loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali yaanza utafiti mafuta Bonde la Eyasi

SERIKALI imeanza kufanya utafi ti wa mafuta katika Bonde la Eyasi Wembere, kwa kufanya uchorongaji wa visima vitatu, vyenye urefu wa mita 300 kila kimoja. Utekelezaji huo unaofanywa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa kutumia wataalamu wa kampuni za ndani kwa gharama ya Sh milioni 300.

Inaelezwa kuwa kisima namba moja, kitachorongwa katika Kijiji cha Kining’nila Wilaya ya Igunga, huku namba mbili na tatu vitachorongwa wilaya za Meatu mkoani Shinyanga na Iramba mkoani Singida. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa uchorongaji wa kisima namba moja, Meneja Utafutaji wa Mafuta na Gesi kutoka TPDC, Venosa Ngowi alisema utafiti huu unakuja kufuatia ukusanyaji taarifa za bonde hilo, uliofanyika mwaka 2015 kwa kutumia ndege maalumu.

Baada ya utafiti huo wa kutumia ndege, ilibainika kuwa katika eneo hilo ulionesha eneo la Bonde la Eyasi Wembere, lina miamba tabaka mizuri inayoweza kutumika kwa utafutaji mafuta na gesi. Hivyo, uchorongaji huo wa visima vifupi vya utafiti ni awamu ya pili ya utafiti, ukifuatia ule wa mwaka wa fedha 2015/2016. Meneja Mradi wa Utafutaji Mafuta katika Bonde la Eyasi Wembere, Sindi Mduhu alisema eneo la bonde hilo, linalotambaa katika mikoa ya Manyara, Singida, Simiyu, Tabora na Arusha lina kila dalili ya mafuta.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio aliyefika eneo la utafiti, kujionea jinsi uchimbaji huo unavyoendelea na kuuzindua rasmi, alisema utafiti huo unafanyika kwa matumaini kuwa Tanzania inaweza kugundua mafuta. Katika ushirikishaji kampuni za ndani katika utafiti huo, Dk Mataragio alisema kazi hiyo inafanywa na TPDC kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambalo ni mkandarasi mkuu katika mradi huo. Alitaja sifa za maeneo ambayo kuna uwezekano wa ugunduzi wa mafuta kuwa ni maeneo ya Bonde la Ufa na kama ilivyo nchini Kenya katika eneo la Lokcha au Turkana, walipogundua mafuta.

Vilevile Uganda katika Ziwa Albert, ambalo lipo katika Bonde la Ufa nao wamegundua mafuta. Dk Mataragio alibainisha kuwa utafiti wa kutumia ndege zilitumika Sh bilioni 2.4, zote zikiwa fedha za ndani za serikali. Mwenyekiti wa Kijiji cha Kining’inila, Christopher Njilezengo kunakofanyika utafiti, alipongeza serikali kwa kuwekeza katika mradi huo, kwani utakuwa na tija ikiwa nchi itafanikiwa kupata mafuta. Utafiti huu unafanyika ikiwa ni miaka miwili baada ya Rais Magufuli na Rais Yoweri Museveni wa Uganda kutia saini Mkataba wa mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania.

KAYA zilizobainika kuwa na historia ya kutochukua mara ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Igunga

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi