya upanuzi wa kituo cha afya Mkoani na ujenzi wa hospitali ya Wilaya ikipewa Sh bilioni 1.5. Wananchi 155,160 watanufaika na matibabu ikiwemo huduma za kibingwa na rufaa kutoka kwenye zahanati. Aidha, kitaifa Serikali imejenga hospitali mpya za wilaya 67 zilizogharimu Sh bilioni 100.5.

Hii ni historia mpya kwani tangu nchi ipate uhuru ilikuwa na hospitali za wilaya 77 pekee. Serikali kwa mwaka huu 2019 imefikisha hospitali za wilaya 144 tena utekelezaji wake ukifanyika ndani ya miezi sita tu.

Kupitia maboresho ya sekta hiyo na kuendelea kuwasomesha wataalam wa kutosha wa kibingwa, sasa mahitaji ya CT Scan, MRI, utambuzi wa DNA, upandikizaji wa figo, unafanyika nchini tofauti na nje kama ilivyokuwa awali.

SEKTA YA NISHATI

Ndani ya miaka minne ya utawala wake, Rais Magufuli amekuja na uamuzi mgumu na wa kuushangaza ulimwengu. Tatizo la nishati ya uhakika nchini linakwenda kuwa historia baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa kufua umeme katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji utakaozalisha megawati 2,115, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961. Serikali pia imeendelea kupeleka umeme vijijini kwa kasi.

ELIMU BURE

Serikali imeendelea kutoa elimu bila malipo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari (kidato cha nne), ambapo zaidi ya Sh bilioni 920 zimeshatolewa kwa ajili ya ada.

Ni kipindi ambacho idadi kubwa ya wanafunzi wameandikishwa kuanza darasa la kwanza.

Kwa mfano, kwa shule za msingi kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha mwaka 2019, watoto 5,172 (wavulana 2,625) na (wasichana 2,547) waliandikishwa ikilinganishwa na watoto 2,944 (wavulana 1,390) na (wasichana 1,554) waliaoandikishwa mwaka 2015.

Wingi huu wa wanafunzi umleta changamoto ya miundombinu ya madarasa na samani. Watawala sasa wanakuna vichwa ili kuwawekea watoto mazingira mazuri ya kujifunza. Hata hivyo, bado serikali imewajibika kwa kuja na utaratibu mpya wa EP4R ili kukamilisha majengo ya madarasa.

Waraka wa Elimu Na.5 wa mwaka 2015, unaohusu elimu bila malipo, unampa fursa mwanafunzi kusoma na kupata elimu bila mzazi au mlezi kulipa ada wala michango ya fedha iliyokua inatozwa shuleni kabla ya waraka huo.

Waraka huu sasa unatekelezwa kwa vitendo. Aidha, Waraka wa Elimu Na.3 wa Mwaka 2016 unasisitiza utekelezaji wa elimu ya msingi bila malipo nao unatoa mwongozo wa namna ya utekelezaji kulingana na Sera ya Elimu na mafunzo ya Mwaka 2014 iliyozindulia Februari 13, 2015 na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete. Sera hii inalazimisha elimu ya awali kutolewa kwa mtoto kuanzia miaka mitatu mpaka mitano kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Innocent Byarugaba

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi